Monday, December 10, 2012

WAZEE WA MUSOMA WANG'AKA,HAKUNA WATU 17 WALIOCHINJWA

*Wataka mwandishi aliyeandika habari hiyo akamatwe
 *Siasa zaharibu Manispaa hiyo
 *Kaimu kamanda wa Polisi katika wilaya hiyo Lucas Hupa asema  matukio yaliyoripotiwa ni matatu na sio ya kuchinjwa

 Wachungaji wa Makanisa mbalimbali Manispaa ya Musoma, Mkoa wa Mara wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya hiyo, Jackson Msome (hayupo Pichani) baada ya Wazee, viongozi, Mashehe na Wachungaji kukanusha habari za watu 17 kuchinjwa.



 Wazee wa Manispaa ya Musoma wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya hiyo Jackson Msome (Hayupo Pichani) baada ya wazee hao kupinga vikali taarifa zilizochapishwa kwenye baadhi ya Vyombo vya Habari na kutangazwa kuwa watu 17 wachinjwa Musoma.
 Wazee waliofurika katika ukumbi wa Chuo cha Waganga Manispaa ya Musoma waliojitokeza kwa ajili ya kupinga habari za upotoshaji na uzushi zilizotangazwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini kuwa watu 17 wachinjwa musoma.
 Mkuu wa Wilaya Jackson Msome akisoma gazeti la Mtanzania ambalo hivi karibuni lenye kichwa cha habari Watu wachinjwa Musoma. Ambapo wananchi wa Manispaa hiyo kuingiwa na hofu na kusababisha baadhi ya wanafunzi kugoma kwenda shuleni kuogopa kuchinjwa. 
 Mkuu wa Wilaya ya Musoma Jackson Msome Akizungumza jambo mbele ya Wazee, Viongozi Mbalimbali, Mashehe na wachungaji (Hawapo Pichani) wakati akizungumza nao kwenye ukumbi wa Chuo cha waganga Manispaa hiyo.
 Katibu wa NCCR Mageuzi Mkoa wa Mara Tabu Said akimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Musoma Jackson Msome wakati akizungumza na wazee, viongozi, wachungaji na mashehe hivi karibuni.

Na Thomas Dominick,
Musoma

WAZEE, Viongozi wa vyama vya Siasa na Serikali, Wachungaji na Mashehe Wilaya ya Musoma, Mkoa wa Mara wamekanusha vikali taarifa zilizochapishwa kwenye baadhi ya magazeti na Televisheni nchini kuwa ndani ya wilaya hiyo watu 17 wakiwemo wanawake 5 wamechinjwa kati ya Oktoba hadi Desemba mwaka huu.

Wazee hao pia waliiagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo kumkamata mwandishi wa habari hizo ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria kutoa ushahidi wa watu waliochinjwa kisha kumfikisha mahakamani kujibu mashitaka ya kuandika habari za uzushi na uchochezi na kuwatia hofu wananchi.

Wakizungumza na Mkuu wa Wilaya hiyo Jackson Msome na kamati yake ulinzi na usalama kwenye kikao cha dharura kilichofanyika kwenye ukumbi wa chuo cha Waganga katika Manispaa hiyo wazee hao kwa kauli moja walimuhakikishi Mkuu wa wilaya hiyo kuwa habari hizo ni za uzushi zenye kuwatia hofu wananchi.

“Ukisoma kwenye haya magazeti utagundua habari hii imekaa kisiasa kwani hata Mbunge wa Chadema Vicent Nyerere anadiriki kusema kuwa anamtaka IGP said Mwema akomeshe mauaji hayo pia kamati ya ulinzi na usalama imekalia siasa huu ni uzushi na tunapinga kama kuna ukweli tunaomba otoe ushahidi kwa kuonyesha maiti zilizochinjwa,”alisema Mzee Seleman Kerenge.

Alisema kuwa vyombo hivyo vya habari vinalengo vya kuvuruga hali halisi ya amani na usalama ndani ya mji wa Musoma na kudai kuwa hakuna mtu yeyote aliwahi kuchinjwa ndani ya Manispaa hiyo.

Mzee Abdu Husein wa Makoko alisema kuwa wazazi wengi nchini hawapendi kutoa matatizo ya watoto wao hata kama wanashiriki katika vitendo viovu ambapo wanazua matatizo makubwa kwenye jamii.

“Tuna mapungufu makubwa sisi kama wazazi hata kama unajua matatizo ya vijana wako hutaki kusema ukweli, wazazi wengi hata vikao na vijana wao hawafanyi, tuna mamlaka lakini hatuyatumii,”alisema Husein kwa hasira kubwa.

Akitoa taarifa mbele ya wazee na mkuu wa wilaya Kaimu kamanda wa Polisi katika wilaya hiyo Lucas Hupa alisema kuwa matukio ambayo yalitokea katika kipindi cha mwezi Oktoba na Novemba ni matatu.

Alisema kuwa tukio la kwanza lilitokea Oktoba 19, Enock ambaye
alikuwa mlinzi alifariki dunia katika Hospitali ya Mkoa wa Mara baada ya kukatwa kwa mapanga na watu wanaodaiwa kuwa majambazi.

Tukio la pili lilitokea Oktoba 28, mwaka huu ambapo Msichana Lilian Bonifance (12) aliuawa na watu wasiojulikana na mwili wake kutupwa na tukio la mwisho lilitokea Novemba 21 ambapo mlinzi wa kampuni ya ulinzi ya Salama aliuawa na watu wanaodai kuwa majambazi.

Hupa alisema kuwa tayari jeshi hilo linawashikilia watu 16 na
watuhumiwa nane walisomewa mashitaka ya mauaji na kupelekwa magereza.

Naye Mkuu wa Wilaya Msome alisema kuwa kuna matukio yapo ndani ya wilaya hiyo lakini sio kama inavyozungumzwa kwa sasa ambapo ni hali ya kuwatisha wananchi wa Manispaa hiyo.

“Waandishi wa habari ni ndugu zetu wote tunafanya kazi kwa kuwatumikia wananchi tuache kuandika habari za uzushi na uchochezi ambazo zinatia hofu wananchi wetu,”alisema Msome.

Msome alisema kuwa Waandishi wa habari hawajaitendea haki Manispaa hiyo kutokana na habari hiyo ambayo alisema kuwa ni ya uzushi na kuwaomba kuandika habari sahihi ambazo hazipotoshi umma.

“Madhumuni ya vyombo vya habari na kazi ya mwandishi wa habari ni kufundisha, kuburudisha na kuelimisha sio kupotosha na kuchochea hayo sio maaili ya uandishi wa habari,”alisema.

Baada ya ukanushaji wa mauaji hayo Msome amewaomba wazee, Viongozi naViongozi wa dini kushirikiana na kuanzisha ulinzi shirikishi ili kuepukana na uzushi kama huo uliotokea ambapo ataanza na mafunzo juu ya ulinzi huo ambao yataanza Desemba 13 mwaka huu kwa kata nne za Iringo, Mkendo, Kitaji na na zingine zitafuata.

Taarifa ambazo hivi karibuni zilitolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara kupitia kwa Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa huo, Japhet Lusingu kuwa ni matukio mawili ya watu kuchinjwa ndiyo yaliyoripotiwa na yalitokea katika Wilaya ya Butiama na sio watu 17 kama ilivyotangazwa.

Tukio la kwanza ni mwanawake aliyetambulika kwa jina la Blandina Peru (28) mkazi wa kijiji cha Mahare, kata ya Etaro aliuwawa Desemba 2 mwaka huu kwa kukatwa koromeo na kubakwa na wauaji kabla ya kumuua wakati akiwa porini akikata kuni na watuhumiwa wa tukio hilo bado hawajakamatwa.

Tukio la pili lilitokea Kijiji cha Kabegi, Kata ya Nyakatende, Wilaya hiyo hiyo ambapo Sabina Mkireri (44) mkazi wa kijiji cha kiemba aliwawa kwa kuchinjwa shingo na kichwa chake kuchukuliwa na watu wasiojulikana katika kijiji cha kabegi na watu sita wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano.


No comments:

Post a Comment