Thursday, December 12, 2013

Sherehe ya Uzinduzi wa siku ya watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania



     B w Onesmo Olengurumwa - Mratibu Wa Kitaifa Wa Mtandao


                                                                  TAREHE 12/12/2013

KUHUSU SIKU YA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU
TANZANIA

Ndugu waalikwa, mabibi na mabwana, mabalozi na wawakilishi wa baadhi ya balozi zilizopo nchini, familia ya watetezi wa haki za binadamu, waaandishi wa habari na wageni wote waliakwa, habari za asubuhi. 

Mhe Mwenyekiti, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) ni Mtandao ambao unajumuisha watetezi wa haki za binadamu hapa nchini. Lengo la Mtandao huu ni kujenga mazingira salama kwa watetezi kufanya kazi zao za utetezi. Malengo makuu ya Mtandao   ni kama ifuatayo.

a)      Mfumo wa kisheria, kisera na hata wa  kiuzoefu, unaotambua na kulinda watetezi wa haki za binadamu na utandaa/ushirikiano wa mashirika yasiyo ya kiserikali kuboreshwa ( Uraghabishi/ Utetezi)        
b)     Uwezo wa waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu umeongezeka na hivyo wanaweza kushiriki kikamilifu katika michakato ya ulinzi kwa watetezi wa haki za binadamu na kushughulikia haki za watetezi wa haki za binadamu (KUJENGA UWEZO).
c)      Utaratibu wa ulinzi imara kupatikana kwa kuwaondoa watetezi katika hatari (USALAMA/ULINZI)
d)      Utendaji bora na endelevu kwa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (UJENZI WA TAASISI)

Mhe Mwenyekiti, Watetezi wanayo haki ya kulindwa na sheria za nchi husika pale wanapokuwa wanatimiza majukumu yao. Lakini utetezi huo usihusishe matumizi ya nguvu, na kitendo chochote cha kutowalinda watetezi ni ni cha uvunjifu wa haki za binadamu. Mpaka sasa Tanzania bado haijaridhia mikataba kadhaa ya kimataifa inayowatambua na kuwalinda watetezi wa haki za binadamu katika mfumo wa sheria zake. Ni kwa sababu hiyo Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania umedhamiria kutumia njia za uraghabishi mbalimbali kupata mafanikio. Ili kukamilisha azma hii Mtandao huu umedhamiria kuwakutanisha wadau mbali mbali katika ngazi ya kitaifa na ngazi ya kimataifa.  Zifuatazo ni baadhi ya shughuli ambazo zimekamilishwa na mtandao huu katika muktadha huu:

Katika utekelezaji wa lengo la kwanza la Mtandao (Advocacy) , Mtandao umeanzisha siku ya Watetezi Tanzania wa Haki za Binadamu hapa nchini kwa lengo la kuongeza utambulisho na ulinzi wa watetezi hapa nchini. Siku hii ya watetezi nchini ni tofouti na siku ya haki za binadamu inayoazimishwa kila mwaka tarehe 10 Disemba. Siku hii ni mahususi kwa ajili ya maslahi, haki na usalama wa watetezi wa haki za Binadamu nchini. Siku hii itakuwa inaazimishwa rasmi kila tarehe 12 Disemba.

Mhe Mwenyekiti, Mtetezi wa haki za binadamu ni mtu yeyote, ambaye kama mtu binafsi au kwa kushirikiana na wengine amejitolea kupigania na kulinda haki za binadamu. Kuwa mtetezi wa haki za Binadamu huhitaji kuwa na shahada wala stashahada kama alivyopata kusema Jaji Mkuu wa Tanzania Othman Chande. Kazi hii ni ya kujitolea, kujituma na wakati mwingine kuweka maisha hatarini kwa ajili ya kutetea wengine. Watetezi wengi hapa nchini wanafanya kazi zao wengi kwa kujitolea, lakini mwisho wake wengi wameitwa wachochezi ama wapinzani.

Watetezi wa haki za binadamu wanatambulishwa na kazi zao na mazingira wanayofanyia kazi ili mradi wanafanya shughuli zao kwa njia ya amani, kwa kuzingatia sheria na miktaba ya kimataifa ninayowalinda hususani Tamko la Umoja wa Mataifa la Mwaka 1998 Kuhusu Watetezi wa Haki za Binadamu.

Mhe Mwenyekiti, Katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia watetezi wakikutana na changamoto mbali mbali. Watetezi wamekuwa mara nyingi wakibambikiziwa kesi mbalimbali, wakipewa majina mabaya kama vile wachochezi au wapinzani, wamekuwa wakitishiwa na wengine kupoteza maisha. Kwa hiyo mkutano huu unamaanisha kwamba mawazo ya aina mbali mbali yatawekwa kwa pamoja kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili watetezi nchini Tanzania.

Lengo la Siku ya Watetezi

·         Lengo kuu la siku ya watetezi hapa nchini ni kuwaweka pamoja watetezi wa haki za binadamu, viongozi kutoka serikalini, washirika katika maendeleo, na washiriki wengineo kutoka sehemu mbali mbali duniani katika eneo hili la haki za binadamu kwa lengo la kujadili kwa kina usalama na maslahi ya watetezi wa haki za Binadamu Tanzania.
·         Siku hii pia itakuwa siku maalum ya kuwatunikia tuzo mbalimbali watetezi wa haki za binadamu, hasa wale waliopata misuko suko mingi wanapokuwa katika kazi za utetezi.
·         Kualikwa kwa wageni mbalimbali kwenye maazimisho ya siku hii, hasa wenye uzoefu katika masuala ya haki za watetezi kutaleta fursa ya kujifunza, na kuangalia namna bora ya kupata ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili watetezi wa Tanzania. Na pia itakuwa nafasi nyingine ya kuangalia jinsi ambavyo tunaweza kuchota weledi na uzoefu wa wenzetu wa Ulaya na maeneo mengine.
·         Pia Lengo lingine ni kuwakumbusha watetezi juu ya majukumu yao na pia kuwaenzi kwa namna mbali mbali wale ambao wameonesha ujasiri na kusonga mbele katika kutekeleza majukumu yao ya kitetezi bila woga pamoja na misukosuko mbali mbali wanayokutana nayo.
·         Siku hii itakuwa siku maalum kwa watetezi kuonyesha kazi zao, kukutana na wadau mbalimbali, kukaa meza moja na serikali na kujadili umuhimu wa watetezi wa haki za binadamu na mashirika yao katika kuzisimamia haki za binadamu nchini.

Mhe Mwenyekiti, Kwa kuwa leo ni siku ya uzinduzi tu, hatutakuwa na mambo mengi ya kufanya ila Mtandao utatoa tuzo 2 kwa watetezi wa haki za binadamu. Tuzo ya kwanza itakwenda kwa Mtetezi wa Haki za Wanawake na Tuzo ya pili itakwenda kwa kwa Mtetezi Bora wa haki za binadamu vijijini. Watu hawa wameteuliwa na mtandao kutokana na kazi zao za utetezi wa haki za wengine. Washindi wa Tuzo hizi wametokana na mapendekezo ya watu waliofanya nao kazi pamoja lakini pia kutokana na utafiti wa mahitaji ya kiusalama kwa watetezi yalifanyika katika mikoa 16 na kuhoji watu 330 katika mashirika 200. Wasifu wa kila mshindi utasomwa baada ya kutangazwa washindi.

Mhe Mwenyekiti, Tunaomba Tume yako iendelee kushirikiana na Mtandao katika kuboresha usalama wa watetezi hapa nchini na maazimisho ya siku hii ya watetezi hapa nchini. Pi tunaomba ofisi yako ingilie kati kifungo cha Mtetezi Bruno Mwambene huko Mbeya.

Hatimaye nawashukuru wote mliohudhuria uzinduzi huu na Mtandao unaomba mzidi kufikiria zaidi siku hii muhimu kwa watetezi hapa nchini.

Na Onesmo Olengurumwa

Mratibu Wa Kitaifa Wa Mtandao
                                        

No comments:

Post a Comment