Friday, December 13, 2013

Sababu za Migogoro katika hifadhi vyaelezwa


 Waandishi wa habari wakiwa kwenye semina-picha na Journo tourism.
 
MAENDELEO duni, uchu wa madaraka, mila potofu na usimamizi mbovu wa sheria kwa wananchi wanaoishi karibu na hifadhi za taifa, imetajwa kuwa ni kichocheo kikubwa cha migogoro kati ya Shirika la Umma la Hifadhi za Taifa nchini (TANAPA), na jamii husika.
Hayo yalibainishwa juzi na mwezeshaji wa semina ya mafunzo kwa waandishi wa habari inayoendelea mjini hapa, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tanzania Audio-Visual and Communication Management, Charles Kayoka, wakati alipozungumzia chanzo cha migogoro.
 
Kayoka alisema hali hiyo inatakiwa kukomeshwa kwa kila mamlaka husika kuwajibika ipasavyo katika suala zima la kusogeza huduma karibu za kimaendeleo kwa jamii yote, ikiwemo inayozunguka hifadhi za taifa.
 
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, mbali na hayo viongozi wa halmashauri zinazozunguka maeneo hayo ya hifadhi za taifa, hawana budi kuwajibika katika kuboresha huduma kwa wananchi wao.
 
“Migogoro mingi katika maeneo ya pembezoni mwa hifadhi za taifa, inasababishwa na mfumo duni wa maendeleo, usimamizi mbovu wa sheria, wanasiasa na mambo mengine kama vile mila potofu.
 
“Kwa hali hii, halmashauri lazima ziwajibike kuhakikisha zinaboresha mfumo bora wa kiuchumi kwa wananchi wao. Suala hili siyo la TANAPA pekee,” alisema Kayoka.
Alisema Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa ikichangia asilimia 17.5 katika fedha zote zinazopatikana katika pato la taifa, hivyo ni lazima maeneo ya hifadhi yaheshimiwe kwa mujibu wa sheria za nchi.
 
Baadhi ya washiriki wa semina hiyo, waliwalaumu waandishi wa habari kwa kufanya kazi zao maeneo ya mijini na kushindwa kufika katika maeneo ya vijijini ambako kuna mahitaji na migogoro mingi.
 
Mhariri wa habari wa gazeti la Rai, Masyaga Matinyi pamoja na Naibu Mhariri Mtendaji gazeti la Jamhuri, Jackton Manyerere, walisema kamwe tatizo la ujangili halitaisha iwapo serikali haitawajibika kuchukua hatua za kisheria kwa wanaoonekana kuhusika na hujuma hizo.

No comments:

Post a Comment