Monday, October 4, 2010

WAGOMBEA WAKUTANISHA SERA

TARIME

Mgombea ubunge kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mwita Mwikwabe amesema kuwa kama atapata ridhaa ya wananchi wa jimbo la Tarime atahakikisha anaiboresha hospital ya wilaya ya hiyo kwani kwasasa hospital hiyo imekuwa ni sehemu ya kutafutia dawa na kupumzika kuliko mgonjwa kupata tiba.

Mwikwabe aliyasema hayo katika mdahalo wagombea wa nafasi ya ubunge wa vyama vitatu katika jimbo la Tarime mkoani mara  mdahalo ambao umeandaliwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Mara Development Forum mpango uliofadhiliwa na taasisi ya kijamii ya jijini Dar es Salaam ya The Foundation For Civil Society.

Katika mdahalo huo mgombe wa CHADEMA Mwita Mwikwabe alisema kuwa kama atapata nafasi hiyo katika kuwakilisha wananchi wa Tarime katika bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mbali na hospital hiyo atahakikisha usalama wa raia unakuwepo ili wananchi hao waweze kushirikiana katika kutafuta maendeleo ya jimbo hilo na kuondoa dhana nzima ya kuwa Tarime ni sehemu ya korofi.



Alisema kuwa shule za kata kwa sasa zimeleta ubaguzi kwa watanzania kwani wanaosoma katika shule hiyo ni vijana wa maskini huku hao wakiandaliwa kuwa vibaraka kwa watoto wa viongozi waliojilimbikizia mali.

Mwikwabe alisema kuwa endapo wananchi wa jimbo la Tarime watampatia ridhaa ya kuwawakilisha kwa kipindi cha miaka mitano atahakikisha katika uongozi wake jimbo hilo linakuwa na shule nne za kidato cha tano na sita ili kupunguza ubaguzi ambao upo kwa sasa kwani wanafunzi katika shule hizo watatoka sehemu mbalimbali Tanzania.

Katika upande wa kilimo Mwikwabe aliongeza kuwa Tarime ni sehemu ambayo inebarikiwa kuwa na rutuba nzuri,watu wa eneo hilo si wavivu na hali nzuri ya hewa hivyo atahakikisha serikali inatoa elimu kwa wahusika ili kuweza kuliam kilimo chenye tija.

Naye mgombea wa Chama cha United Democratic Party (UDP) Mchungaji Mwita Chacha alisema kuwa endapo atafanikiwa kupata nafasi hiyo atahakikisha kero kwa wananchi wa Tarime na wawekezaji inatoweka kwani ni aibu kwa wananchi wa eneo hilo kutonufaika na dhahabu ya eneo hilo.

Alisema kuwa atapambana kubadili sera ya madini ili iwanufaishe wanaTarime kwani kwa sasa serikali imewatenga watu wa Tarime kama vile si watanzania na kuwahimiza wananchi hao kuacha kilimo cha mkono kwani kimepitwa na wakati.

Kwa upande wa mgombea ubunge kupitia chama cha NCCR Mageuzi Peter Keba Wangwe alisema kuwa ili nchi iendele lazima iwe na viongozi bora wenye elimu ya kutosha.

Alisema kuwa kwa sasa kilimo cha mkono hakina tija hivyo katika nafasi yake ya ubunge atahakikisha kuwa wananchi wa Tarime wanakuwa na kilimo chenye tija ili kuongeza kipato kwa wananchi hao.

Wangwe ambaye ni ndugu yake na Marehemu Chacha Wangwe aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia CHADEMA alisema kuwa atahakikisha asilimia 25 ya mapato kutoka Sirari na Nyamongo yanasaidia wakazi wa jimbo hilo.

Katika mdahalo huo ambao umewakutanisha wagombea wa vyama vya siasa vya NCCR Mageuzi,United Democratic Party(UDP)  na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) huku mamia ya wafuasi wa vyama hivyo nao wakiwa wamejitokeza katika kuwaunga mkono wagombea wao na kusikiliza sera za wagombea wa vyama vingine na kuuliza maswali mbalimbali.

Mdahalo huo ambao uliongozwa na Sarah Mughwira ambaye ni mratibu wa asasi za kiraia Tanzania uliwakutanisha wagombea wa Peter Keba Wangwe(NCCR Mageuzi),Mchungaji Jacob Chacha(UDP) na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mwita Mwikwabe.

No comments:

Post a Comment