Saturday, June 4, 2011

WATENDAJI WATAKAOSHINDWA KUPELEKA TAARIFA TAMISEMI KUKIONA

Musoma
 
Serikali imewaagiza watendaji wake wakuu katika ngazi za wilaya kutoa taarifa za utekelezaji wa kazi zao kwa kwa chama cha mapinduzi CCM katika wilaya husika kila wanapotakiwa kufanya hivyo.

 
Aidha watendaji wa ccm pia wametakiwa kutoa taarifakwa mamlaka za serikali hasa TAMISEMI kuhusu watendaji watakashindwa kufanya hivyo ili waweze kuwajibishwa.
Kauli hiyo ya serikali ilitolewa mwishoni mwa wiki na naibu waziri wa TAMISEMI Aggrey Mwanri wakati akizungumza na wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwamo madiwani na watendaji wa halmashauri ya Manispaa ya Musoma katika ukumbi wa kanisa katoriki mjini hapa.

 
Alisema kuwa watendaji hao wanapaswa kutambuwa serikali iliyopo madarakani inatekeleza ilani ya chama tawala cha CCM kilichopewa ridhaa na wananchi kupitia uchaguzi mkuu hivyo hawana budi kutoa taarifa za utekelezaji wa ilani hiyo kila wanapotakiwa.
“Najua wengine mkisikia huyu katibu wa CCM akimwita mkurugenzi ofisini kwake na kuhoji hayo mnaweza kushangaa na kupiga kelele ndivyo inavyotakiwa hata kama CHADEMA,CUF au TLP ndio wengekuwa wamepewa ridhaa hiyo wengefanya hivyo hata kule Marekani nao wanafanya hivyo”alisema Mwanri.
Alisema endapo watendaji wa serikali watabainika kuficha ama kushindwa kutoa taarifa za utekelezaji wa ilani kwa kwa ccm,mamlaka iliyoweka madarakani haitashindwa kuwachukulia hatua kali zinazostahili.

 
“Lazima watendaji wa serikali,mkuu wa wilaya na mkurugenzi mtoe taarifa kwa uongozi wa CCM wa wilaya yenu juu ya namna mlivyotekeleza ilani yao waliyowakabidhi baada ya kushinda uchaguzi,”alisema
Alisema ni wajibu wa chama tawala kufahamu kila hatua iliyofikiwa na serikali yake katika utekelezaji wa ilani ya uchaguzi inayopaswa kutekelezwa na halmashauri zote hata zile zinazotawaliwa na madiwani wa upinzani na hivyo sharti watendaji hao wa wilaya wakipatie chama hicho taarifa hiyo katika wakati uliopangwa bila kusita.

 
Katika kuharakisha maendeleo ya halmashauri za wilaya hapa nchini Mwanri aliwataka madiwani kuondokana na tofauti zao za kisiasa pindi wanapojadili juu ya uwajibikaji wa halmashauri zao katika kuwahudumia watu wake badala yake washikamane kwa pamoja wakijua kuwa wanachohitaji wananchi ni maendeleo na wala siyo malumbano yao ya kisiasa aliyosema yalikufa mara tu baada ya uchaguzi.

 
“Tunapojadili maendeleo tuachane na malumbano ya vijiweni wala yaliyojitokeza wakati wa uchaguzi,hayo yalishapitwa na wakati,ndani ya halmashauri mle hakuna vyama tofauti,sote chama chetu kinapaswa kuwa kile kiitwacho maendeleo,”alisema Mwanri.

 
Mapema katika taarifa yake mkurugenzi mtendaji wa Manispaa hiyo Nathan Mshana alisema pamoja na kukabiliwa na changamoto kadhaa katika kuwahudumia wakazi wake manispaa hiyo imefanikiwa kutoa huduma za kijamii kama elimu;afya na maji katika kiwango cha kuridhisha huku ikifanya jitihada zaidi ili kuhakikisha kuwa inawaboreshea watu wake maisha kama ilani ya CCM inavyoelekeza.

 
Mwisho

No comments:

Post a Comment