Thursday, August 9, 2012


             DC  AFUNGUA MAFUNZO YA SENSA MUSOMA


Pendo Mwakyembe

MUSOMA

Washiriki wa mafunzo ya sensa ya watu na makazi Waagizwa kufuatilia na kusikiliza kwa makini mafunzo watakayopewa na wawezeshaji wa zoezi hilo ili kuleta ufanisi katika zoezi hilo.


 Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya ya Musoma Bwana Jackson Msome wakati akifungua semina ya sensa na
 makazi katika ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mara.

                                      Mkuu wa wilaya ya Musoma,Bw Jackson Msome 

Bwana Jackson amesema kuwa mafunzo hayo yatawawezesha washiriki kupata mbinu za kuuliza maswali, namna ya kudodosa taarifa mbalimbali za kaya na kujua kutambua namna ya kuhifadhi siri na taarifa za kaya ambazo wamezipata.

Amesema kamati imewaamini kufanya kazi hiyo hivyo washiriki wanaombwa watambue dhamana kubwa waliyopewa na serikali hivyo ufanisi na uhodari wao katika kazi utapimwa kwa mafanikio ya sensa iyo itakayoanza tarehe 26, mwezi wa nane 2012.

Aidha ameongeza kuwa serikali inapenda kuona sensa hiyo ikipata mafanikio makubwa hivyo semina hiyo inalenga kuwajengea uwezo mkubwa na ufanisi ili kila wilaya ifanikishe zoezi hilo kwa ufanisi zaidi kwa maslahi ya taifa kwa ujumla.

Wakati huohuo mkuu huyo wa wilaya ameviomba vyombo vya habari kutoa ushirikiano mkubwa katika kuelimisha wananchi kuhusiana na sensa ya watu na makazi.

Amesema vyombo vya habari vina nguvu na mchango mkubwa katika kutoa elimu ya uhamasishaji hivyo ni vema kama vyombo hivyo vitatumia nafasi hiyo kuhamasisha  wananchi ili watoe ushirikano wa  kutosha katika zoezi hilo.

Mafunzo hayo ya sensa ya watu na makazi yamefunguliwa rasmi hii leo katika wilaya ya Musoma  na yatadumu kwa siku kumi na moja. Zoezi la kuhesabu watu na makazi litaanza mwezi huu tarehe ishirini na sita.



No comments:

Post a Comment