Thursday, June 27, 2013

MKUU WA SEKONDARI ATUHUMIWA KUIBA VIFAA MBALIMBALI VYA SHULE,


Serengeti:
 
ALIYEKUWA Mkuu wa shule ya Sekondari Machochwe wilayani Serengeti Epifan John anatuhumiwa kuiba  vifaa  mbalimbali vya shule  ikiwemo laptop,magodoro,madawati,viti vya plastiki na vifaa vingine.
 
Uongozi wa  kata ya Machochwe ,ofisi ya elimu sekondari,halmashauri na  Mkaguzi wa hesabu wa ndani  umethibitisha kutokea  wizi wa vifaa hivyo.
 
Kwa mjibu wa ripoti ya mkaguzi iliyothibitishwa na ofisi ya elimu sekondari imebainisha vifaa vilivyopotea kuwa ni viti vya mbao kwenye mabano( 86),na kubaki 44,madawati (98)  yameibiwa na kubaki 153,viti vya plastiki (33 ) kubaki 67 na magodoro (61) na kubaki 107.
Vifaa vingine anavyotuhumiwa kuiba ni komputa mpakato(laptop) zote (6 )zilizotolewa na wafadhili mbalimbali kwa ajili ya watoto kujifunzia,komputa kubwa desk top (1) na kubaki 7,Cpu (5)Monitor (5)Keybod 5 zote zilizokuwepo.
 
Diwani wa kata hiyo Samweli Gibewa ameiambia blog  kuwa wizi  huo umebainika mwaka jana wakati anahama,huku  Mkuu wa sekondari aliyehamia hapo Emmanuel Mgini akishiriki kuficha ukweli kwa  kusaini makabidhiano vitu ambavyo havipo kwa lengo la kumlinda.
 
“Niliita bodi ,pamoja na WDC tukakaa na kubaini upotevu wa vitu hivyo… mtuhumiwa akawa hatoi ushirikiano baada ya kuhamishiwa sekondari ya Mbalibali,Mgini alikiri kudanganywa na mwenzake …nikatoa taarifa halmashauri,mkaguzi wa ndani alipotumwa akabaini upotevu huo”anasema  na kuongeza
“Leo(jana )tuna kikao cha WDC nimemwalika Mwenyekiti wa halmashauri maana taarifa ya mkaguzi tunayo sasa …maana suala hili linachangia kurudisha nyuma maendeleo ya elimu…wazazi wanachangia vitu,walimu wanageuza miradi yao”anasema.
 
Mwalimu John alipoulizwa alikiri vifaa hivyo kutoweka,”ni kweli havipo lakini viko kwenye nyumba za walimu…vitarudishwa …maana wengine walikuwa masomoni….nikuahidi kuwa vitarudishwa hivyo vifaa maana nimeishapata taarifa ya mkaguzi…nimeitwa kwenye kikao nitawaambia kuwa nitarudisha”alisema.
 
Alipotakiwa kufafanua ilikuwaje akabidhi vitu ambavyo havipo,na toka mwaka 2012 alipohama ameombwa arudishe bila mafanikio,alisema,”nakwambia vifaa vitarudi baadhi kama magodoro yapo yaliyokwisha “alisema bila kufafanua mangapi yalibaki.
Alipotafutwa siku moja baada ya kikao kutoa ufafanuzi kama amerudisha kama alivyoahidi,alijibu kwa ujumbe mfupi wa simu “kuwa na subira nitakujibu”.
 
Uchunguzi wa Blog hii umebaini  mwalimu huyo aliandikiwa barua ya kutakiwa kueleza mali hizo zilipo akapewa siku 30 ,hakujibu akaandikiwa barua ya kusudio la kuchukuliwa hatua za kisheria ,lakini akarejesha Laptop 6 mbovu zikakataliwa.
 
Aidha mkuu wa shule aliyepo Mgini ameazimiwa na kikao cha halmashauri achukuliwe hatua za kinidhamu kwa kushiriki wizi huo kwa kusaini  vitu hewa,hali ambayo inaonyesha walikuwa na dhamira moja.
 
Uchunguzi zaidi umebaini katika kikao cha kamati ya Uchumi,ardhi na Mazingira ya baraza la madiwani iliyoketi juni 25 mwaka huu imeazimia Mwalimu huyo kuvuliwa madaraka,ndani ya siku 30 awe amerudisha vitu vyote vilivyopotea,au apelekwe mahakamani.
Sekondari ya Machochwe ndiyo inaongoza kwa kuchangia harambee nyingi,na  ilikuwa miongoni mwa shule mbili na Natta zilizoandaliwa kuwa kidato cha tano na sita,na baada ya uchaguzi wa mwaka 2010 kata hiyo kuchukuliwa na Chadema , baraza la madiwani liikabadili uamzi na kuchagua shule zingine ambazo hazikuwa zimeandaliwa .
Wimbi la wakuu wa shule kufuja mali za umma linaendelea kutikisa wilaya hiyo hasa ,hivi karibuni aliyekuwa mkuu wa sekondari Nyambureti Patrick Majige kwa kushirikiana na ofisa elimu sekondari William Makunja walichota sh.mil.9 za ujenzi wa nyumba na haikujengwa,baada ya ukaguzi kubaini alihamishiwa Mugumu sekondari,kisha kusimamishwa.
Hata hivyo baada ya kusimamishwa  aliwasilisha barua ya kustaafu na kupitishwa,huku ofisa aliyeidhinisha fedha za ujenzi wa nyumba kutumiwa kwa posho za safari akiendelea na kazi kama kawaida.
Sekta ya elimu ni miongoni mwa sekta 6 za vipaumbele ambapo Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika semina ya wakuu wa mikoa aliahidi atakaye shindwa kusimamia atafukuzwa kazi.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment