WATENDAJI WATAKIWA KUSIMAMIA MAPATO NA MATUMIZI
Dinna Maningo,Rorya.
WATENDAJI
wa vijiji na Kata katika kata ya Kisumwa Wilayani Rorya Mkoani
Mara wametakiwa kusimamia vyema Mapato na Matumizi yatokanayo na vyanzo
vya ndani katika kukuza Uchumi wa Wilaya ili kupata maendeleo endelevu.
Hayo
yalibainishwa jana na Mkaguzi wa ndani wa Wilaya hiyo, Peter
Chuwa,katika kikao na viongozi hao kilichofanyika katika Shule ya
Sekondari ya Kisumwa iliyoko kata ya Kisumwa Tarafa ya Subha Wilayani
hapa.
Alisema kila kiongozi anapaswa kutambua wajibu na dhana ya uwajibikaji katika Usimamizi wa ukusanyaji wa mapato.
Aidha
kwa upande wa usimamizi wa matumizi ya miradi ya ujenzi alisema sio
mzuri kutokana na watu kutokuwa na dhana ya uwajibikaji na kutoweka kwa
uadilifu hali inayosababisha Wilaya hiyo kuwa nyuma kimaendeleo.
Akijibu
hoja ya watendaji hao ya kutokuwa na elimu ya ujazaji wa vitabu vya
fedha pamoja na utunzaji wa kumbukumbu za kihasibu, alisema kuwa hiyo
ni changamoto kubwa inayokabili idara hiyo na kwamba inapaswa kuwepo kwa
mafunzo kwa wasimamizi wakuu wa rasilimali fedha.
Aliongeza
pia kuwa kutokana na kasumba ya maduka kutokuwa na risiti za fedha,
watendaji hao wamekuwa wakitumia fedha hizo bila kuwepo kwa kumbukumbu
yoyote hali ambayo inaweza kuleta utata wa matumizi ya fedha za Serikali
na kusababisha kiongozi kupata tuhuma ya ubadhilifu wa fedha nahivyo
kuwataka kutunza kumbukumbu hata kama ni kumbukumbu za kuandikishana na
kuweka sahihi bila risiti.
Kwa
upande wa Watendaji nao walilamikia kuwepo kwa ucheleweshaji wa asilimia
20 ya mapato yanayoingia kila mwezi katika mfuko wa kila kijiji hali
inayowanakatisha tamaa kwa kuendelea kuwatumikia wananchi huku wakiwa na
mazingira magumu ya kazi hali ambayo inachochea kuwepo kwa mianya ya rushwa.
Naye
Mjumbe wa Dawati la kuzuia ukatili wa kijinsia, Neema Antony aliwataka
watendaji hao kufikisha ujumbe kwa wananchi kuwepo kwa Dawati hilo
maalumu kwa kusaidia baadhi ya familia zinazokuwa na unyanyasaji ili kutatua
matatizo yao yanayokuwa yakiwakabili hasa wanawake ambao wamekuwa
wakipata vipigo kutoka kwa waume wao, pia wanaume ambao nao wanapata
vipigo kutoka kwa wake zao.
Alisema Dawati si sehemu iliyotegwa katika Jeshi
la Polisi pekee bali pia wananchi wanaweza kuanzisha ili kutatua kesi
za unyanyasaji wa kijinsia, na watoto pamoja na kurithi wajane.
,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,MWISHO,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,
No comments:
Post a Comment