Tuesday, May 7, 2013

LEMA ANENA

Serikali huwezi kutibu Malaria kwa kumpa Mgonjwa Panadol” - G. Lema

Nimefuatilia leo asubuhi juu ya maneno niliyotamka Olasiti Kanisani baada ya bomu , nimeona michango mbali mbali katika mitandao ya jamii , nawapongeza wale wenye kutambua ukweli na kuutetea ukweli lakini pia wale wasiojua ukweli lakini wamefanikiwa kupata maarifa ya kujua matumizi ya kompyuta kwa hiyo nakusikia fahari kuandika maoni yeyote wanayotaka , Watu hawa ni muhimu kwani wanasaidia kutambua kwa wepesi kuwa sio kila mtu anayeweza kutumia Internet ni mwenye uelewa na akili , hivyo inasaidia Wazazi kujua namna ya kusaidia watoto wao katika siku zijazo.

Maneno niliyotamka ni muhimu sana , NUKUU , “ Nawapa pole wote mliofikwa na majanga haya , Mimi nichukue fursa hii kuwapa pole , lakini niwe jasiri sana kusema ukweli kama ninyi waandishi wa habari hamtafanya editing…..

“ Kwanza kabisa niweke wazi kuwa jambo hili limesababishwa na chokochoko za udini ambazo muasisi wake ni Serikali ya CCM na viongozi wake, aliyepiga bomu hapa leo siyo jambazi wa kutaka mali bali ni mtu aliyeelewa na kufundishwa tofauti kwa nia mbaya kuhusu dini nyingine, haya maneno ya udini yalianzishwa na viongozi wa Chama tawala lengo likiwa ni kuwagawa na kuwatawala raia lakini kwa sasa wamelikoroga, wamewachonganisha watu wa dini mbalimbali hasa Waislam na wakristo ambao ndio wengi katika taifa hili bila kujua madhara ya mkakati huu kuwa utaligawa Taifa.
Sasa basi kazi hiyo waliyoifanya haya ndio mavuno yake kwani tukio hili lina sura zote za kiimani na kigaidi na nilitake jeshi la polisi kufanya kazi ya kuwakamata haraka kama ambavyo walinikamata mimi nyumbani kwangu kwa mabomu na vitisho , nawapa pole sana watu wote mliopatwa na janga hili .

Niliposema maneno haya ni maneno ya msingi kwa wakati muhimu , watu wameumizwa na wengine wamekufa na sababu ni uchochezi ulionza muda mrefu kufanywa na Chama tawala Wakati siasa ya udini na ukabila na Ukanda zinafanywa iliwafurahisha watawala kwani lengo lao la Wagawe na watawale lilifanikiwa bila kujua matokeo yake ni mabaya kiasi gani . Tukio la Jana Olasiti Arusha sio la kijambazi ni mgongano wa imani ambao watawala wanataka kuuzima kwa propaganda badala ya kujadili ukweli wa hali halisi ili kutibu jeraha hili baya ambalo halita muacha Mtu yeyote salama .

Kuna mambo mengi yanaendelea katika jambo hili linalohusu udini katika Taifa letu na ushauri wangu kwa Serikali ni kwamba hawawezi kutibu Malaria kwa kumeza panadol kuogopa kusema ukweli sio uzalendo bali ni ujinga , tena ujinga mkubwa sana , Malcom X alisema “ Huwezi kuwa mzalendo kiwango cha kupuuza ukweli na kujifanya hauoni , Leo hii ndivyo watu wanavyotaka kufanya katika jambo gumu kama hili , swali muhimu sana ,ni nani kati ya Mkristo au Mwislamu atakayekwenda kusali kwa amani kama vitendo hivi visipo kemewa kwa ukweli na kuweka bayana mzizi wa jambo hili la uvunjifu wa amani ambalo tiyari kuna Sheikh alimwagiwa tindikali kule Zanzibar na matukio mengi kama haya ambayo yamewapata Mapadri na Wachungaji , hivi kweli katika Taifa hili tunafika mahali tutaanza kuingia katika Nyumba za Ibada kwa kufanyiwa upekuzi kama tunasafiri kwenda Marekani? kwani inavyoonekana huko ndiko tunakoelekea, ieleweke kwamba jambo hili litakwenda kupunguza idadi ya watu kwenda kuabudu na mwisho wahalifu wataongezeka kwani kazi ya Msikiti na Kanisa ni kufundisha watu nia njema dhidi ya uovu ambao ni chukizo kwa Mungu ambapo mafunzo haya hayapatikani kwingine kokote kirahisi isipokuwa huko ni vyema watu wakajifunza kusema ukweli kwani hakuna namna unaweza kupata uhuru kamili bila kuwa mkweli .

Wachungaji na Maaskofu wanajua pale Chama Tawala kiliposema CUF ni chama cha Udini tena Waislamu na Watu wote wanaona na kusikia pale Chama Tawala kinaposema kuwa Chadema ni Chama cha Wakristo , limeonekana ni jambo la kawaida sana bila kutafakari madhara yake na sasa haya ni madhara makubwa ya siasa yenye lengo la “ Wagawe halafu watawale “

Ni Jambo la kusikitisha kama mgogoro huu wa Udini utashindwa kujadiliwa kwa makini na badala yake kutafuta propaganda za kuzima jambo hili , mtaweza kufanikiwa kwani nyie ni Serikali na mnazo njia nyingi za propaganda lakini ukiona unafanikiwa kufanya jambo baya bila kuyumba basi tambua mwisho wake ni mbaya na mkubwa sana , Hekima sio kukwepa ukweli , hekima ni kujadili ukweli , hekima sio kuita viongozi wadini Ikulu, hekima ni kuacha Siasa chafu kwa vitendo na kutubu dhambi kubwa ya kuwagawa Watanzania ambayo mmekwishaifanya .

Niliposema CCM na Rais Kikwete ndio kinara wa Udini mlinibeza bila hata kuona ushaidi wangu na hata mimi nilishangaa sana huo ujasiri wa kunibeza mliupata wapi bila hata kujua ni kitu gani ninacho kama ushahidi , sio kazi nyepesi kumtuhumu Rais kwa kiwango hicho na wala sio jambo jepesi pia kusema maneno hayo , kwani Rais ndio mwenye mamlaka ya vyombo vyote vya usalama katika Taifa letu , ni hatari kubwa ambayo inaweza kufupisha maisha yangu lakini tunajipa moyo tukijua kuwa hakuna Mtu hatakayeishi milele , familia zetu zinaishi kwa mashaka lakini tunavumilia matusi , mateso , udhalilishwaji , kebehi na vitisho kwa ajili ya siku zijazo za Nchi yetu na watoto wetu .

Kuna tatizo kubwa Tanzania linahitaji hekima na ujasiri na propaganda za CCM hazitaweza kutibu tatizo hili isipokuwa unyenyekevu wa hali ya juu na kukubali kuwa lipo tatizo na chuki zinaendelea kusambaa siku hadi siku na kama mtapuuza iko siku mtasema tuliambiwa na haya maandishi yangu sio ya mara ya kwanza kuandika kuhusu Udini , naogopa sana kuishi kwenye nchi ambayo watu wataheshimiana kwa dini na kabila zao na sio utu wao na ubinadamu .

Miaka ya nyuma tuliishi vizuri sana tu na Chama tawala mlipoona mnatoka madarakani mlitumia propaganda za Udini na Ukabila , lakini pia baadhi ya viongozi wa Dini wamekuwa wakitumika vibaya pale wanapofikiri na kujua kuwa Wanasiasa wanaweza kuchangia vyema katika mambo mbali mbali ya maendeleo ya taasisi za Kidini hapo ndipo mnapotoa mwanya wa Wanasiasa kufanya siasa za udini , hivi kweli nini kinawapa ujasiri baadhi ya Viongozi wa dini kuamini kuwa Wanasiasa wanaoishi kwa mshahara wanaweza kuwa matajiri wakubwa wanaochangia mamilioni ya fedha. Hili nalo ni tatizo , Viongozi wa kisiasa kuzunguka kwenye nyumba za Ibada kila kukicha ili kutafuta thamani ya kuungwa mkono katika matarajio yao , ili Viongozi wadini wawe na mamlaka ya kuisadia Serikali wajue kwamba wanahitaji kutambua mamlaka waliyonayo katika shughuli zao lakini Mbunge au Waziri au Kiongozi yeyote wa Kisiasa anapokuwa na heshima kuliko Viongozi wa Dini ni dhahiri kuwa Mamalaka yao imepotea nalo hili ni tatizo kubwa sana kwani kazi kubwa ya Viongozi wa dini ni kusimamia haki , kukemea maovu na kukosoa na vile vile kusaidia Viongozi wa Serikali kutenda kweli na sio kugeuza Nyumba za ibada kuwa maficho ya Viongozi waovu .

Mwanafalsafa maarufu wa Kiyahudi Elie Wiesel alisema, “there may be times when we are powerless to prevent injustice, but there must never be a time when we fail to protest.” Kwa Kiswahili, “kuna nyakati tunaweza kuwa wadhaifu katika kuzuia uovu na dhuluma, lakini kamwe isijetokea wakati ambapo tutashindwa kupinga uovu na dhuluma.”

Lakini pia , Frederick Douglass zaidi ya miaka mia moja na hamsini iliyopita alisema “he is a lover of his country who rebukes rather justify its sins”, yaani, “mpenzi wa nchi ni yule anayekemea madhambi yake badala ya kuyahalalisha”!
Nawapongeza pia Wananchi wote waliokubali kujitolea Damu baada ya Mimi na Mbunge mwenzangu kuhamasisha jambo hilo ambalo limebeba utu mwingi , asanteni sana na Mungu awabariki sana na wale ambao hamkutoa Damu kwa sababu vifaa viliisha tafadhali naomba sana siku ya Jumatano mkajitolee damu katika uwanja wa Abeid Karume .
“ Dhambi kubwa na mbaya kuliko zote Duniani ni Uoga “

GODBLESS J LEMA (MP)

No comments:

Post a Comment