WANA CCM WATAKIWA KUKUBALIANA NA MATOKEO KATIKA CHAGUZI
Na Shomari Binda
Musoma.
Mjumbe wa Halimashauri kuu ya CCM Taifa (NEC) kutoka Mkoa wa Mara
Vedastus Mathayo amewataka wana CCM kukubaliana na matokeo katika
uchaguzi wa ngazi ya Chama kuanzia ndani ya Jumuiya ili kuepusha makundi
ambayo yanaweza kujitokeza na kuibua malumbano yasiyo na msingi.
Kauli hiyo ameitoa jana wakati akifungua mkutano mkuu wa uchaguzi
wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM Musoma Mjini (UWT) katika ukumbi wa
mikutano wa CCM katika Makao makuu ya chama hicho Mjini Musoma.
Amesema mwanachama yeyote anapoingia katika kinyang'anyiro cha uchaguzi
ni budi kukubaliana matokeo ya namna mbili kushinda na kushindwa na
kuacha kujiingiza katika makundi ya kutafuta mchawi mara baada ya
uchaguzi.
Amedai kushinda na kushindwa ndio maana ya uchaguzi
na kuwataka wale walioomba nafasi kukubali matokeo ya namna hizo mbili
na kutoa ushirikiano kwa wale walioshinda katika kufanya kazi za jumuiya
na zile za Chama katika shughuli za kila siku.
Mathayo amesema
kujiingiza katika makundi yakutafuta sababu za kushindwa mara baada ya
uchaguzi kutaibua mambo ambayo yataweza kukidhohofisha chama na
kushindwa kufanya mambo ya msingi katika kukijenga.
Uchaguzi wa
jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT) umefanyika jana katika Wilaya zote za
Mkoa wa Mara huku Wanawake wa Chama hicho wakiwania nafasi mbalimbali
huku uchaguzi mwingine wa Jumuiya ya Vijana wa Chama hicho (UVCCM)
ukitarajiwa kufanyika siku ya kesho.
Katika hatua nyingine
Mjumbe huyo wa Halimashauri kuu ya CCM Taifa (NEC) Vedastus Mathayo
amechukua fomu ya kutetea nafasi yake katika Ofisi ya CCM Musoma Mjini
na kusema kuwa kila Mwanachama wa Chama hicho anayo haki ya kuomba
nafasi yeyote ya uongozi ndani ya Chama
No comments:
Post a Comment