Watetezi kutoka mikoani ambao ni wanachama wa Mtandao wa
Watetezi wa Haki za Binadamu Nchini (THRD-Coalition), waliokutana kwa siku tatu
jijini Dar es Salaam, pamoja na kupata mafunzo adhimu ya usalama kwa watetezi yatolewayo na
THRD-Coalition, pia walifanya tathmini ya hali ya usalama kwa watetezi nchini; asasi za haki za binadamu, waandishi wa habari
na watu wanaojitolea katika eneo la msaada wa kutetea wenzao yaani
(volunteers). Tathmini imeonyesha kwamba yapo mambo kadhaa yanayosababisha
kukosekana kwa usalama kwa watetezi nchini na kupotea kwa amani.
1. Utendaji wa Vyomba Serikali na Vuguvugu la Kisiasa
Serikali ndicho chombo chenye jukumu la kuwalinda watetezi wa
haki za binadamu na watu wengine waliomo ndani ya mipaka ya nchi yetu, wao na
mali zao. Vitendo vya watu kujichukulia sheria mikononi mwao, kuteka, kutesa,
kung’oa meno, na macho, kukata vidole na hata kuwarushia bomu waamini wakiwa
katika maeneo ya maombi ni ishara ya dhahiri ya serikali iliyoshindwa kutimiza
majukumu yake. Vitendo vya baadhi ya viongozi nchini hasa katika ngazi za
Serikali za Mitaa kuwakandamiza watetezi wa haki za binadamu kwa namna
mbalimbali ikiwemo kuwafungulia kesi za kubambikiza vimefikia kiwango cha
kutovumilika. Matamko mengi yanayotolewa na viongozi wa juu wakiwamo mawaziri
dhidi ya watetezi na asasi za haki za binadamu nchini yanaonyesha kuwa ni
viashiria vya vitisho vya kiusalama wazi wazi kwa watetezi nchini. Pia watetezi
wamekuwa wakishutumiwa kuwa ni wapinzani kwa sababu kazi zao zimekuwa
zikilinganishwa na kazi za vyama vya upinzani na za kiuchochezi.
Kuwa mtetezi ni kiungo
muhimu katika kuibua na kufichua maovu ili kujenga utawala unaoheshimu haki za
binadamu, lakini siku zote tumejikuta tukihatarisha maisha yetu. Katika
mazingira ya aina hiyo watetezi hawawezi kujiweka katika kundi salama hata
kidogo, bali kwamba usalama wao umo hatarini kwa sababu kazi nyingi
wanazozifanya huwalazimisha kuikosoa serikali pale inapokuwa haitimizi wajibu
wake kuhusiana na kulinda haki za msingi za binadamu na haki nyinginezo stahiki.
Mifano halisi ya migongano kati ya asasi
na serikali ni kesi za kugombea ardhi Pugu, Loliondo, Bagamoyo na migogoro
isiyoisha katika migodi mkoani Mara.
2. Wamiliki wa vyombo vya habari
Katika
kudadisi ni kwa nini wanahabari wanakabiliwa na changamoto nyingi za kiusalama
iligundulika kwamba wamiliki wa vyombo hawana mikakati mizuri juu ya suala zima
la usalama kwa waandishi wao. Pia malipo finyu kwa wanahabari ilionekana kuchangia kwa kiasi kikubwa kwa sababu baadhi
yao hawapati malipo ya uhakika wala mikataba. Hali hiyo husababisha waandishi
waishi maisha ya kubahatisha na wakati mwingine hujikuta wakishawishika kuingia
katika makundi ya kisiasa ili kuanza
kuvitumikia ‘vyanzo vyao’ jambo ambalo husababisha wakiuke maadili ya kazi zao
na mwisho hushambuliwa na wale wanaoguswa na habari za aina hiyo. Aidha
watetezi wanawasihi wamiliki kuanza kuweka mikakati ya kiusalama kwa waandishi
na kuboresha mishahara kwa waandishi ili wafanye kazi kwa uhakika zaidi.
3. Jeshi la Polisi
Jeshi la
Polisi wawe makini na matumizi ya silaha za moto na nguvu za ziada ambazo
zimekuwa zikisababisha vifo na ulemavu wa kudumu. Katika purukashani nyingi za
kisiasa jeshi hilo limeshindwa kabisa kuonyesha kwamba linafanya kazi ya
kuutumia umma wa Watanzania wote na badala yake limekuwa likichukua mwelekeo wa
kuwatumikia wanasiasa au chama fulani. Aidha askari polisi wanakumbushwa kwamba wao ni sehemu ya jamii
na hao wanaowatesa ni ndugu zao wa karibu wadogo zao mama zao n.k. Jeshi la
Polisi litambue kuwa kazi za watetezi wa haki za binadamu ni kazi halali
zinazolindwa kisheria na wanajukumu la kuweka mazingira mazuri ya watetezi
kufanya kazi zao bila kutekwa, kuteswa ama kungo’lewa macho, meno, kucha n.k. Mfano halisi wa mapungufu ya
jeshi hilo ni kukamatwa kwa askari hivi karibuni waliokuwa na fuvu la kichwa
cha mtu mkoani Morogoro kwa lengo la kumbambika mtu kesi ya jinai. Tunaisihi
Serikali na Jeshi la Polisi kuanza kutekeleza Tamko la Umoja wa Mataifa la
tarehe 15 Machi 2013 linalotaka mataifa yote kutambua umuhimu na uhalali wa
majukumu ya watetezi wa haki za binadamu katika kutetea haki za binadamu
demokrasia, utawala wa sheria, kama nyenzo la kuhakikisha usalama wao ikiwa ni
pamoja na kuheshimu uhuru wa asasi zao na kuepuka kunyanyapaa shughuli za asasi
za kiraia.
4. Wanaharakati na Watetezi wa Haki za Binadamu
Wanaharakati
wote na watetezi wa haki za binadamu wasichukue upande wowote katika masuala ya
itikadi za kisiasa kwani wao ni watu wa kati. Pia wanaharakati wasijiingize
katika matumizi ya nguvu au kupambana na Jeshi la Polisi. Aidha wanaharakati
wametakiwa kuwa waelimishaji wa umma na kujizuia kujiingiza katika mambo
yaliyopandikizwa na watu wasioitakia mema nchi yetu kama vile udini na migogoro
isiyoisha ya kugombea ardhi, maeneo ya malisho, ukabila n.k.
5. Vurugu za Udini
Kwa miaka
mingi Tanzania haikuwahi kupata misukosuko ya udini kama inayotokea sasa.
Lakini kwa miaka ya hivi karibuni uhasama wa kidini umezidi kushamiri. Watetezi
kwa umoja wetu tunaamini Tanzania hatuna udini bali kinachoendelea ni ajenda za
watu fulani kwa maslahi binafsi ama ya kifedha, kidini au kisiasa. Kwa sasa
nchi inaweza kutumbukia katika machafuko ya kidini endapo viongozi wa dini
zote, wanasiasa na serikali hawatachukua hatua za makusudi kuwakomesha wachache
hao ambao wanataka kuondoa amani ya nchi. Katika mazingira haya pia mtetezi wa
haki za binadamu hawezi kubakia salama
na ndio maana tunakemea kwa nguvu zote vitendo hivi viovu.
6. Watanzania Wote Kwa Ujumla
Watanzania katika ujumla wao wameaswa kuwa makini hususani wakati huu tunapoelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Wapo watu wanaochomekea ajenda zao kwa malengo wanaoyafahamu wao wenyewe na hivyo kuligawa taifa katika misingi ya udini na mambo mengine kama hayo yasiyo na tija wala manufaa kwa nchi yetu. Aidha Watanzania wameshauriwa kuirejea kazi nzuri ya kuwaunganisha ambayo iliifanya nchi hii ifahamike kama kisiwa cha amani miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa.
Mwisho
tunaungana na watanzania wengine kulaani kitendo cha kutupa mabomu katika
mikusanyiko ya watu kama ilivyotekea kule Arusha. Tunawapa pole wafiwa na majeruhi
wote. Na kutaka watanzania wote bila kujadili itikadi zao kuendelea kulaani
vitendo hivi vya kinyama.
TAMKO HILI LIMEANDALIWA NA WATETEZI 30 WA HAKI ZA BINADAMU TOKA MIKOA MBALIMBALI
KWA NIABA YA WENZAO KATIKA AZIMIO LA KUIREJESHA NCHI HII KATIKA HALI YA AMANI
NA UTULIVU
No comments:
Post a Comment