Thursday, September 16, 2010

VIFO VITOKANAVYO NA MALARIA VYAPUNGUA MARA

 
MUSOMA
 
MKUU wa Mkoa wa Mara kanali mstaafu Enos Mfuru leo amezindua mradi wa unyunyiziaji wa kiatirifu cha kuua mbu waenezao Malaria majumbani mkoa wa Mara.
 
Akizindua mradi huo mbele ya waandishi wa habari mjini hqapa,mkuu wa mkoa alisema kuwa ugonjwa wa Malaria hapa nchini unaleta kero kubwa kwani kila mwaka watu milioni 17 huugua malaria huku zaidi ya watu laki moja wakifariki kila mwaka kwa ugonjwa huo

                                                  Mkuu wa mkoa wa Mara Kanali mstaafu Enos Mfuru

Alisema katika mkoa wa Mara karibu watu laki saba huugua Malaria huku watu elfu tano hufariki kila mwaka  ambapo vipo hivyo Mfuru alisema ni sawa na asilimia thelathini na tano ya vifo vyote vinavyotokea mkoani hapa.
 
Mfuru alisema ili jamii iwe katika afya njema mikakati ya kisayansi inahitajika ili kuthibiti ugonjwa huo ambapo alisema kuwa ni pamoja na kutumia vyandarua vilivyowekwa viatilifu,kuzingatia usafi wa mazingira na kutoa  matibabu ya mapema na sahihi kwa wagonjwa wa Malaria.
 
Alisema mikakati yote hiyo imekuwa ikitekelezwa mkoa wa Mara ambapo imeweza kuopunguza wagonjwa wa Malaria kutoka laki saba kwa mwaka 2006 hadi laki moja kwa mwaka 2009 pia Mfuru alisema kuwa imeweza kupunguza vifo kutoka laki tano kwa mwaka 2006 hadi kufikia vifo 2808 kwa mwaka 2009.
 
Mkuu wa Mkoa huyo alisema kuwa kuzinduliwa kwa mradi huo mkoani hapa unalenga kuua mbu waenezao Malaria majumbani na kuweza kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Malaria na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo kwa kiasi kikubwa zaidi.
 
Akielezea kwa undani kuhusu mradi huo,Mfuru alisema kuwa uzoefu unaonyesha kuwa mradi huo umeleta mafanikio ya asilimia 98 kwa Zanzibar katika kupunguza maambukizi na vifo vinavyosababishwa na Malaria.
 
Katika mradi huo Mfuru aliwaeleza waandishi wa habari kuwa mradi wa kwanza utaanza kutekelezwa  mwezi Septemba  mwaka huu katika wilaya za Musoma Vijijini na Bunda huku awamu ya pili ikianza mwezi January mwaka kesho kwa wilaya za Tarime,Rorya na Serengeti.
 
Aidha mkuu wa Mkoa wa Mara kanali mstaafu Enos Mfuru alitumia nafasi hiyo  kutoa wito kwa wananchi hususani mkoa wa Mara kutoa ushrikiano ili mradi huo utekelezwe kama ulivyopangwa na kuweza kupunguza maambukizi na vifo vitokanavyo na Malaria.
 
Kwa upande wa Mganga mkuu wa Mkoa wa Mara Samson Winani alisema kuwa ugonjwa huo umekuwa kuero kwa wananchi kwa asilimia 35 ya vifo utokana na Maralia mkoani hapa.
 
Alisema kwa mikakati kama hiyo ana imani itasaidia kupunguza vifo na kuenea kwa ugonjwa huo kama ilivyo kwa Zanzibar ambapo leo vifo ni asilimia 0.6,alisema kuwa mpaka sasa tayari elimu imetolewa kwa viongozi wa vijiji ili nao kutoa elimu wa wananchi wa maeneo hayo katika kupambana na Malaria.
 
Winani aliongeza kuwa dawa hiyo wanayonyunyuzia haina madhara yoyote kwa binadamu hivyo wananchi wasiogope au kutorusuhu kufanyika kwa zoezi hilo
 
Naye mratibu wa Malaria mkoa wa Mara Edwin Nyahindi alisema kuwa kumekuwepo na baadhi ya watumishi wa idara ya afya kutokuwa waaminifu kwa kuiba dawa katika hospital ya mkoa na kwenda kuziuza kwenye maduka ya madawa.
 
Alisema kuwa zoezi hilo litafanyika bila malipo yoyote kwani tayari serikali imegharamia ila ni mhusika atatakiwa kuandaa ndoo moja ya maji
 
Mradi huo unatekelezwa na wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupita shirika la Research Triangle Institute International ( RTI) ,kwa kipindi cha miaka mitano mradi huo utafadhiliwa na serikali ya Marekani kupitia mfuko wa Rais na baada ya kipindi hicho gharama za utekelzaji zitatokana na Bajeti za Halmashauri.
 
……………………………………………………………

No comments:

Post a Comment