Friday, August 24, 2012

HALI MBAYA YA HEWA BAHARINI, WAVUVI WAWILI WA KOMORO WAIBUKIA ZANZIBAR

Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi Zanzibar

ZANZIBAR IJUMAA AGOSTI 24, 2012. Wavuvi wawili Raia wa Komoro, wamekutwa katika Kisiwa Kidogo cha Pungume nje kidogo ya Zanzibar wakiwa hoi kwa uchovu na njaa baada ya kupotea na kuishi baharini kwa muda wa siku 11 bila ya chakula.

Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi Zanzibar Kamishna Msaidizi ACP Yusufu Ilembo, amewataja wavuvi hao kuwa ni Othman Inzudin(24) na Nurdin Ahmed(18) ambao wote ni Raia wa Komboro.

Amesema kuwa wavuvi hao wakiwa na boti ndogo katika shughuli zao za uvuvi huko nchini Komoro, walipatwa na misukosuko ya mawimbi na upepo mkali na kupotea baharini hadi boti yao kuishiwa mafuta.

Amesema kutokana na hali hiyo, vijana hao walijikuta wakiishi majini kwa muda mrefu bila ya chakula wakinywa maji chumvi ya bahari huku wakienda kwa kufuata mwelekeo wa upepo na mawimbi ya bahari hadi walipohika katika kisiwa hicho cha Pungume kilichopo kusini mwa Zanzibar.

Amesema vijana hao wamelazimika kufungua ingini ya boti yao na kuitosa majini kama njia ya kuifanya boti yao kuwa nyepesi ili isukumwe na mawimbi kwa urahisi na kuweza kutokea nchi kavu kunuusuuru maisha yao.

Hata hivyo Kamanda Ilembo amesema kuwa baada ya kuokolewa, wavuvi hao walipelekwa katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja kwa matibabu.

Lakini amesema kwa bahati mbaya Nurdin Ahmed alipoteza maisha wakati madaktari wakiwa katika harakati za kuokoa maisha yake.

Amesema Jeshi la Polisi limewasiliana na ubalozi wa Komoro hapa nchini ili kuona uwezekano wa kumsafirisha kijana mmoja aliyebaki pamoja na mwili wa marehemu hadi nchini kwao Komoro ambako zitafanyika taratibu za mazishi.

Nao Madaktari na Wauguzi wa zamu katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja, Dk. Mohammed Hassan Haji na Dk. Mkasi Khatib Makame, wamesema jambo lililosababisha kifo cha kijana huyo ni uchovu, njaa na hali ya kukata tama kwa wasiwasi.

Hata hivyo Wauguzi hao wamesema kuwa hali ya kijana mmoja aliyebaki wodini hapo inaendelea vizuri baada ya matibabu ikiwa ni pamoja na kumuongezea maji mwilini na kupatiwa chakula ili kurudisha nguvu mwilini. 

Mwisho


SERIKALI YA JAMHURI YAOMBWA KUISADIA ZANZIBAR KATIKA WAZO LAKE LA UNUNUZI WA MELI KUBWA YA MIZIGO NA ABIRIA.

Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi
ZANZIBAR IJUMAA AGOSTI 24, 2012. Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imeshauriwa kuungana na Serikali ya Zanzibar katika nia yake ya kununua meli kubwa kwa ajili ya mizigo na abiria ili kutoa huduma bora ya usafiri kati ya Dar es Salaam, Zanzibar na Pemba na kuepusha ajali za mara kwa mara.

Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa Mipango na Sera wa Chama cha Wakulima Tanzania Kanda ya Zanzibar Bw. Rashid Yusufu Mchenga, ambapo amesema kuwa, pamoja na nia nzuri ya Serikali ya Mapinduzi ya kununua meli kama huku ikijibana kibajeti kwa kiasi kikubwa.

Bw. Mchenga amesema maafa yaliyotokea kwa siku za hivi karibuni kutokana na kuzama kwa meli kubwa tatu za abiri za Mv. FATIHI,  Mv. SPAICE SLANDER na MV SKAGIT inatokana na Serikali yenyewe kutokuwa na meli ya uhakika.

Amesema kuwa matokeo ya ajali hizo yamewagusa karibu Watanzania wote na hivyo ukimya ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano katika suala la ununuzi wa meli kubwa ya Serikali ya mizigo na abiria haileti picha nzuri kwa wananchi wake wanaotegemea usafiri wa majini kwao pamoja na mali zao.

"Tumechoka kuona ama kusikia Watanzania wanapoteza maisha na mali zao kwa uzembe unaoweza kuepukika". Alisema Bw. Mchenga.

Amesema kuwa katika kifungu namba 14 cha katiba ya Muungano kinaelezea wazi kabisa juu ya haki ya kuishi na hivyo ajali za mara kwa mara zinazokatiza maisha ya Watanzania wenzetu, ni kinyume na sheria hiyo.

Bw. Mchenga amesema kama ilivyo katika kuimarisha huduma ya usafiri wa treni za abiria na mizogo kwa mikoa ya Tanzania bara, pia kuna haja Serikali  kuona uwezekano wa makusudi wa kuimarisha usafiri wa abiria na mizigo majini kwa maana ya bahari, maziwa na mito.

Amesema usafiri kwenye Maziwa kama Viktoria, Tanganyika, Nyasa na katika vivuko kwenye mito mikubwa kama Kirombero, Wami, Kagera, Pangani na Ruvu unaweza kukumbwa na tatizo kama vivuko na madara hayo hayataangaliwa kwa ukaribu.

Ametilia mfano meli ya Mv. Liemba inayosafarisha abiiria na mizigo kwenye ziwa Tanganyika wanaofanya safari kati ya Kigoma nchini Tanzania na Buurundi kwamba imepitwa na wakati na kuna haja ya Serikali kuona umuhimu wa kutafuta meli nyingine ili maisha ya wasafiri kwenye eneo hilo  yawe ya uhakika.

"Mimi naona kuna haja ya Serikali kujitathimini na  kujipanga upya kwa kuangalia vipaumbele na kuimarisha vikosi vyetu vya uokoaji ili kusaidia kazi za uokozi zitokeapo ajali." Alisema Bw. Mchenga.

Mwisho

No comments:

Post a Comment