NYERERE ASITISHA ZOEZI LA USAFI MUSOMA
Zoezi la kuweka Manispaa ya Musoma mkoani Mara katika hali ya usafi,kwa kuwandoa wafanyabiashara ndogo ndogo,limeingia dosari baada ya mbunge wa Musoma Mjini Mh Vincent Nyerere, kuamuru kikosi kazi cha maafisa afya na wakaguzi wa mji kulisitisha mara moja baada ya kubaini kuwa zoezi hilo halina baraka za madiwani wa Manispaa hiyo.
Kati zoezi hilo ambalo lilianza kufanyika katika maeneo ya kituo cha mabasi, mitaa ya soko kuu ,chini ya usimamizi wa Afisa Afya Mkuu wa Manispaa ya hiyo Bw. Peter Mtaki akiwa na ulinzi wa askari wa Manispaa, Maafisa Afya na Wakaguzi wa Mji lilisimamishwa ghafla baada mbunge huyo kubaini kuwa hakukua na sababu za kuwandoa wafanyabiashara wagodo kabla ya kuwatengea eneo mbadala.
Hata hivyo wakati maafisa hao wakianza kuondosha mabanda yanayodaiwa kuwekwa kiholela sehemu zisizostahili ghafla lilizimwa na mbunge huyo wa Musoma Mjini Mh Vincent Nyerere na kusema hakuna mtu atakayeondolewa eneo hilo kwa vile machinga hao hawajaelekezwa mahali pa kwenda.
Nao baadhi ya wafanyabiashara hao ndogo ndogo, maarufu kama machinga wamelazimika kuvunja ukimya baada ya kuona vibanda vyao ambavyo wamekuwa wakivitumia kujipatia riziki vikisombwa na kuwekwa ndani ya gari la Manispaa lenye namba za usajili STK 5448 aina ya Isuzu Tipper na kitendo hicho cha vManispaa kinalenga kuwanyanyasa na kuwakata mitaji.
Mmoja ya wafanyabiashara hao Bi Vaileth Mafuru, mkazi wa Nyakato amedai kwamba kama serikali inaona kazi wanayoifanya vijana hao ni uchafuzi wa mazingira, ni bora waruhusiwe kuendesha biashara haramu ya ngono, huku huku Bw James Mwita mkazi wa Kigera akitahadhalisha uwezekano wa kuibuka tena kwa vikundi vya uhalifu, kama vile mbio za vijiti, mdomo wa furu na Jamaica kutokana na vijana kuishi bila ajira.
Afisa Afya Mkuu wa Manispaa ya Musoma Bw. Peter Mtaki, akizungumza kwa unyonge amesema hatua ya mbunge kulipiga stop zoezi hilo, ni kuchanganya siasa na utendaji, hivyo jambo hilo limewakatisha tamaa ya kutekeleza majukumu yao ya kuhakikisha mji unakuwa safi.
Hivi karibuni madiwani wa Manispaa ya Musoma walifanya ziara ya mafunzo katika Manispaa ya Moshi kujifunza hali ya usafi, katika manispaa hiyo,ziara ambayo imegharimu mamilioni ya fedha za walipa kodi kwaajili ya kujifunza namna bora ya kuweka mji katika hali ya usafi.
Mji wa Musoma ambao kuanzia mwaka 1993 uliwahi kushika nafasi ya kwanza mfululizo kwa miaka 6 kwa usafi wa miji nchini, sasa umepoteza mwelekeo baada ya uchafu kuendelea kuzagaa kila kona ya mtaa wa mji huu hivi sasa.
No comments:
Post a Comment