Pichani ni baadhi ya majengo ya Shule ya Msingi Rongai, wilayani Rombo. Shule hii ni miongoni mwa maeneo yanayoathiriwa na uvamizi wa tembo waharibifu ambao huathiri taaluma shuleni hapo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Judethadeus Mboya akizungumza na mtandao wa www.thehabari.com hivi karibuni wilayani Rombo.
Na Thehabari.com, Rombo
HALMASHAURI
ya Wilaya ya Rombo imeanza mipango ya kutumia ufugaji wa nyuki
kukabiliana na tembo waharibifu ambao mara kadhaa huvamia baadhi ya
makazi ya wananchi maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo na kufanya uharibifu
wa mazao pamoja na kuua au kujeruhi wakazi.
Akizungumza na
mwandishi wa habari hizi hivi karibuni wilayani hapa, Mkurugenzi
Mtendaji wa halmashauri hiyo, Judethadeus Mboya alisema tayari
halmashauri hiyo imetengeneza mizinga ya nyuki ambayo imesambazwa maeneo
kadhaa ili kukabiliana na tembo waharibifu eneo hilo.
"Unajua
nimetembea mbuga mbili za Kenya ikiwemo Tsavo ambazo tumepakana nazo
eneo hili sehemu ambayo tembo hutokea huko na kuvamia maeneo yetu,
sehemu hizi wao wamedhibiti uvamizi wa tembo...wamefuga nyuki wengi sana
na maeneo mengine wametumia hadi teknolojia kuwazuia tembo kuvamia
makazi ya raia hivyo hawapati madhara kama yetu," alisema Mboya akifanya
mazungumzo na gazeti hili ofisini.
Alisema
kwa sasa tayari wametengeneza mizinga 50 ya nyuki na kuifunga ukanda wa
chini wa vijiji kama Chala, Ibukoni, Ngoyoni na maeneo mengine ambayo
tembo huyatumia kama njia kipindi cha uvamizi na kwa sasa mizinga
mingine 100 ya nyuki inaandaliwa kuenezwa maeneo mengine kukabiliana na
tembo hao hatari.
Alisema
viongozi wa halmashauri hiyo pia wametoa elimu kwa wanakijiji maeneo
husika ya kuhamasisha uvugaji nyuki katika vikundi ikiwa ni jitihada za
kukabiliana na tembo hao waharibifu ambao idadi kubwa hutokea nchi
jirani ya Kenya na kufanya uharibifu pamoja na kutishia maisha ya
wanavijiji upande wa Tanzania.
Aidha
kiongozi huyo alisema tembo hao mbali na kufanya uhalibifu mkubwa wa
mazao ya wanavijijini kipindi cha uvamizi wakati mwingine wamekuwa
wakiuwa raia jambo ambalo ni hatari zaidi kiusalama.
Uchunguzi uliofanywa
na mwandishi umebaini uvamizi wa wanyama hao umekuwa kero kwa maeneo
mbalimbali ya vijiji vya wilaya hiyo, kiasi ambacho unatishia shughuli
za maendeleo ya wananchi kama kilimo pamoja na maendeleo ya elimu kwa
ujumla.
Akizungumzia
hali ya uvamizi wa tembo na athari za elimu, Mwalimu wa Taaluma Shule
ya Sekondari Tanya, Shuma Himidiel alisema miezi ambayo tembo huanza
kufanya uvamizi huingilia ratiba za masomo na mara kadhaa kusimama
kutokana na hofu ya wanafunzi na usalama wao hasa wanapotoka na kuja
shuleni.
"Kimsingi
wanyama hawa wanapoanza usumbufu kijiji kizima huwa na heka heka na
wakati mwingine hata wanafunzi wanashindwa kuja shule kuhofia maisha
yao...hata wazazi huwazuia watoto wao kutoka hadi hali ya hatari
inaporejea kuwa ya kawaida.
Akifafanua
zaidi mwalimu Himidiel alisema mara ya mwisho tembo kufanya uvamizi
katika Kijiji cha Tanya waliua mtu mmoja walipokuwa wakidhibitiwa na
askari wa wanyamapori eneo hilo.
No comments:
Post a Comment