Thursday, July 12, 2012



    DC BUNDA  ATOA AGIZO KWA POLISI NA WATENDAJI  

SERIKALI wilayani Bunda mkoani Mara imetoa siku tatu kwa maafisa watendaji wa vijiji,kata na vituo vyote vya polisi wilayani humo,kuwakamata watu  ambao wameanza kulangua zao la pamba kwa wakulima kinyume na taratibu.

Agizo hilo limetolewa na mkuu wa wilaya ya Bunda Bw Joshua Mirumbe,kwa nyakati tofauti wakati akiongea na wananchi wa vijiji vya tarafa ya Chamriho katika ziara ya kujitambulisha baada ya kuteuliwe kushika wadhifa huo Rais Jakaya Kikwete.


Awali wananchi wa vijiji hivyo wamemueleza mkuu huyo wa wilaya kuwa kutokana na kuchelewa kufunguliwa kwa msimu wa pamba na ugumu wa maisha wananchi wameanza kuuza pamba yao kwa walanguzi ambao wamekuwa wakilangua kwa shilingi 500 kwa kilo moja.

Wamesema wameamua kufikia uamuzi huo kutokana na bodi ya pamba kuchelewa kutangaza bei halisi ya zao hilo na tarehe maalum ya kuanza kwa msimu wa pamba ambayo ni zao tegemezi kwao.

Kufuatia  malalamiko hayo mkuu wa wilaya, amesema kuwa msimu wa pamba tayari umeshatangazwa na bei elekezi ambayo makampuni yanatakiwa kununu kwa shilingi 650 kwa kilo na kwamba wakulima hawapaswi kuuza chini  ya hapo kwa walanguzi hao.

Amesema kuwa kitendo cha walanguzi kupita vijijini na kuwahadaa wakulima na kuwapa bei ndogo ni kosa la jinai na hivyo akawaagiza viongozi hao kuwakamata mara moja na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola wale wote watakaobainika kufanya hivyo kuanzia sasa.

Hata hivyo amewaomba wananchi hao kuhakikisha hawaweki pamba yao maji na magadi kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanaharibu ubora wa pamba na kufanya ikose ubora katika soko la dunia.

No comments:

Post a Comment