Elimu ya watu wazima ni elimu ambayo hutolewa kwa watu wenye umri
mkubwa, lengo la Elimu ya watu wazima ni pamoja ya kujifunza jambo
lolote lenye shabaha ya kumwendeleza mwanadamu ili aweze kuyamudu
mazingira yake.
Pamoja na hayo nia kubwa ya elimu hii ni kumwendeleza mtu ambaye hakubahatika kupata elimu ya Msingi.
Kwa Tanzania inaelezwa kuwa mkakati huu ulianza mara baada ya nchi
kupata uhuru Mwaka 1961 ambapo suala hili lilipewa kipaumbele lengo
likiwa ni kupambana na ujinga, Maradhi na Umaskini.
Taarifa zinaeleza kuwa mpango huu ulifanikiwa kwa asilimia kubwa
kupunguza idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika wakati wa Serikali
ya awamu ya Kwanza lakini kwasasa inaonekana idadi ya watu wasiojua
kusoma na kuandika imeongezeka kwa kasi.
Wakati wa Serikali ya awamu ya kwanza chini ya hayati Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere idadi ya walimu katika Shule za Msingi na Sekondari
ilitosheleza ambapo ilipelekea walimu hao kuweza kufundisha Elimu ya
watu wazima.
Kutokana na hali ngumu ya Uchumi kwa sasa na ongezeko la uandikishaji
wanafunzi wa Shule za Msingi kuwa mkubwa kumekuwepo na upungufu mkubwa
wa walimu na hivyo kushindwa kufundisha katika madarasa ya elimu ya watu
wazima na hivyo madarasa mengi ya elimu ya watu wazima kukosa
wawezeshaji.
Kaimu Afisa elimu ya watu wazima katika halmashauri ya manispaa ya
Musoma mkoani Mara Mwalimu Fibe Okelo alisema kwasasa elimu ya watu
wazima ni kama vile imepuuzwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Alisema mwaka 1964 katika mpango wa miaka 5, 10 hadi 20 msisitizo
ulikuwa elimu kwa wote na Mwaka 1970 Msisitizo wa elimu ya watu wazima
ulitangazwa na Mwalimu Nyerere kuwa suala la kuelimisha watu wazima
lilikuwa ni jukumu la kila Mtanzania aliyekuwa anajua kusoma na kuandika
tofauti na ilivyosasa.
"Nyakati za Mwalimu kulikuwa na msisitizo mkubwa sana katika suala la
elimu ya watu wazima jambo ambalo kila mtanzania aliliona kama linamhusu
tofauti na leo kila mtu na mambo yake" alisema Afisa huyo.
Mwalimu Okelo anaendelea kuelezea kuwa juhudi hizo wakati wa mwalimu
ziliweza kupunguza idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika kuwa
asilimia 6.7 Mwaka 1967 huku Mwaka 1980 idadi ya watu wasiojua kusoma na
kuandika ilianza kuongezeka kutokana na vita ya Kagera ambapo idadi
iliongezeka hadi kufikia asilimia 9.6 huku kwa sasa idadi hiyo ikiwa
imeongezeka hadi kufikia asilimia 31.
Kwa sasa hali ngumu ya Maisha na kiuchumi imeweza kuzalisha kundi
lingine la vijana la wasiojua kusoma na kuandika kutokana na kukosa
nafasi ya kuandikishwa darasa la kwanza.
Aidha afisa elimu huyo watu wazima alieleza kuwa kwasasa takwimu za
watu wasiojua kusoma na kuandika katika wilaya ya Butiama ni pamoja ana
ME 89,396 huku KE 103,501 huku idadi ya watu wasiojua kusoma,kuandika na
kuhesabu ikiwa ni asilimia 82 na idadi ya wanakisomo ikiwa ni 3,575.
Akielezea kuhusu sera ya elimu ya watu wazima,Mwalimu Okelo alisema
kuwa Sera ya Kisomo chenye Manufaa (KCM) haiwezi kufanikiwa kutokana na
viongozi kutotoa kipaumbele katika elimu hiyo bali kwa sasa limebaki
jina la kuwepo kwa elimu ya watu wazima (EWW).
Alisema kutokuwepo kwa bajeti ya kutosha katika kuendesha Madarasa na
idara hiyo ni tatizo katika mustakabali wa elimu hiyo kwani viongozi
wetu hawaoni kama kuna umuhimu katika elimu hiyo.
"Itakuwa kazi sana kufanikiwa katika Elimu ya watu wazima na hii ni
kutokana na viongozi kutotekeleza sera ya Elimu ya watu wazima,tunapanga
bajeti lakini bajeti hailetwi sasa hapo sisi tutafanya nini" alisema
Mwalimu Okelo.
Alisema EWW si mfumo rasmi kama ulivyo mfumo wa elimu wa Moja kwa moja
hapa kuna madarasa ambayo wahusika huzalisha na hiyo ndiyo tafsiri
sahihi ya EWW kuwa ni kisomo chenye Manufaa.
Mbali na kutokuwepo kwa bajeti lakini pia hakuna vitabu ambavyo
vinaendana na sera yenyewe katika kutoa elimu ya watu wazima.Madarasa
rasmi na hivyo kusababisha kutoa elimu hiyo katika mfumo usio sahihi.
Katika hatua nyingine imeonekana kuwepo kwa uzembe wa viongozi katika
kusimamia na kuhimiza sera ya elimu ya watu wazima kutekelezwa kutokana
na kutokuwepo kwa hamasa kwao,mfano katika wilaya Mwenyekiti wa
kuhamasisha elimu ya watu wazima ni Mkuu wa wilaya akisaidia na
Mkurugenzi lakini viongozi hao pamoja na kuwepo kwa jukumu kubwa katika
kufanikisha suala hilo hakuna msumo wowote wanaoutoa katika Jamii au
vikao vya Madiwani.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma Bw Musiranga Muhabi alisema
tatizo kubwa ambalo linasababisha kutofanikiwa katika utekelezaji wa
elimu ya watu wazima ni ukosefu wa Bajeti ambao umekuwa tatizo kubwa
katika halmashauri.
Alisema mara nyingi bajeti ya elimu ya watu wazima inaunganishwa katika
idara ya elimu hivyo fedha zinapokuja huunganishwa katika mfumo wa
elimu ulio rasmi kutokana na mahitaji yake hivyo nadhani ingekuwa bora
kama serikali ingetenga idara ya elimu ya watu wazima ambayo
inajitegemea.
"Kufanikiwa bado nji tatizo kutona na bajeti kuwa ndogo mimi nadhani
kama kweli tunataka kufanikiwa katika suala hili ni bora kitengo hiki
kingejitegemea ili kuleta ufanisi mkubwa" alisema kaimu Mkurugenzi huyo.
Baadhi ya watu waliosoma elimu ya watu wazima nyakati za serikali ya
awamu ya kwanza walisema kwa sasa elimu ya watu wazima ipo kwa sababu
isije kuonekana imekufa mikononi mwa watu lakini hakuna ambaye anajali
eneo hilo.
Mzee Nyanjofu Majaaliwa alisema kuwa kama sio kisomo hicho leo
hasingejua kusoma na kuandika lakini kulingana na sera nzuri iliyokuwepo
waliweza kufanikiwa hadi kufikia kufanya kazi kwenye Makampuni wakati
huo.
Naye Mwalimu Mstaafu Juma Nyasoro ambaye aliwahi kufundisha madarasa ya
Elimu ya watu wazima alisema kuwa wakati wa Serikali ya awamu ya kwanza
hayati walimu Nyerere aligundua watanzania hawajui kusoma wala kuandika
hivyo hatua za haraka zilihitajika.
Alisema kuwa hata walimu waliokuwa wanajitolea kufundisha Madarasa hayo
walikuwa na moyo tofauti na leo walimu wengi wametanguliza Masilahi
mbele bila kuangalia athari ambazo jamii inazipata.
"Sisi tulikuwa na moyo wa kujitolea katika kuhakikisha watanzania
wanaondokana na tatizo la kutojua kusoma na kuandika tofauti na leo kila
mwali mu anatnguliza pesa kwanza" alisema Mwalim huyo Mstaafu.
Katika hatua hiyo Mwalimu huyo Mstaafu alisema kuwa bila kuwepo na
msukumo kutoka idara huska elimu ya watu wazima itabaki jina huku
akieleza kuwa hajui kama madarasa hayo bado yapo.
Nao baadhi ya wananchi mbalimbali walipata nafasi ya kuhojiwa na
mwandishi wa Makala hii walisema kuwa itakuwa kazi kukuza eneo hilo
kutokana na Serikali kutoiona kama ina manufaa katika jamii,mmoja wa
mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la Ally Ramadhani Mkazi wa manispaa
ya Musoma alisema kuwa si rahisi kufanikiwa katika eneo hilo kwasasa
kutokana na hali ya uchumi ilivyo lakini viongozi kutotoa msukumo katika
elimu hiyo.
Alisema kuwa Mamlaka huska zinapaswa kuweka bajeti ambazo zitasaidia
katika kukuza na kuendeleza elimu ya watu wazima ili kionekana kuwa na
Manufaa tofauti na sasa ambapo idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika
inaongezeka na hasa kundi la vijana.
source: http://www.jambotanzania.com
No comments:
Post a Comment