Na mwandishi wetu
MULEBA
Serikali imesema kuwa amani ya nchi inaweza kuwa hatarini endapo hakutakuwa na mkakati wa haraka wa kuwezesha upatikanaji wa ajira kwa makundi ya jamii hasa vijana.
Kauli hiyo ya serikali ilitolewa na jana mjini hapa na waziri wa nchi ofisi ya rais Mahusiano na Uratibu Stephen Wassira,baada ya kutembelea vikundi vya uzalishaji mali vinavyoendeshwa na makundi ya vijana na wanawake kwa kuwezeshwa na mfuko wa maendeleop ya jamii TASAF.
Alisema imebainika idadi kubwa ya vijana hasa wasomi wamekuwa wakijiunga katika maandamano ya mara kwa mara na wakati mwingine kutumiwa na vyama vya siasa kutokana umaskini unaochangiwa na ukosefu wa ajira.
“Hatuwezi kuwa na amani kama kundi la vijana ambao ndio wengi nchini litakuwa halina kazi za kufanya kwani tumekuta tatizo la ukosefu wa ajira ndio chanzo kikuu cha vijana wengi kutumiwa katika maandamano kama sehemu ya ajira yao”alisema na kuongeza.
“Sisi kama serikali tumeanza kuchukua hatua za haraka za kuhakikisha tunaliwezesha kundi hili la vijana na kwa taarifa tu katika utekelezaji wa mradi wa tasaf awamu ya tatu tumepanga vijana wengi kuwezeshwa ili waweze kujiari wenyewe kupitia vikundi vya uzalishaji mali”alisema waziri Wassira.
Alisema katika utekelezaji wa tasaf awamu ya tatu miradi ya vijana itakayonufaika ni ile ya bustani za umwagiliaji kwa vile ndio pekee inaweza kuleta mabadiriko ya haraharaka kiuchumi kwa vijana.
“Tunasisitiza sasa kilimo cha bustani kwani vijana wanataka mapato ya haraka haraka sasa hawawezi kulima mazao ya muda mrefu ndio maana tunasema wajiunge katika makundi kwaajili ya kuwezeshwa na tasaf pia kupitia mifuko maalum kama vile mamilioni ya Jk”alisisitiza .
Hata hivyo waziri Wassira,aliwataka madiwani nchini kote kusimamia kikamilifu fedha za miradi ya maendeleo hasa zile za tasaf ili ziweze kutumika kwa mipango iliyapangwa na si vinginevyo.
Alisema miradi iliyotekelezwa na tasaf awamu ya kwanza nchini chini ya wananchi wenyewe ilionyesha mafanikio makubwa tofauti nay a awamu ya pili ambayo ilikuwa ikitekelezwa kupitia usimamizi wa halmashauri za wilaya.
“Tumebaini kuwapo kwa matumizi mabaya ya fedha za umma ama kwa kutosimamiwa vizuri katika halmashauri nyingi nchini kwani miradi inayoandikwa katika makaratasi sio iliyopo kwa hiyo mingi inatekelwezwa vitabuni sasa kazi yetu madiwani ni kujitoa muhanga kuhakikisha fedha hizi zinafika panapostahili kwa kuzingatia utoaji ajira kwa kundi la vijana”alisema.
Waziri Wassira,alisema ili nchi iweze kuwa na amani ya kudumu ni lazima kundi la vijana likawezeshwa kikamilifu pamoja na viongozi wa wilaya kusimamia mipango yote ya serikali ambayo inalengo la kuondoa umasikini kwa wananchi na si vinginevyo.
“Katika halmashauri za wilaya serikali imekuwa ikileta mabilioni ya shilingi kwa kila bajeti lakini pamoja na mabilioni hayo kuingia halmashauri hakuna mabadiriko yoyote ya kuwakombo wananchi hali hii inawafanya wananchi kukosa imani na serikali yao kwa sababu ya watu wachache tu wanaoshindwa kusimamia fedha za umma”alisisitiza.
Akisoma taarifa za miradi ya tasaf kwa wilaya ya Muleba,kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Pastory Kajuna,alisema miradi 82 imetekelezwa na tasaf awamu ya pili yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2.2 wananchi wakiwa wamechangia shilingi milioni 309.4.
Waziri Wassira yuko mkoani Kagera kwa siara ya siku nne kwaajili ya kukagumia miradi ya tasaf,mkurabita na kuzungumza na makundi maaklum katika jamii hasa viongozi wa dini katika kuhimiza amani hasa wakati huu wa kuelekea katika mchakato wa kuandikwa kwa katiba mpya.
MWISHO
No comments:
Post a Comment