Shirika la kiraia la Mara Hope for Life(MHL) linaloundwa na wanahabari mkoani Mara limelitaka jeshi la polisi mkoani Mwanza kuhakikisha kwamba linawasaka kwa udu na uvumba na kuwatia mbaroni watu waliohusika katika mauaji ya Mwandishi wa habari mkoani humo marehemu Richard Masatu aliyefariki dunia leo siku ya jumatano.
Kauli hiyo imetolewa na mkurugenzi wa habari na mawasiliano wa shirika hilo bw. Gaya Masatu katika taarifa ya salamu za pole alizomtumia mwenyekiti wa chama cha wandishi wa habari mkoani Mwanza (MPC) kufuatia kifo cha mwandishi huyo aliyefariki muda mfupi baada ya kufikishwa katika hospitali ya serikali ya Seketure jiji humo.
Katika salamu hizo bw. Gaya Masatu amesema jeshi la polisi halina budi kuchukua hatua za kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria ili haki itendeke, watu waliohusika katika mauaji hayo ya kinyama ambayo yamekatisha uhai wa mwanahabari huyo aliyeitumia kalamu yake kuielimisha jamii .
Kwa mujibu wa taarifa ya salamu hizo za pole,shirika la Mara Hope for Life limesema limepokea kwa majonzi na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha marehemu Richard Masatu aliyejiunga na tasnia ya habari mwanzoni mwa miaka ya tisini akiandikia vyombo mbalimbali vya habari kama vile magazeti ya Heko, Shaba na Msanii Afrika.
Mkurugenzi huyo wa Habari na Mawasiliano amemuelezea marehemu kwamba wakati wa uhai wake alikuwa mchapakazi na mpenda umoja miongoni mwa wanahabari wenzake huku akikumbukwa pia katika harakati zake za kujihusisha na mambo ya kisiasa hususani ndani ya chama tawala cha Mapinduzi(CCM) katika ngazi ya mkoa na Taifa.
Bw. Gaya Masatu amesema kutokana na wasifu huo, marehemu Richard Masatu ataendelea kukumbukwa daima na wapenda maendeleo huku akiwataka wanahabari wote nchini,familia,ndugu na jamaa kuwa wavumilivu na wastahimilivu na kujipa matumaini katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.
No comments:
Post a Comment