Sunday, May 6, 2012

MWANASHERIA MKUU AFAFANUA UTEUZI WA WABUNGE NA MAWAZIRI WAPYA


Mheshimiwa Rais
Jakaya Mrisho Kikwete, tarehe 4 Mei, 2012 alitangaza mabadiliko katika safu ya
Baraza la Mawaziri.  Katika uteuzi wa
Mawaziri na Manaibu Waziri, Mheshimiwa Rais aliwateua Mawaziri wapya kutoka
miongoni mwa Wabunge aliokuwa amewateua na kuwatangaza.  Baada ya uteuzi huo, kumetolewa maoni kwamba
hatua ya Mheshimiwa Rais kuwateua Wabunge Wapya ambao hawajaapishwa Bungeni kuwa
Mawaziri ni kitendo cha uvunjaji wa Katiba



Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali inayachukulia maoni haya kama ni jambo lenye
maslahi ya jamii na linalohitaji kufafanuliwa; kwa upande mmoja lakini pia,
kutolewa kwa elimu ya Umma; kuhusu Mamlaka ya Rais ya uteuzi wa Wabunge. 

Msingi wa
Katiba tunaoanza nao ni maelekezo ya masharti yaliyomo kwenye Ibara ya 55(4)
kwamba:

“Mawaziri na Naibu
Mawaziri wote watateuliwa kutoka     miongoni
mwa Wabunge”
Pili, ni
mamlaka ya Rais ya uteuzi wa Wabunge aliyopewa na masharti ya Ibara ya 66(1)(e)
yenye aina ya Wabunge wasiozidi kumi watakaoteuliwa na Rais kutoka miongoni mwa
watu wenye sifa zilizotajwa katika aya za (a) na (c) za ibara ya 67 na angalau
Wabunge watano kati yao wakiwa Wanawake.
Wabunge aliowateuwa Mheshimiwa Rais wanatokana na Ibara hii.

Tatu, baada
ya hatua zote hizi ikumbukwe kwamba aliyeteuliwa au kuchaguliwa kuwa Mbunge
anakuwa Mbunge ama baada ya kutangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi; au baada ya
kuteuliwa na Tume ya Uchaguzi kwa wale Wabunge wa viti maalum au anapochaguliwa
na Baraza la Wawakilishi au anapoteuliwa na Rais akitumia Mamlaka yake ya
uteuzi yanayotokana na Ibara ya 66(1)(e). Hivyo Wabunge wanaohusika hawahitaji
kuapishwa kwanza Bungeni ili wawe Wabunge.
Kiapo cha Mbunge Bungeni kinamwezesha tu kushiriki katika shughuli za
Bunge. 

Katiba ya
nchi haiweki kwa Rais masharti kwamba kabla ya kumteua Mbunge wa aina hiyo kuwa
Waziri au Naibu Waziri Mbunge huyo awe ameapishwa Bungeni kwanza.  Masharti mawili muhimu na ya kuzingatia ni
kwamba mteule wa nafasi ya uwaziri au Naibu Waziri hatashika madaraka yake ila
mpaka kwa mujibu wa Ibara ya 56 ya Katiba, awe ameapa kwanza mbele ya Rais
kiapo cha uaminifu na pia kiapo kingine chochote kinachohusika na utendaji wa
kazi yake kitakachowekwa kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge.  Sharti la pili, litahusu kiapo cha Uaminifu
katika Bunge kabla Mbunge hajaanza kushiriki katika shughuli za Bunge kwa
masharti ya Ibara ya 68 ya Katiba.  Viapo
hivyo havitegemeani na vinaweza kufanyika kwa nyakati tofauti.

Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali inasisitiza kwamba Wabunge ambao hawajaapishwa
ndani ya Bunge ni Wabunge na wanapoteuliwa kushika nafasi ya Uwaziri au Naibu
Waziri ni halali kwa kuwa uteuzi huo haukiuki masharti yoyote ya Kikatiba au
Sheria.  Aidha, katika kutekeleza
madaraka ya kazi ya Uwaziri au Naibu Waziri Mbunge atahitaji kiapo mbele ya
Rais hata kama hajaapishwa Bungeni.
Busara ya uandishi wa Katiba na Sheria imetambua kwamba kunaweza kukatokea
uteuzi wa aina hiyo wakati Bunge limeahirishwa kama ilivyo sasa.  Masharti ya Ibara ya 68 ya Katiba yatazingatiwa
katika kikao cha Bunge kijacho.

Bila shaka
ufafanuzi huu utaleta uelewa katika jambo hili na kuepusha mikangayiko
isiyokuwa ya lazima.

Imetolewa na Jaji
Frederick M. Werema (Mb)
MWANASHERIA
MKUU WA SERIKALI
06 Mei, 2012

No comments:

Post a Comment