Musoma
BARAZA la Madiwani katika Halmashauri ya Musoma vijijini mkoani Mara,limeikataa taarifa ya mwaka ya utekelezaji ya miradi mbalimbali ya maendeleo kwa halmashauri hiyo baada ya kubaini miradi mingi ni hewa na mingine imetekelezwa chini ya kiwango.
Madiwani wa baraza hilo la halmshauri ya Musoma vijijini,wakiongozwa na mwenyekiti wao Magina Magesa,walifikia hatua hiyo juzi mchana muda mfupi baada ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Dk Karaine ole Kunei kutoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo ambayo na ilisomwa kwa niaba yake na afisa mipango wa halmashauri Bw Yared Mgula katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo mjini hapa.
Baadhi ya miradi hiyo iliyotajwa kutekelezwa chini ya kiwango ama kutokuwepo kabisa vijijini licha ya fedha zake kunyeshwa katika taarifa hiyo kutolewa na kudaiwa kutekelezwa ni Malambo kwajili ya matumizi ya binadam na mifugo,majosho ya mifugo,barabara,ujenzi wa zahanati na nyumba za walimu na wataalama wa sekta za afya vijijini yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 800.
Baadhi ya Madiwani hao Nathon Thomas wa kata ya Kianyari Gunje Christopher wa kata ya Murangi na Malinde Changwe wa kata ya Kiriba,wamedai wakuu wa idara wakiongozwa na mkurugenzi wao,wamekuwa wakitekeza miradi hiyo kupitia katika katibu lakini mingi haipo kabisa vijijini na mingine kutekelezwa chini ya kiwango.
“Mimi nasema sikubaliani kabisa na taarifa hii ya mwaka ya utekelezaji kwani miradi inayotajwa hapa mingi haipo ama imetekelezwa ndani ya vitabu kwa mfano lambo la Lyasembe limejengwa lakini halijawahi kuingiza maji kutokana na kujengwa chini ya kiwango sasa nalo katika taarifa hii lina tajwa”alisema Christopher diwani wa Murangi.
Kutokana na hoja hizo,wajumbe hao wa baraza la madiwani wakikata kwa kauli moja kupokea taarifa hiyo na kutaka kurejeshwa katika kamati husika ya kila mradi ili kupitiwa upya kwaajili ya kupatiwa majibu ya uhakika kabla ya kuchukua hatua dhidi ya watendaji.
“Mimi nashauri baraza lijigeuze kama kamati tumjadili mkurugenzi hatiwezi kuletewa vitu vya kupikwa katika baraza hili kila leo inaonekana tunachezewa kana kwamba sisi si wawakilishi wa wansanchi”alisema Thomas.
Miongoni mwa hoja zilizokusudiwa kwenda kujadiliwa katika kamati kwa kumjadili mkurugenzi huyo kuwa ni pamoja na madiwani hao kudai kutoridhishwa na utendaji wake,kujiuzia magari mawili mali ya halmashauri bila kufuta taratibu,kubadili watumishi katika idara kwa maslahi binafsi na kutowachukulia hatua watendaji wa kata wanalalamikiwa kukwamisha mipango ya maendeleo.
Hoja nyingine ambayo ilitajwa kuwa kusudio kubwa kujigeuza baraza hilo kuwa kamati ni pamoja na mkurugenzi huyo kushindwa kutekeleza maagizo ya serikali ya waraka wa 2008 wa kupunguza wajumbe wa kamati ya fedha kutoka 17 hadi 8 ili kunusuru matumizi ya fedha za umma lakini alishindwa kutekeleza hadi hivi sasa.
Hata hivyo mwenyekiti Magina Magesa,alilishauri baraza hilo kuacha kujigeuza kwa vile tayari kuna tume zimeundwa kuchunguza tuhuma hizo na kusema majibu ya tume hizo yatasadia kupata njia sahihi ya kuchukua dhidi ya wahusika.
“Kuna tume imeundwa na baraza letu linafuatilia mambo ya malambo na miradi mingine pia DC(mkuu wa wilaya) ameunda tume ya kufanya kazi hiyo hivyo hakuna sababu ya kutoa hukumu kwa mtu kabla ya taarifa za tume kuletwa tunasema kamwe hatutakuwa tayari kumvumia yoyote hata kama ni mkurugenzi hizi ni fedha za umma na mali ya halmashauri”alisema Mwenyekiti huyo.
Wakati huo huo kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Musoma mkoani Mara,imepitisha maazimio kadhaa ya kuleta amani katika wilaya hiyo likiwemo la kukabiliana na tatizo kubwa la njaa ambalo limesababisha kila mwaka wilaya hiyo kuomba msaada wa chakula serikalini.
Mwenyekiti wa kamati hiyo kapteni mstaafu Geofrey Ngatuni,alitangaza hatua maazimio hayo katika kikao cha baraza la madiwani la halmashauri ya Musoma vijijini mkoani Mara.
Kapteni mstaafu Ngatuni ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Musoma,alisema katika kukabiliana na njaa ambayo imekuwa ikikosesha amani ya kudumu katika wilaya yake,amesema kamati ya ulinzi na usalama imeagiza kila mjumbe wa kamati hiyo,madiwani na wakuu wa idara katika Manispaa ya Musoma na halmashauri ya Musoma vijijini kuanzisha mashamba ya mfano katika kutekeleza dhana ya KILIMO KWANZA.
Alisema shabaha ya mashamba hayo ya viongozi ni kusaidia kubadili hali ya kilimo cha wananchi wa kawaida na kwamba viongozi hao watalima,kupanda kwa kufuata ushauri wa wataalam wa kilimo na kuvuna wao wenyewe bila kutegemea msaada hatua itasadia kuleta mabadiliko hayo makubwa katika sekta ya kilimo.
Kuhusu matukio ya uhalifu,kiongozi huyo wa wilaya ya Musoma,alisema pamoja na Manispaa ya Musoma hivi sasa kuwa shwari lakini hali ni tofauti kwa halmashauri ya Musoma vijijini kutokana na kushamili vitendo vya ujambazi wa kutumia Silaha,wizi wa mifugo,mauji ya kulipizana visasi na uchukuaji wa sheria mikononi kwa kuuawa watumiwa na kuchoma makazi yao.
Ili kumaliza hali hiyo kapteni mstaafu Ngatuni,aliwaomba viongozi wa kisiasa hasa madiwani kuhamasisha mpango wa ulinzi shirikishi katika maeneo yao na kutambua wazi ni uvunjifu wa katiba kwa kuwaua ama kuteketeza makazi ya watumiwa bila kuwafikisha wahusika katika vyombo vya sheria.
Mwisho
No comments:
Post a Comment