HAWA
ni baadhi ya Waandishi wa habari wanaochukua mafunzo ya Habari za
uchunguzi za Biashara na Uchumi katika chuo kikuu cha Mtakatifu
Augustine (SAUT) Jijini Mwanza (Picha na David Azaria)
Na David Azaria, SAUT-Mwanza yetu
WAANDISHI
wa habari nchini wameshauriwa kujikita katika uandishi wa habari za
Biashara na Uchumi ili kuibua fursa za kibiashara hususani mipakani ili
kuwafanya Watanzania kuelewa mazingira ya kibiashara vizuri na
kuyatumia.
Ushauri
huo umetolewa na Makamu Mkuu wa chuo kikuu cha Mtakatifu Augustin
kilichoko jijini Mwanza Padri Charles Kitima hivi karibuni wakati
akifungua mafunzo ya uandishi wa habari za uchunguzi juu ya biashara na
uchumi yatakayodumu kwa mwaka mmoja kwa awamu nne tofauti yanayofanyika
katika chuo kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT).
Mafunzo
hayo yanawashirikisha jumla ya waandishi wa habari 30 kutoka katika
vyombo mbalimbali vya habari nchini, ambao walipatikana kufuatia mchujo
kutoka miongoni mwa waandishi wa habari zaidi ya 60 waliotuma maombi yao
kuomba kujifunza mafunzo hayo.
Padri
Kitima alisema kuwa sio kila mtu anaweza kuelezea habari inayoifaa
jamii bali waandishi pekee ndio kiungo muhimu hapa nchini na duniani
kote ambao wanaweza kutoa maelezo mazuri kwa kuonyesha changamoto na
mafaniko mwishowe fursa zilizopo ziweze kitumika ipasavyo.
“Waandishi
mkichambua vizuri kuhusu hali ya uchumi wa Tanzania kuanzia ngazi za
vijijini mpaka taifa wananchi watajifunza na kuzitambua fursa zilizopo
na kuzitumia kisha wataepukana na dhana ya Rais wa nchi atuletee pesa na
wakati wana uwezo wa kutumia fura hizo kujikomboa na lindi la umaskini
na kukuza uchumi wao wenyewe”alisema Padri Kitima na kuongeza.
“Vyuo
vikuu vyote vinavyojihusisha na kufundisha masomo ya uandishi wa habari
havikuwahi kufundisha somo la uandishi wa habari za biashara na uchumi,
kwa hiyo ni changamoto ambayo inatukabili, ni muhimu kwenu kutumia
mafunzo haya kuhakikisha mnaibua mianya na fursa za kiuchumi kwa
kuandika habari za uchunguzi zinazohusu uchumi ili vikwazo
viondolewe…..’’.
Alisema
kwa upande wake anaamini wananchi wakizifahamu fursa zilizopo na
wakazitumia ipasavyo kutakuwa na mabadiliko makubwa katika maisha yao,
tofauti na ilivyo sasa ambapo kila mmoja anamlilia rais kwamba ndiye
chanzo cha mambo yote hususani suala zima la mfumuko wa bei hali
iliyosababisha kupanda kwa gharama za maisha.
“Kwa
mfano angalia nchi za wenzetu wao wanafanya biashara masaa 24 lakini
Tanzania tunafunga benki saa kumi alasiri wakati muda huo Marekani ni
saa nne za asubuhi tunadai kuwa hayo mambo ya kufanya biashara usiku na
mchana ili kukuza uchumi ni ya nchi zilizoendelea….’’ Alisema Kitima.
Alibainisha
kuwa endapo nchi inahitaji kubadilika na kuingia katika rekodi za
miongoni mwa nchi zenye uchumi mzuri na unaoheshimika ni lazima
waandishi wa habari wajitume na kuandika habari zinazohusu uchumi na
kuwafumbua macho Watanzania katika suala zima la kutumia fursa zilizopo
hususani sekta ya utalii ambapo aliishauri Serikali kuwa asilimia 90 ya
uwekezaji katika sekta ya utalii ni vyema ikamilikiwa na wazawa ndipo
uchumi utaweza kupanda na kukua kwa kasi.
No comments:
Post a Comment