Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya tukio la leo,
Jumapili, Mei 5, 2013 la mlipuko kwenye Kanisa Katoliki la Mt. Joseph
Mfanyakazi la Olasiti Jijini Arusha. Tukio hilo la kigaidi
limesababisha mtu mmoja kupoteza maisha na wengine 40 kujeruhiwa. Rais
Kikwete analaani vikali shambulio hilo lililofanywa na mtu au watu
katili, waovu na wenye dhamira mbaya na nia mbaya kwa Tanzania na watu
wake.
Rais Kikwete ameagiza
vyombo vya usalama nchini kumsaka mtu au watu waliohusika na kitendo
hicho kiovu na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria. Vile vile Rais
Kikwete amewataka wananchi wote kuwa watulivu wakati Serikali na vyombo
vyake inaendelea kufuatilia tukio hili. Tutawasaka popote walipo na
kupambana nao bila huruma. Aidha, tutakabiliana na aina yoyote ya
uhalifu nchini iwe ni ugaidi au aina yoyote ya uhalifu wa namna hiyo au
wa namna nyingine, uwe na chimbuko lake ndani ya nchi ama nje ya nchi
yetu. Kamwe hatutakubali kuwaacha wavuruge amani na usalama wa Tanzania
na watu wake. Rais anaamini kuwa Serikali, kwa msaada na ushirikiano wa
wananchi, watu hao watapatikana na kuadabishwa ipasavyo.
Aidha, Rais
Kikwete anatoa rambirambi za dhati ya moyo wake kwa wafiwa na wale wote
ambao wamejeruhiwa katika tukio hilo. Anaungana nao katika machungu na
msiba. Rais pia anawaombea wote walioumia katika tukio hili wapate nafuu
ya haraka na waendelee na shughuli zao za ujenzi wa taifa.
Rais Kikwete vilevile
anatoa pole nyingi kwa viongozi na waumini wa Kanisa Katoliki kwa tukio
hili la kusikitisha na kuvurugika kwa ibada na shughuli yao muhimu ya
uzinduzi wa Kanisa lao.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU,
DAR ES SALAAM
5 Mei, 2013
No comments:
Post a Comment