Wednesday, June 29, 2011

VIJIJI SITA VYAUNGANA RORYA

Rorya

WANACHAMA wa umoja unaounganisha vijiji sita UMONI wilayani Rorya mkoani Mara,wameufukuza uongozi na bodi ya umoja huo kwa madai ya kukiuka katiba kwa kushindwa kuitisha mikutano,kukosa umamifu na kusababisha kukwama kwa maendeleo ya umoja huo kwa kipindi cha zaidi ya miaka saba.

Mkutano wa wanachama hao uliitishwa juzi katika kijiji cha Utegi na kuhudhuriwa kaimu mkuu wa wilaya ya Rorya Dickison Michael baada ya wanachama 32 kujiorodhesha majina kwa kuomba kuitishwa mkutano wa wanachama ili kujadili uhai wa umoja huo.

Miongoni mwa viongozi walifukuzwa kwa mujibu wa katiba hiyo ambayo inataka kufanyika kwa uchaguzi kila baada ya mia mitatu ni mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya UMONI FARMERS DEVELOPMENT ASSOCIATION(UFADA) Dk Abdiel Abayo  na  mwenyekiti wa chama hicho Johanes Igogo pamoja na wajumbe wao.

Vijiji hivyo sita vya Utegi,Mika,Omuga,Nyasoro,Nyanduga na Ingiri viliomba serikali kupitia tume ya rauis ya kubinafsisha mashirika ya umma PSRS kununua shamba la mifugo la Utegi.

Hata hivyo wananchi hao walishauriwa kuanzisha kampuni ya kibiashara ya Utegi Dairies  and Farming LTD (UDAFCO)inayomilikiwa wana hisa kutoka UFADA kwaajili ya kununua shamba hilo na kiwanda cha maziwa cha Utegi.

Wakizungumza katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa na wanachama 216 kutoka vijiji vyote vinavyounda UMONI,Joseph Kishe,alisema kuwa katiba ya umoja huo inataka kufanyika kwa uchaguzi mkuu kila baada ya miaka mitatu lakini tangu mwaka 2004 hakuna mkutano wa kawaida ama mkutano mkuu ambao umewahi kuitishwa.

Alisema kuwa kushindwa kutishwa kwa mikutano hiyo kumechangia kudhorotesha maendeleo ya umoja huo,kuongeza umasikini kwa wananchi wa vijiji hivyo hivyo huku migogoro ikizidi kuongezeka kila kukicha.

“Tangu mwaka 2004 viongozi hawa waingie madarakani hakuna mkutano ambao umeitishwa kueleza maendeleo ya chama chetu,lakini awali tuliponunua shamba likiwa na ng’ombe zaidi ya 800,kiwanda cha maziwa tukaanza kupata manufaa kwa kukopeshana lakini sasa hakuna kinachoendelea jambo ambalo limetuletea umasikini mkubwa”alisema Kishe.

Aidha mwanachama mwingine Jamoco Katete,alisema katika mkutano huo kuwa hali ya umasikini imeongezeka mara dufu kwa wanachama hao kutokana mipango mibovu ya uongozi kinyume na malengo ya serikali ya kutoa shamba hilo kwa wananchi ikiwa ni njia moja wapo ya kujikombo na umasikini.

Mwanzilishi wa UMONI mzee Grishon Kimori,ambaye alikuwa mwenyekiti wa muda wa mkutano huo,alisema kutokana na ukikwaji wa katiba hakuna sababu ya kuendelea na uongozi huo hivyo kuwataka wanachama kutoa kauli ambayo itawezesha kumaliza mgogoro na kuharakisha maendeleo ya umoja wao.

“Sisi tumesikitishwa sana sana na viongozi hawa kushindwa kufuata katiba na kutumia mali ya wananchj wanavyotaka,hata kufikia hatua ya kupinga kampuni yetu tuliyoianzisha wana hisa ili kuwezesha kununua shamba hili  sasa tunasema hatuko tayari kuendelea na viongozi hawa hata kidogo”alisema mzee Kimori.

Madiwani wa kata za Koryo Peter Sarungi na Nyathorogo Samwel Maugo,walisema wanachama wa umoja huo wamekuwa wakiishi maisha magumu wakati serikali iliamua kuwapa shamba hilo kuliendeleza katika kupunguza umasikini kwa wananchi.

“Wananchi wanaishi kwa shida hakuna chakula wakati tuna ardhi ya kutosha katika eneo hili..juzi tumeletea trekta 12 na kampuni yetu ya Udafco kwaajili ya umoja wetu ili kusadia shughuli za kilimo lakini trekta hizo hazijatumika  sasa tunasema tumechoka”alisema Diwani Maugo.

Kufuatia malalamiko hayo,kaimu huyo mkuu wa wilaya rorya alitoa kibali cha wanachama hao kupiga kura kwaajili ya kutoa maamuzi ya mwisho ambapo katika kura 216 kura 215 zilifuta viongozi hao kwa kukiuka katiba na kushindwa kuitisha mikutano kwa kipindi cha zaidi ya miaka saba huku kura moja ikipinga.

Kwa sababu hiyo wanachama hao walichagua wajumbe wawili wawili kutoka kila kijiji kwenye vijiji hivyo sita kama kamati ya kufanya maandalizi ya mkutano mkuu wa uchaguzi utakaofanyika baada ya siku 21 kuanzia juzi june 28.

Mwisho

No comments:

Post a Comment