MUSOMA
LEO Oktoba14 mwaka 2010 wananchi wa Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla wanakumbuka miaka 11 tangu kufariki Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mtetezi wa wanyonge.
Katika jambo lolote,kitu chochote au mtu yeyeto ambaye amewahikutenda jambo jemana jamii ikalikubali ni vigumu kusahaulika na ndio maana leo kama ilivyo kwa watanzania kumsahau mwalimu Nyerere baada ya kifo chake kwa miaka 11
Katika miaka kumi na moja ya kifo chake watanzania bado wanasema kuna pengo kubwa ambalo kamwe ni vigumu kuzibika kwani hajatokea kiongozi ambaye anaweza kufananishwa naye hasa katika kutetea haki za wananchi wake na bara la Afrika kwa ujumla.
Na kama leo tutawaeleza watanzania nin wangapi ambao wanakumbuka kwa vitendo yale aliyotenda Baba wa Taifa ni vigumu kumkosa mtu,katika hilo wapo wengi lakini miongoni mwa watanzania hao ni pamoja na mwalimu James Irenge ambaye alikuwa mwalimu wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika shule ya msingi Mwisenge ya mjini Musoma mkoani Mara.
Niliongea na Mwalimu Irenge kwake
Mwalimu Irenge akifanya mahojiano na mwandishi wa gazeti hili nyumbani kwake maeneo ya Mwisenge mjini hapa anasema kuwa alianza kumfahamu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1934 wakati alipokwenda kuanza darasa la kwanza katika shule hiyo ambapo yeye alimfundisha Mwalimu Nyerere mwaka 1935 darasa la tatu mwaka mmoja baada ya kuvushwa darasa la tatu kutokana na uelewa wake kuw mkubwa darasani.
Katika shule hiyo ya Mwisenge Mwalimu Irenge alimfundisha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere darasa la Tatu somo la Kiswahili,Hisabati na siasa ambapo anasema ingawa Mwalimu Nyerere alikuwa anayamudu vyema masomo yote lakini somo la siasa ndilo somo ambalo mwalimu alikuwa akipenda sana kusoma na kumudu vizuri darasani.
Anaongeza kuwa katika nyakati hizo za ukoloni ilimlazimu kumfundisha mwalimu somo hilo nyakati za usiku kutokana na wakoloni kutopenda wanafunzi wa Tanganyika(Tanzania) kufundishwa masomo hayo.
Mwalimu Irenge akiwa Kitandani
Pamoja na kumfundisha masomo ya siasa Mwalimu Irenge ambaye kwa sasa ana miaka (120) ambapo imekuwa vigumu hata kukaa na muda wote kushinda amelala anasema kuwa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alikuwa na tabia moja ambayo ilimtofautisha na wanafunzi wenzake shuleni hapo kitu ambacho kilipelekea hata kuwa kiongozi mwenye kujali watu anaowaongoza.
Mwalimu Irenge anaongeza kuwa Mwalimu Nyerere hakuwa na tabia ya kujisifu wala kujikweza ingawa alikuwa na uwezo mkubwa darasani mpaka kufikia kuvuka darasa la pili na kwenda darasa la tatu na pia ni mtu ambaye alikuwa anapenda kushirikiana na wenzake kwa kila jambo,pamoja na kuwa hivyo alikuwa anchukia watu kuwa wavivu na mtu asiyependa kumaptia mtu haki yake.
Bweni alilotumia Mwalimu lakini kwasasa ni darasa
Anasema manyanyaso ya wakoloni ndio anadhani yalipelekea Mwalimu Nyerere kupenda somo la siasa ili siku moja akomboe Taifa lake ambalo wazee wake walikuwa wakinyanyaswa na wakoloni
‘Kambarage alikuwa anachukia sana unyanyasaji nadhani hicho ndicho kilipelekea kupenda sana somo la siasa ili siku moja awakomboe watanzania,hatukujua kama atakuwa rais lakini dhamira yake ilikuwa ikionyesha kuwa ni mtu anayependa haki” alisema mwalimu Irenge
Pamoja na kuwepo watu mbalimbali ambao wanatoa historia,Mwalimu Irenge anasema kuwa kumekuwepo na upotofu wa historia ya mwalimu Nyerere kuwa katika maisha yake ya shule alikuwa akitembea kutoka Butiama mpaka Mwisenge kitu ambacho si kweli,anaongeza kuwa kuwa Kambarage alikuwa ni mtoto wa chifu na shule ya Mwisenge ilikuwa maalum kwa watoto wa machifu ambapo Kambarage alikuwa ni mmoja wa watoto wa Chifu.
Dawati alilotumia mwalimu Nyerere kusoma
Katika hilo Mwalimu Irenge anaongeza kuwa katika maisha yake yote ya shule Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere hakuwa mtu ambaye anapenda michezo kwani muda mwingi kwake ulikuwa ni kusoma vitabu vya siasa
Anasema ilikuwa ni vigumu nyakati hizo kumkuta Mwalimu katika masuala ya kimichezo na kama ulikuwa unamhitaji ilikuwa ni lazima umtafute sehemu ambayo alikuwa anapenda kusomea
'Kuna sehemu pale Shuleni alikuwa anapenda kusomea na kama ulikuwa unamhitaji lazima utamkuta pale” aliongeza mwalimu Irenge
Hali ya Mwalimu Irenge kwa sasa si nzuri kiafya na kiuchumi ambapo anasema kuwa wakati mwalimu akiwa hai alikuwa anamjali kwani kuna wakati alikuwa anakwenda Butiama na kukaa huko huku wakiongea kuhusu masuala ya nchi na Mwalimu wakati mwingine alikuwa anakwenda kwake kumjulia hali na ambapo kwa sasa imekuwa vigumu kwa viongozi kufika katika mjini .
Mwalimu Irenge anasema kitendo hicho kinamuumiza kwasasa kwani viongozi wa sasa wamekuwa tofauti na alivyokuwa mwalimu Nyerere kwani kiongozi anayefika kumsalimia mara moja moja nyumbani kwake ni mbunge wa jimbo la Musoma Vijijini Nimrod Mkono ambaye amekuwa mtu wa karibu tangu kufariki kwa Mwalimu Nyerere.
Maisha ya mzee huyo anasema kuwa alifurahi sana siku ambayo mwalimu alikuwa akikabidhiwa hati ya kuonyesha kuwa nchi yetu imekuwa huru kwani aliona amewashinda wakoloni kupitia kwa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kwa kuwa harakati zilianzia shule za Mwisenge alipokuwa akimfundisha somo la siasa.
‘Wakoloni walitunyanyasa sana nyakati za ukoloni lakini siku anapokea hati ya kuonyesha kuwa nchi yetu imekuwa huru nilifurahi sana maana niliona Kambarage Shujaa” anasema Mwalimu Irenge.
Mwalimu James Irenge kwa sasa ni mtu wa kushinda nyumbani na alistaafu kazi ya ualimu mwaka 1970 ambapo mpaka sasa watoto 12 na wajukuu 27,Mwalimu huyo anaishi katika maisha ya mateso baada ya serikali kushindwa kumlipa kiinua mgongo wakati alipostaafu anaongeza kuwa tangu amestaafu amekuwa akilipwa pensheni ya shilingi mia mbili mpaka mwaka 2005 ndipo ikapandishiwa na kufikia shilingi 20,000 na mwaka 2010 ndipo pensheni hiyo ikapanda mpaka kufikia kiasi cha shilingi 50,000.
Akiongea kwa tabu huku akisaidiwa na kijana wake Mwalimu Irenge anasema aliishaandika barua sehemu mbalimbali kuanzia kwenye ofisi ya Rais,haki za binadamu,wizara ya fedha na wizara ya kazi ambapo barua ya wizara hiyo ilikabidhiwa kwa waziri wa wizara hiyo Profesa Athuman Kapuya alipokuja Musoma kwenye sikukuu ya wafanyakazi mwaka 2009.
Pamoja na kunyimwa haki yake mwalimu huyo anasema kuwa kwa sasa serikali imewabagua sana wazee kwani hata yeye alialikwa mwaka jana tu kwenye sherehe ya wafanyakazi mjini hapa na kupewa zawadi la Blanketi lakini malalamiko yake wameshindwa kuyasikiliza mpaka sasam kitu kinazidi kumsononesha
Amesema mpaka leo hata mkuu wa Mkoa wa Mara hajawahi kwenda kumtazama wakati anaishi jirani kitu inachoonyesha kuwa viongozi wa siku hizi hawana upendo kwa wazee na hiyo ndiyo tofauti kubwa kati ya viongozi kama Mwalimu Nyerere na wa leo
Akiongelea kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere mwaka 1999,Mwalimu Irenge anasema kuwa Mwalimu hakupenda kufia nje ya nchi yake ingawa kuna watu ambao walimlazimisha kwa kuwa walikuwa na lengo lao katika nchi hii
Anasema kuwa wakati Mwalimu anaenda Uingereza alilia wakati akiongea naye kwani alisema kuwa hawezi kurudi mzima na anawaacha watu wake,anasema kuwa kwasasa nchi imepoteza uelekeo kwani baada ya kufa Mwalimu Nyerere nchi imekuwa ya kila mtu kufanya anavyotaka huku rushwa na ufisadi ukizidi kuwaumiza watanzania walio wengi.
Akiongelea wizi uliotokea hivi karibuni benki kuu na mikataba mibovu inayofanywa na serikali ni kipimo tosha kuwa serikali haiko makini katika masuala makubwa ya nchi na hivyo kuacha watanzania wakiishi katika umaskini mkubwa huku viongozi wachache wakiendelea kuwalaghai wananchi.
Anasema leo viongozi wetu wamekuwa kama wakoloni maana wakoloni ndio walikuwa wanatudanganya sana,kitu ambacho leo tena kimerudi kwa viongozi wetu.
“Hawa viongozi wetu leo wamekuwa kama wakoloni maana wamekuwa wakiwalaghai wananchi kwa vitu vidogo huku wao wakiendelea kuwa matajiri” aliongeza Mwalimu Irenge
Pamoja na Mwalimu huyo kuwa mwasisis wa TANU lakini anasema Chama Cha Mapinduzi kimepoteza mwelekeo kwani lengo lake lilikuwa ni kuwasaidia wakulima na wafanyakazi katika kuendeleza Taifa lao lakini kwa sasa chama hicho kimekuwa cha wafanyabiashara kitu ambacho Mwalimu hakupenda kwani aliona madhara yake
Mbali na Mwalimu Irenge kumfundisha Mwalimu Nyerere katika shule ya Mwisenge mjini hapa lakini mwalimu huyo anasema pia kuna viongozi ambao aliwafundisha katika shule hiyo.
Akiwataja kwa tabu kabla ya kupata ukweli wa majina hayo katika ofisi ya shule hiyo viongozi hao ni pamoja na Seleman Kitundu mwasisi wa Tanu na Oswald Marwa ambao wamewahi kuwa wakuu wa mikoa, huku Joseph Warioba alikuwa wazari mkuu wa Tanzania,Bhoke Munanka ambaye amewahi kuwa waziri ofisi ya Rais, Pius Ng’wandu,Richard Wambura ambaye amewahi kuwa balozi wakiwakilisha Tanzania,Mtaragara Chilangi ambaye amewahi kuwa katibu wa Elimu,Joseph Butiku ambaye amewahi kuwa Ka tibu wa Rais na mkuu wa Mkoa.
Baada ya kustaafu maisha ya Mwalimu Irenge kwasasa si mazuri kama anavyosema yeye ambapo kibaya zaidi anasema atajisikia vibaya kama ataondoka duniani pasipo kulipwa haki yake ambayo anaidai Serikali,mbali na hilo pia Mwalimu Irenge anasema kuwa uchaguzi wa Mwaka huu watanzania wapige kura kwa amani kwani hilo litakuwa jambo jema katika miaka kumi na moja ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Mwalimu Irenge alimalizia kwa kusema kuwa viongozi wabadilike na wawathamini wananchi kwani leo wananchi wanaishi kama vile si watanzania na pia hawathaminiwi na kuwafanya wachukie nchi yao.
“Mimi naomba viongozi wawajali watanzania ili wawe na upendo kwa nchi yao maana kama hawatawathamini watakuwa wanaichukia nchi yao” alimalizia Mwalimu Irenge
Mwisho
No comments:
Post a Comment