Friday, August 17, 2012


WATAALAMU  WA MIPANGO MIJI  TARIME WADAIWA KUUZA ENEO LA SERIKALI.


Dinna Maningo,Tarime.


MAMLAKA ya Mji mdogo Tarime imeunda kamati ndogo  kwa ajili ya kuchunguza eneo la wazi  la Serikali lililoko kitongoji cha Mwangaza kata ya Nyamisangura Wilayani Tarime uliodaiwa kuuzwa na wataalamu wa mipango miji na ardhi wa mamlaka ya mji mdogo  kwa kanisa la  EAGT Tarime.


Uamuzi huo wa kuundwa kwa kamati ndogo umekuja baada ya kudaiwa kuwa kuna uwanja  wa wazi uliotengwa na Serikali kwa ajili ya kujengwa Zahanati na shule ya awali lakini matokeo yake wataalamu wa ardhi wa mipango miji wameuza eneo hilo la wazi kwa kanisa la EAGT.


Wajumbe wa Baraza la mamlaka hiyo walisema kuwa wameshangazwa kwa kitendo cha wataalamu kuuza eneo la Serikali kwa kanisa  huku wakijua  eneo hilo lilitengwa kwa ajili ya Shule na Clinic.


“Mwaka  1998 nikiwa Mwenyekiti wa eneo la mwangaza Serikali ilitenga eneo  la wazi kwa ajili ya kijengwa  shule na zahanati Serikali ikatoa fidia  kwa watu wakahamishwa kupisha eneo leo hii wataalamu wa mipango miji na ardhi wamepima eneo wanasema ni lakanisa!


Aliongeza”ndugu Mwenyekiti tunaomba kamati ndogo iundwe kuchunguza swala hili hapa kuna jambo limejificha kuna rushwa imetumika na istoshe nina nyaraka za watu waliolipwa fidia na Serikali tofauti inavyoelezwa sasa kuwa kanisa la EAGT ndilo limelipa wananchi fidia  kupisha eneo”alisema mwenyekiti wa kitongoji cha Ronsoti Chacha Kisanta.


Ofisa mipango miji wa mamlaka ya mji mdogo Tarime Nzengula Wilfred alisema kuwa  eneo hilo la EAGT taratibu zote zilifuatwa kutoka kwa kamishna  wa Ardhi na kwamba tatizo la ufahamu mdogo wa wajumbe kuhusu maswala ya ardhi ndiyo chanzo cha kuibua migogoro.


Hata hivyo maelezo ya Ofisa mipango miji yaliwakwaza wajumbe ambapo walimtaka ofisa huyo kufuta kauli yake kwa kile alichodai kuwa wajumbe wana uwelewa mdogo kuhusu ardhi.


Mwenyekiti wa kitongoji cha Mwangaza Joseph Maseke  na wajumbe wengine wakaomba watafutwe watu waliolipwa fidia na Serikali mwaka 1998 ili kuthibitisha  kwakuwa wapo hai kutokana na madai ya kanisa la EAGT kudai kuwa wao ndio waliolipa fidia wananchi.


“ Tuna akiri timamu! sisi si wanjiga uzuri watu waliolipwa fidia wapo hai tuwatafute watupe hali halisi tujue ni taratibu zipi zilitumika  hadi kanisa likamilikishwa  eneo la wazi kwani tumekuwa tukiona wataalamu wakifika kwenye maeneo wanapima bila hata kuwahusisha wenyeviti wa vitongoji, na mitaa na hili tatizo ni kwasababu maeneo mengi hayana hati miliki basi hilo kanisa lingejenga shule au zahanati kama ilivyokuwa kipaumbele cha Serikali!alisema Maseke.


Hali hiyo ya wajumbe  wote kuwalalamikia wataalamu kwa kuuza eneo la Serikali na kuomba iundwe kamati ndogo ya uchunguzi Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo Tarime Christopher Mantago alichagua kamati ndogo ya wajumbe 6 watakaofanya uchunguzi kati yao 3 wanaotokea eneo la Ronsoti na mwangaza kuliko na kanisa la EAGT,wajumbe wawili kutoka mamlaka ya mji mdogo na mmoja kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

.........   .........  ..........  ..........   ...........  ................. 


MAMLAKA YA MJI MDOGO TARIME YAONGEZA  MAKUSANYO.

Dinna Maningo,Tarime.

MAMLAKA ya Mji Mdogo wa Tarime kupitia vyanzo vyake vya ndani vya mapato imekusanya jumla ya 220,788,095.97 sawa na asilimia 85% ya kiasi kilichokuwa kimekasimiwa kipindi cha mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 mwezi juni  2012.

Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Tarime Christoper Mantago wakati wa kikao cha wajumbe wa baraza la mamlaka ya mji huo,Mantago alisema kuwa  kwa kipindi hicho mamlaka ya mji ilikisia kutumia jumla ya 260,026,600 na kiasi halisi kilichotumika ni 212,811,995.95 sawa na asilimia 82 ya matumizi yaliyokasimiwa.

Pia Mantago alisema kuwa katika  upande wa usafi wa mazingira mamlaka hiyo imefanikiwa kushika nafasi ya sita Kitaifa na kwamba malengo yao ni kushika nafasi ya kwanza.
Mantago alisema kuwa pamoja  na juhudi hizo za mamlaka katika makusanyo bado mamlaka hiyo inakabiliwa na tatizo la kutokuwa na baadhi ya wataalamu wanaohitajika hususani mwanasheria na muhandisi wa ujenzi.

Aliongeza kuwa baadhi ya wafanya biashara wanaotumia vibanda vilivyoko soko kuu na stendi ya mabasi kwa kutokuafikiwa kusaini mkataba utakao wawezesha kulipa mamlaka ya mji kodi ya vibanda.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime John Henjewele aliipongeza mamlaka hiyo kwa makusanyo mazuri ya mapato kupitia vyanzo vyake vya ndani ambapo aliwataka kuzidi kuongeza zaidi makusanyo huku akisisitiza siasa isihusishwe katika maendeleo ndani ya mamlaka ya mji mdogo wa Tarime kwani inakwamisha maendeleo.

No comments:

Post a Comment