JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI
JESHI LA POLISI TANZANIA
Anuani ya Simu “MKUUPOLISI”
Ofisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi,
Simu : (022) 2110734 Makao Makuu ya Polisi,
Fax Na. (022) 2135556
S.L.P. 9141,
Unapojibu tafadhali taja: DAR ES SALAAM.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
DAR ES
SALAAM DISEMBA 24, 2012.
1. Jeshi la
Polisi Nchini, linawakumbusha wananchi wote kuwa, tunapoelekea kipindi hiki cha
sikukuu za Christmas na Mwaka Mpya itakayoadhimishwa kati ya tarehe 24-26 Disemba,
2012 na tarehe 01 Januari, 2013 wanatakiwa kusherehekea sikukuu hizo kwa amani
na utulivu pasipo vitendo ama viashiria vyovyote vya uvunjifu wa sheria. Wananchi wote wachukue tahadhali kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kuhakikisha
kuwa vitendo vyote vya uhalifu na wahalifu kwenye maeneo mbalimbali
vinadhibitiwa.
2. Ikumbukwe kuwa,
wananchi wenye imani ya Kikristo na hata madhehebu mengine hutumia muda huo
kwenda kuabudu pamoja na muendelezo wa sherehe hizo kwenye maeneo mbalimbali ya
starehe, uzoefu unaonyesha kuwa baadhi ya watu hutumia kipindi hicho cha
sikukuu kufanya matukio ya uhalifu kutokana na mikusanyiko hiyo ya watu.
3. Jeshi la Polisi
limejipanga kikamilifu kuhakikisha kwamba wananchi kote nchini wanasherekea sikukuu
hizo kwa amani na utulivu, ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo yote ya kuabudia,
fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine yote ambayo yatakuwa na
mikusanyiko mikubwa ya watu.
4. Aidha, tunawatahadharisha
wale wote ambao watakuwa wakitumia barabara, kuwa makini kwa kuzingatia sheria
za usalama barabarani, madereva kuepuka kwenda mwendo kasi na kutumia vilevi
wawapo kazini.
5. Katika
kuhakikisha usalama kwenye kumbi za starehe, wamiliki wa kumbi hizo wazingatie
uhalali na matumizi ya kumbi zao katika uingizaji wa watu kulingana na uwezo wa
kumbi hizo, badala ya kuendekeza tamaa ya fedha kwa kujaza watu kupita kiasi. Vilevile,
wazazi wawe makini na watoto wao na hasa disko toto na kutokuwaacha kutembea
peke yao, ili kuepuka ajali na matukio mengine yanayoweza kusababisha madhara
juu ya watoto hao.
6. Wananchi wote wanakumbushwa
kwamba, watokapo kwenye makazi yao wasiache nyumba wazi ama bila mtu na endapo
kuna ulazima wa kufanya hivyo watoe taarifa kwa majirani zao, na pale
wanapowatilia mashaka watu wasiowafahamu wasikae kimya bali watoe taarifa kwa
Jeshi la Polisi ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa haraka kwa wahusika
kupitia namba simu 0754 785557 ama
namba za viongozi wa polisi zilizokwishatolewa hapo awali.
7. Jeshi la Polisi
linatoa wito kwa taasisi mbalimbali za serikali, madhehebu ya dini, asasi za
kiraia, vyama vya siasa, vyombo vya habari, makampuni binafsi ya ulinzi na wananchi
kwa ujumla, kuendelea kutoa ushirikiano na hasa katika kipindi cha mwisho wa
mwaka, ili kuhakikisha usalama wa nchi yetu unadumishwa na raia wote wema
wanaishi kwa amani na utulivu bila hofu ya uhalifu.
8. Mwisho, nawahakikishia
wananchi kwamba, Jeshi la Polisi linatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia
sheria za nchi na hivyo halitawajibika kumwonea huruma ama upendeleo mtu yeyote
atakayeenda kinyume na sheria.
NAWATAKIENI
WATANZANIA WOTE KHERI YA CHRISTMAS NA MWAKA MPYA.
Imetolewa na:
Advera Senso-ASP
Msemaji wa Jeshi la Polisi (T)
POLISI MAKAO MAKUU.
No comments:
Post a Comment