Saturday, February 26, 2011

WANANCHI WALILIA MASHAMBA YAO

Musoma

WANANCHI wa kata ya Bugwema katika halmshauri ya Musoma vijijini,wametoa madai mazito dhidi ya viongozi waandamizi wa wilaya ya Musoma na mkoa wa Mara kwa kuwatuhumu kuwa wamekuwa wakila njama kwaajili ya kuwapora shamba la Bugwema ambalo awali lilikuwa likitumiwa na jeshi la kujenga taifa J KT.

 
Wakizungumza katika mkutano huo uliofanyika katika senta ya kijiji cha Bugwema ambao waliuitisha wenyewe ili kutoa kero hiyo kwa mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Nimrod Mkono,wananchi hao walisema hivi sasa wanakabiwa na njaa kutokana na kukosa maeneo ya kilomo huku serikali ikishindwa kuwarusu kulima katika shamba hilo ambalo awali walilikabidhi kwa JKT kabla ya kushindwa kuliendeleza,

 
“Kwanza alikuja katibu tarafa hapa kijijini akituambia eti katumwa na mkuu wa wilaya tukubali shamba hili ligawawenywe ama serikali ilichukue tulikataa akaondoka baada ya siku kadhaa akaja DC mwenyewe tena kwa vitisho kwamba lazima wachukue shamba hili sisi tulimwambia hatuko tayari kukubali kwa vile hatuna maeneo ya kilimo sasa wewe kama mbunge unatusaidiaje ili kutatua tatizo hili”alisema Faustine Thamas.

 
Walisema viongozi hao ambao ni mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya wamekuwa wakitoa kauli za kuwachanganya juu ya shamba hilo huku wakidai kuwa tayari limepata mwekezaji jambo ambalo linawashangaza hasa ukizingatia kuwa hivi sasa hawana maeneo ya kilimo.

 
Akisoma taarifa kwa niaba ya wananchi hao afisa mtendaji wa kijiji hicho Julius Mtongori,alisema kijiji hicho kinakabiliwa uhaba mkubwa wa chakula kutokana  wananchi kukosa maeneo ya kilimo hivyo kumuomba mbunge huyo kuwasadia ili kunusuru maisha ya wananchi.

 
“Mh Mbunge tumekuita kukueleza hapa tunakabiliwa na njaa hivi sasa ambayo inaytokana na kukosa maeneo ya kilimo kwani tunalazimika kuomba maeneo ya kilimo kutoka shamba la JKT ambalo kimsingi ni mali yetu”alisema kiongozi huyo wa kijiji.

 
Naye mmoja wa madiwani katika halmashauri ya Musoma vijijini ambaye ni miongoni mwa viongozi waliokuwa katika mkutano huo Ruti Mayamba,alisema wako tayari kupoteza maisha hata kwa kupigwa risasi lakini kutetea wananchi hao kupata haki yao ya kumiliki shmba hilo.

 
Hata hivyo akiongea na wananchi hao mbunge Mkono,pamoja na kuonesha kusikitishwa na malalamiko hayo ya wananchi aliwaomba viongozi hao wa serikali kuacha kutumia nguvu kuwanyika haki wananchi wanaowaongoza.

 
“Mimi siamini mtu kama DC au RC anakuja bila kushirikisha watu na kulazimisha kuchukua shamba nadhani watambue kuwa wanawajibu wa kuwasadia wananchi wao si kuendekeza uekezaji ambao hauna tija kwa wananchi..hivi kweli unawezaje kusema unaleta wawekezaji bila kuchangia kwanza ujenzi wa shule,zahanati na kuwapatia wananchi maji hivi huu sio wizi mimi nitaenda kuongea nao kujua ukweli wa jambo hili”alisema Mkono.

 
Mkono ambaye alipokelewa kwa mabango yalikuwa yamebebwa na wananchi hao yenye ujembe mbalimbali kuhusu mgogoro wa shamba hilo,alisema aliwahi kuwa waziri mkuu Edward Lowasa alitoa uamuzi huo shamba hilo kurudishwa kwa wananchi baada ya JKT kuacha kuliendeleza hivyo endapo kuna wawekezaji lazima wananchi washirikishwe.
“Mwalimu Nyerere aliwahi kusema ukikuta kuku laki moja barabarani hata ukiwa mwendawazimu kamwe huwezi kuwakanyaga lazima usimame wapiti kwanza sasa iweje leo DC na RC ambao ni watumishi wenu waje kwa vitisho je hao wawekezaji wakiwapa shamba watashirikiana na nani hapa kama hakuna mahusiano”alihoji mbunge Mkono.

 
Hata hivyo alisema pamoja na kwenda kuzungumza na viongozi hao aliwahidi wananchi kulifikisha suala hilo kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye alidai tayari alishajulishwa kuhusu shamba hilo ili aweze kulitolea uamuzi na kuondoa mgogoro huo.
Akizungumzia suala hilo kwa njia ya simu jana,mkuu wa wilaya ya Musoma Kapteni Mstaafu Geofrey Ngatuni,alisema si kweli aliwahi kutoa vitisho juu ya shamba hilo bali aliwahi kuwashauri wananchi jinsi ya kutumia shamba hilo.

 
“Kwanza sikwenda kule mara tatu kama walivyodai nilikwenda mara moja kwaajili ya kuwaelimisha juu ya umuhimu wa kutumia shamba hilo je hapo kuna vitisho”alisema Dc Ngatuni.

 
Mkuu wa mkoa wa Mara alipotumiwa ujumbe mfupi wa maadishi kuhusu madai hayo ya wananchi alipiga simu na baada ya kutaka kuelezwa kuhusu jambo hilo alijibu kwa mkata wewe ni Marato basi niko kikaoni.

 
Kuna taarifa zisizo rasimi kuwa kuna mmoja ya watu kutoka nje amekuwa akitumia baadhi ya viongozi kutaka kupewa shamba hilo hata pasipokuishirikisha halmashauri ya Musoma vijijini na kijiji husika jambo ambalo sasa linazua shaka kuhusu uwekezaji huo.

No comments:

Post a Comment