Sunday, April 22, 2012





HABARI KUTOKA KAHAMA

Viongozi wa wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga,wameiomba bodi ya usajili wa makandarasi nchini CRB,kuifuta kampuni ya ujenzi ya JASCO ya jijini Mwanza,kwa madai ya kujenga chini ya kiwango barabara  za lami katika mji mdogo wa Kahama.

Barabara hizo ambazo tayari zimeigharimu serikali zaidi ya shgilingi bilioni moja,zinajengwa ikiwa ni utekelezaji wa  ahadi ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete ambayo aliitoa wakati wa kampeni za mwaka 2010 kwaajili ya kuupatia mji huo barabara za lami ambao umekuwa ukikua kwa kasi kubwa.

Wakizungumzia ujenzi wa barabara hizo ambazo zimeamriwa kubomolewa baadhi ya maeneo na kutakiwa kujengwa upya kutokana na kujengwa chini ya kiwango,mbunge wa jimbo la Kahama Mh James Lembeli,amesema endapo serikali itazidi kutoa zabuni kwa mkandarasi huyo yuko tayari kupiga kampeni ya kukwamisha bajeti ya wizara ya ujenzi  inayotarajia kuwasilishwa bungeni mwezi julai mwaka huu.

Diwani wa kata ya Kahama mjini Bw Abbasi Omari Jafari,amesema ujenzi huo ambao uko chini ya Tanroads mkoa wa Shinyanga haukushirikisha kabisa halmashauri hiyo lakini licha ya madiwa kuhoji kila wakati baada ya barabara hiyo kuanza kubomoka kipindi kifupi baada ya ujenzi wake kukamilika.

Nao baadhi ya wananchi wa mji wa Kahama,wameitaka  serikali kupitia Tanroads,kuwa makini wakati wa kutoa kazi za ujenzi wa miundo mbinu hasa ya barabara,badala ya kutoa kazi hizo  kwa wakandarasi wasio na uwezo na sifa jambo ambalo limekuwa likichangia barabara hizo kuharibika kwa kipindi kifupi tu baada ya ujenzi wake kukamilika huku zikiwa zimegharimu mamilioni ya fedha za walipa kodi

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kahama Meja Mstaafu Bahati Matala,amesema tayari serikali imemuamuru mkandarasi huyo kuibomoa barabara hiyo na kutakiwa kuijenga upya kwa gharama zake huku akionya kuwa serikali kamwe haita wavumilia wakandarasi wa aina hiyo.

Miezi kadhaa iliyopita mkandarasi huyo kampuni ya Jasco,ililalamikiwa na wananchi wa kijiji cha Wegero katika halmashauri ya Musoma vijijini wakiongozwa na mbunge wao Mh Nimrod Mkono kwa madai ya kujenga bwawa la maji lenye thamani ya zaidi ya bilioni tatu ambalo lilibomoka ndani ya mwezi mmoja tu baada ya ujenzi wake kukamilika.

No comments:

Post a Comment