Tuesday, May 21, 2013

UHURU WA VYOMBO VYA HABARI UWE NA MIPAKA.

IMG_1475Na Zawadi Msalla-MAELEZO Dodoma
Vyombo vya Habari nchini vimeaswa kutumia uhuru wake vizuri bila kusababisha madhara ndani ya nchi kama ilivyotokea katika baadhi ya nchi za Afrika.
Akichangia hotuba ya wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Mhe.Jaddy Simayi Jaddy mbunge wa Mkwajuni alisema baadhi ya vyombo vya habari vilivyopo hapa nchini vinaweza  kuchangia machafuko ndani ya nchi kwani mwelekeo wa mambo yanayoandikwa yana dalili ya uchochezi.
Alisisitiza kuwa hata kama wananchi wanavihitaji vyombo vya habari lakini vikiachiwa vifanye vinavyotaka vitaipeleka nchi pabaya. “Ni kweli tunavihitaji sana vyombo hivyo ila kwa sasa inabidi viangaliwe kwa umakini sana” Alisema mchangiaji.
Aliiomba Serikali iwasilishe sheria ya vyombo vya habari kama ilivyo ahidi ili kuweza kudhibiti baadhi ya mambo yasiyo sahihi yanayoonekana kwa sasa kwenye vyombo vya habari.
Akielezea uwezo wa vyombo vya habari alisema vyombo hivyo vina nguvu kubwa katika kujenga nchi na kuleta maendeleo ya nchi yeyote ile duniani.
Naye Mbunge wa Bunda Mh. Stephen Wasira  akichangia hoja hiyo alisema uhuru lazima uwe na mipaka . Kama hakuna nidhamu ya vyombo vya habari uwepo wa demokrasia inapotea.
Alisema Tanzania ni kati ya nchi inayojali uhuru wa vyombo vya habari kwani mpaka sasa ni nchi pekee Afrika Mashariki iliyo na vyombo vingi vya habari. Takwimu zinaonesha mpaka sasa kuna jumla ya magazeti na majarida 781, magazeti yanayotoka kila siku 13 na magazeti na majarida yanayotoka kwa wiki 62 na kuongeza kuwa hiyo ni moja ya mafanikio makubwa ya kutekeleza uhuru wa Vyombo vya Habari nchini.
Hata hivyo aliwaomba waandishi wa habari waache kuandika habari zisizo na ukweli ndani yake kwani wanao athirika na hilo ni wengi. Alisema uandishi wa habari ni taaluma hivyo wanaoitumikia taaluma hiyo inawapasa kufanya kazi kwa weledi na kufuata kanuni na taratibu za taaluma hiyo.
Akichangia hoja ya vijana alisema vijana ni Taifa la leo. Iwapo Serikali itatoa kipaumbele kwa vijana ajira itapatikana. Hata hivyo aliisifu Serikali kwa jitihada inazochukua za kusaidia vijana katika mikopo inayo wanyanyua, mpango mkakati wa maendeleo ya vijana ni moja ya njia ya kuinua vijana nchini.

WABUNGE WAITAKA SERIKALI KULETA HARAKA MUSWAADA WA VYOMBO VYA HABARI

IMG_1656Na Lydia Churi- MAELEZO-DODOMA
Baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameitakaSerikali kuharakisha kuulet
a bungeni Muswada wa Sheria ya Kusimamia Vyombo vya Habari ili kuhakikisha waandishi wa habari wanatekeleza majukumu yao kwa kufuata maadili na misingi ya taaluma hiyo.
Wakichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na  Michezo kwa nyakati tofauti, wabunge hao waliipongeza wizara hiyo kwa kuridhia Sheria ya Kusimamia Vyombo vya Habari kwa kuwa itasaidia kuikuza na kuiimarisha taaluma ya habari nchini.
Akichangia hotuba hiyo mbunge wa viti Maalum (CCM) Esther Bulaya alisema wakati umefika kwa waandishi wa habari nchini kuandika habari kwa kuzingatia maadili ya taaluma hiyo ikiwa ni pamoja na kuandika habari zilizofanyiwa utafiti wa kina na zinazohusisha pande mbili za chanzo cha habari.
Mhe. Bulaya  amewataka waandishi wa habari wasitumie vibaya uhuru wa habari kwa kutoa habari zinazoshabikia vyama vya siasa na zenye kuleta chuki zitakazowafanya vijana kujenga taifa la visasi. Aliongeza kuwa taifa ni zaidi ya vyama vya siasa.
Naye mbunge wa Kondoa Kusini, Mhe. Juma Nkamia alisema kupatikana kwa sheria ya kusimamia vyombo vya habari kutasaidia kuondokana na tatizo lililopo sasa la kuwa na waandishi wa habari wengi wasiokuwa na sifa maarufu kama ‘makanjanja’.  
Akizungumzia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Nkamia aliitaka serikali kupitia wizara ya habari kuhakikisha inafanya kila liwezekanalo kuyamalizia majengo yaliyopo Mikocheni ambayo yametelekezwa kwa muda mrefu. Aliongeza kuwa majengo hayo yaliwekwa jiwe la msingi na Rais wa awamu ya pili Mzee Ali Hassan Mwinyi lakini mpaka sasa ni Serikali ya awamu ya nne na majengo hayo hayajakamilika.
Mhe. Nkamia pia aliitaka serikali kuiongezea bajeti TBC ili iweze kununua vifaa vipya na vya kisasa vya kurushia matangazo kwa kuwa vifaa vilivyopo vimechakaa. Aliongeza kuwa matangazo ya TBC hivi sasa hukatika katika kutokana na tatizo hilo.
Akiwasilisha hotuba ya Bajeti, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara aliliambia bunge kuwa serikali imeridhia kutungwa kwa Sheria ya Kusimamia Vyombo vya habari na muswada wa kutunga sheria hiyo utawasilishwa bungeni hivi karibuni.

No comments:

Post a Comment