Saturday, June 16, 2012

                            SIKU YA MTOTO WA AFRIKA


SERIKALI wilayani Butiama mkoani Mara,imelaani vikali vitendo vya ukiukwaji wa haki za watoto ikiwa ni pamoja na unyanyasaji ambao umekuwa ukifanywa na baadhi ya walezi na wazazi katika wilaya hiyo na mkoa wa Mara kwa ujumla.

Mkuu wa wilaya ya Butiama Bi Angelina Mabula,ameyasema hayo katika kijiji cha Kwibara kata ya Mugango wilayani humo katika maazimisho ya mtoto wa Afrika ambayo yamefanyika kiwilaya kijijini hapo.

Amesema wazazi na walezi wanawajibu wa kuwapa watoto haki zao za kimsingi ikiwa ni utekelezaji wa sera ya mtoto ya Tanzania ya mwaka 2008 na sheria ya mtoto ya mwaka 2009,kuwalinda watoto na mambo yote maovu ikiwemo kuwasikiliza,kuwajali na kuwaendeleza kiroho na kimwili.

Awali katika risala iliyosomwa na watoto wa Halmashauri hiyo wamesema kuwa wanahitaji kulindwa  dhidi ya mambo maovu ikiwemo ukatili,utekelezwaji,ubakaji,unajisi,ukeketwaji,ubaguzi wa kijinsia na kufanyishwa kazi za malipo.

Wamesema kumekuwepo na vitendo vya ubaguzi kwa watoto ambao ni walemavu  wakitolea mfano sense ya mwaka 2008 katika wilaya hiyo watoto 1056 hawakupelekwa shule kwa sababu ya ulemavu wao.

Maadhimisho ya mtoto wa Afrika hufanyika kila june 16 ambapo nchi mbalimbali barani Afrika hukumbuka mauaji ya kikatili ya watoto wa kitongoji cha Soweto nchini Afrika Kusini, waliokuwa wakidai haki za usawa katika elimu,kufundishwa kwa kutumia lugha yao kutoka mikononi mwa makaburu.

No comments:

Post a Comment