ORODHA YA WANAFUNZI WALIOSOMA SHULE YA MSINGI MWISENGE
MWALIMU MKUU WA SHULE YA MSINGI MWISENGE MWALIMU TAIRO
JENGO ALILOKUWA AKIISHI MWALIMU WA MWALIMU NYERERE
JENGO LILILOKARABATIWA
OFISI YA WALIMU
OKTOBA 14, mwaka huu, taifa la Tanzania linaadhimisha Miaka
14 ya Kumbukumbu ya Kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere aliyeaga
dunia 0ktoba 14, 1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas, jijini London,
nchini Uingeleza alikokuwa amekwenda kupata matibabu.
Mazuri mengi yatazungumzwa kuhusiana na Mwalimu Nyerere lakini
mimi nitajikita pale shule ya msingi Mwesenge
iliyopo Manispaa ya Musoma,shule ambayo Baba wa Taifa hili alitembea
umbali wa kilometa 37 kutoka Kijijini Mwitongo Butiama kwenda kupata elimu ya
msingi kwenye shule hii.
Hii ni shule yenye historia kwani licha ya Mwalimu Nyerere kusoma
kwenye shule hii wapo viongozi wengine waliopata kushika nafasi kubwa na
wengine bado wana nafasi kubwa akiwemo Waziri Mkuu wa zamani na Mwenyekiti wa
wa Tume ya mchkato wa kupata Katiba mpya Jaji Joseph Sinde Warioba.
Orodha ni ndefu ya viongozi waliokuwa wanafunzi wa shule hii ambayo
inaelezwa licha ya Serikali kujitahidi kuweka mazingira mazuri ya shule
kutokana na historia yake bado inakumbwa na matatizo lukuki ikiwemo kukosa matundu
ya vyoo na kupelekea wanafunzi wa shule hiyo kukosa mahala pa kujisaidia!.
Licha ya viongozi hao nilioanza nao waliosoma kwenye shule
hii,wengine waliosoma Hapa ni Bhoke Munanka huyu alipata kuwa Waziri katika
Ofisi ya Rais wa awamu ya kwanza na kufanya kazi kwa karibu na Mwalimu.
Pia kuna majina ya Joseph Butiku aliyekuwa Katibu wa Rais
Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ambaye kwa sasa yupo karibu na makumbusho
ya Mwalimu,Richard Wambura aliyepata kuwa Balozi wa Tanzania katika Nchi
mbalimbali naye amesoma Mwisenge.
Majina kama Mutaragara Chirangi aliyekuwa Katibu wa
elimu,Selemani Kitundu na Oswrd Marwa waliopata kushika nafasi ya Mkuu wa mkoa
wa Mara kwa vipindi tofauti wote wamesoma kwenye shule hii.
Kwa safu hiyo ya viongozi waliosoma Mwisenge shule ya msingi kuna
kila sababu ya kusema ni shule ya kihistoria kwa Taifa hili inayopaswa kuenziwa
kwa kuangalia changamoto zinazoikabili hili historia yake iendane na mazingira
yake.
“Baadhi ya majengo hali yake ni nzuri kutokana na Serikali
kuamua kuyakarabati ili kumuenzi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lakini
mengine bado hayajakarabatiwa ni chakavu na nyumba wanazoishi walimu ni mbovu
na haziendani na hadhi ya jina la shule hii.
“Ile nyumba unayoiona ndio aliyokuwa anaishi Mwalimu
aliyekuwa anamfundisha muasisi wa Taifa hili pamoja na viongozi wengine
waliopata kusoma kwenye shule hii ni budi viongozi waliopata kupitia hapa na
wadau wengine waienzi shule hii,”anaeleza mwalimu mkuu wa shule ya msingi
Mwisenge Redigunda Tairo.
Ukilitazama jengo ambalo aliishi Mwalimu aliyemfundisha
Mwalimu Nyerere na viongozi wengine wakubwa katika Taifa hili utaungana nami katika
makala hii kuona kuna umuhimu wa kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa dhati na sio
unafiki!.
Serikali haishindwi kujenga zile nyumba za walimu na kumalizi
majengo chakavu ya shule ya msingi Mwisenge ambayo historia yake inatakiwa kuwa
shule ya mfano maana hata wageni wanaofika Musoma uwa wanatamani kuona shule
aliyosoma Baba wa Taifa lakini kwa hizi nyumba za walimu tunatia aibu.
Tukiachana na hilo la uchakavu wa baadhi ya majengo na
nyumba za walimu,kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo ambaye hakusita
kuzungumzia changamoto za shule hiyo alielezea kuwepo na uhaba wa matundu ya
vyoo na kusababisha usumbufu wa sehemu ya kujisaidia kwa wanafunzi wa shule
hiyo!.
Matundu sita ya vyoo katika shule hii ndiyo
yanayotumiwa na wanafunzi 808 wanaosoma kwenye shule hii na kuwafanya wanafunzi
baadhi kwenda kwenye shule jirani kwa ajili ya kujisaidia hii si sawa ikiwa leo
tunafanya kumbukumbu ya Baba wa Taifa aliyesoma kwenye shule hii.
Maji kwenye shule ya Mwisenge yamekatwa kwa zaidi ya
miaka miwili kutokana na deni la miaka mingi ya nyuma na kuwafanya wanafunzi wa
shule hii kutoka na maji nyumbani ama kufuata ziwani kwa ajili ya
matumizi,lazima tuliangalie hili kama kweli tunamuenzi Mwalimu.
Leo tukifanya kumbukumbu ya miaka 14 ya kifo cha Hayati
Baba wa Taifa hili,wanafunzi wa shule ya msingi Mwisenge bado wanakaa chini
kutokana na upungufu wa madawati ili hali viongozi wengi licha Mwalimu wamesoma
kwenye shule hii.
Hivi ni kweli tunapofanya kumbukumbu hii tunashindwa
kuitembelea shule hii nakujua changamoto zake ili tusiwe na mambo mengi ya
kuandika tukiwa tunamkumbuka muasisi wa taifa hili?.
Majibu ya swali hili ni rahisi tunajionyesha tupo
karibu katika kumkumbuka Mwalimu kumbe ni unafiki huku tukiona wanafunzi
wanaosoma kwenye shule aliyoma wakikosa sehemu ya kujisaidia,maji na wengine
wakikaa chini.
Changamoto
za shule zinapaswa kufanyiwa kazi mara baada ya siku hii kupita ili
siku tutakapofanya kumbukumbu ya miaka 15 baada ya kifo cha Baba wa
Taifa tusiwe wa kuandika haya ya wanafunzi wa shule aliyosoma kukosa
mahala pa kujisaidia.
Najua
inawezekana kama tutaamua na tukiacha unafiki wa kufanya kumbukumbu
huku sehemu ya kumbukumbu zake zikiwa hazingaliwi na isitoshe tukaja
kupata hesabu ya fedha nyingi ambazo zitatumika kutokana na siku hii.
No comments:
Post a Comment