Tuesday, September 28, 2010

MUSOMA
Siku chache baada ya mgombea Urais kupitia chama cha Mapinduzi (CCM) Jakaya Mrisho Kikwete awapandishe jukwaani wagombea 13 wa nafasi za udiwani jimbo la Musoma mjini na  kuwaombea kura taarifa zinasema kuwa  madiwani  sita kati ya hao wamekigeuka chama hicho kwa kujiombea kura wao pamoja na rais.
Taarifa zinasema kuwa kufika kwa Kikwete mjini hapa umebaini kuwa madiwani hao wamekuwa wakifanya kampeni za nyumba kwa nyumba na kuomba kura zao na za rais bila ya kumuombea mgombea ubunge wa jimbo hilo Vedastus Manyinyi Mathayo.
Kikwete akihutubia maelfu ya wananchi wa jimbo la Musoma mjini aliwaomba wananchi kuwachagua madiwani hao ili kudumisha amani na kuharakisha maendeleo kwa maelezo kuwa CCM ni chama kinachoaminika kwa utekelezaji wa ahadi zake kwa wananchi.
Aidha imedaiwa kuwa wagombea hao wa udiwani wamelazimika kuacha kumnadi mgombea ubunge wa chama chao baada ya kuonywa na wananchi kuwa kuendelea kuomba kura za ubunge kunaweza kuwaponza na kukosa nafasi hizo.
Wakizungumzia sakata hilo madiwani watatu kati ya sita wanaodaiwa kufanya kampeni ya kujiombea kura bila kuomba za mbunge walisema kuwa wamekuwa wakipewa vitisho na wananchi baada ya kutamka jina la Mathayo katika mikutano ya ndani na ya nje.
Kufuatia taarifa hizo Jambo Leo lilimtafuta mwenyekiti wa CCM Musoma mjini Joseph Obetto ambapo simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita mara sita mfululizo bila mafanikio ili aweze kuelezea juu ya tuhuma hizo.
Haula Kachwamba mbaye ni katibu wa CCM wilaya ya Musoma alipotafutwa kuelezea hali hiyo kwa njia simu pia hakuweza kupatikana kwani simu yake ilikuwa inaita bila kupokelewa.
Katika Jimbo la Musoma mjini kwa sasa limekuwa katika ushindani mkali kuliko majimbo yote ya mkoa wa Mara kati ya vyama vya Chadema,CCM na CUF ambapo vyama vingine vinavyoshiriki uchaguzi huo kwa ubunge ni DP na NCCR Mageuzi.
Mgombea wa Chadema anayeonekana kuleta upinzani mkubwa ni mtoto wa mdogo wake Baba wa taifa mwalimu Julius Nyerere Vicent Nyerere wakati mgombea wa CUF ni Mstapher Juma Wandwi ambaye sasa anagombea jimbo hilo kwa mara ya tatu mfululizo.
Katika barabara za manispaa ya Musoma waendesha pikipiki (Bodaboda) wamekuwa wakiendesha pikipiki zao wakiwa na bendera ya chama cha Demokrasia na maendelo CHADEMA huku wakionyesha ishara ya vidole viwili ishara ambayo inatumiwa na chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA

No comments:

Post a Comment