Thursday, May 23, 2013

CHINUA ACHEBE AZIKWA LEO NIGERIA


Mwili wa mwandishi mashuhuri wa vitabu barani Afrika Chinua Achebe umewasili nyumbani kwake katika jimbo la Anambra nchini Nigeria.
Achebe atazikwa hivi leo Alhamisi

Hafla mbali mbali zimekuwa zikiandaliwa nchini Nigeria kumuenzi bwana Achebe.
Mwandishi huyo mashuhuri alifariki mjini Boston,Marekani, akiwa na umri wa miaka 82 baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Jamaa na maafisa wa serikali walikuwa katika uwanja wa ndege Kusini mwa Nigeria kumpokea marehemu.

Hayati Achebe, anasifika sana kwa kuwa mwanzilishi wa fasihi ya kiafrika kwa kiingereza.
Kitabu chake alichokianda cha kwanza, mwaka 1958, Things Fall Apart, ambacho kilizungumzia sana athari za ukoloni barani Afrika, aliweza kuuza zaidi ya vitabu milioni kumi.

Mwandishi huyo na msomi, aliendelea na uandishi wake na kuandika vitabu vingine 20 baadhi vikikosoa sana wanasiasa na kile alichokitaja kama ukosefu wa uongozi nchini Nigeria.
Alikuwa anaishi nchini Marekani tangu mwaka 1990 baada ya ajali ya barabarani kumjeruhi kiasi cha kumlemaza.

Makundi ya kitamaduni yalifanya tamasha mbali mbali nje ya uwanja wa ndege wa Enugu, huku ndege iliyokuwa inambeba marehemu Achebe ilipotua.

Inaarifiwa kuwa licha ya kuwa watu wana majonzi tele, lakini pia wanasherehekea maisha ya mwandishi huyo.

Achebe atazikwa karibu na nyumbani kwa familia yake mjini Ogidi, mji mdogo kwenye vilima vya jimbo la Anambra

No comments:

Post a Comment