WAKILI MARANDO ASEMA NI SHAHIDI MUHIMU,WATAMLETA KUTOA USHAHIDI WA MANENO
Tausi Ally
RAIS Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, anatarajiwa
kupanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mei 8, mwaka
huu kumtetea aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa
Mahalu.Wakili anayemtetea Balozi Mahalu, Mabere Marando alisema jana
kwamba Mkapa atapanda kizimbani siku moja baada ya Profesa Mahalu
kumaliza kutoa utetezi wake.
Awali, akizungumza mbele ya Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ilvin Mgeta Wakili Marando alisema Mei
8, kutakuwa na shahidi mwingine wa mwisho muhimu ambaye hata hivyo,
hakumtaja.
Alipoulizwa kuhusu shahidi huyo nje ya Mahakama, Marando
alimtaja kuwa ni Rais Mstaafu Mkapa na baadaye alipopigiwa simu kutoa
ufafanuzi zaidi alisema: “Mkapa ni shahidi wa Mahalu hivyo atafika
mahakamani kutoa ushahidi wake kwa maneno.”
Alipoulizwa kwamba
atatoa ushahidi gani mwingine mbali ya ule alioutoa kwa maandishi
alisema: “Safari hii atafika mahakamani kutoa kile anachokifahamu kwa
maneno.”
Kuhusu kama kiongozi huyo mstaafu wa taifa amekubali
kufika mahakamani, Marando alisema: “Kwani kuna nini? Yeye ni shahidi wa
Mahalu. Si kuja kutoa ushahidi tu!”
Profesa Mahalu na aliyekuwa
Ofisa Utawala wa ubalozi huo, Grace Martin wanakabiliwa na shtaka la
uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2,065,827.60.
Akihojiwa
na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Ponziano Lukos dhidi ya mashtaka hayo
yanayomkabili, Profesa Mahalu alidai kuwa Serikali ilitengua ubalozi
wake Februari, 2006 bila ya kupeleka barua ya uamuzi huo kwa Serikali
ya Italia ambayo iliendelea kumtambua kama balozi na kumpa heshima zote
ikiwamo kualikwa kwenye hafla mbalimbali, kuagwa na kupewa tuzo
mbalimbali.
Balozi Mahalu alidai kuwa mwishoni mwa Aprili, 2006
alirejea nchini na Agosti mwaka huohuo aliitwa kwenye Ubalozi wa Italia
na kupewa tuzo.
Akihojiwa kuhusu mikataba miwili iliyotumika
kununua jengo la Ubalozi wa Tanzania nchini Italia alidai kuwa
kulikuwepo na mikataba miwili ya ununuzi wa jengo hilo ambayo yote
aliiwasilisha serikalini.
Alidai kuwa aliiarifu Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwamba wanategemea kununua jengo kwa
mikataba miwili na aliinunua nyumba hiyo kwa faida ya Serikali na yeye
hakupata kitu chochote.
Kuhusu madai kwamba aliingia mikataba
miwili kwa ajili ya kununua jengo hilo bila ya kuwepo mtu mwingine wa
kushuhudia, Balozi Mahali alidai kuwa yeye alikuwa mwakilishi wa
Tanzania nchini Italia na alipata maelekezo ya kununua jengo hilo baada
ya Wizara ya Ujenzi kujiridhisha kutokana na tathmini waliyokuwa
wameifanya.
“Hakukuwa na mtu mwingine aliyeshuhudia lakini,
nilipata mamlaka kisheria ya kufanya hivyo kutoka kwa aliyekuwa Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Jakaya Kikwete,” alidai.
Alidai
kuwa suala la kununua jengo la ofisi ya ubalozi kwa kutumia mikataba
miwili, Kikwete ambaye sasa ni Rais wa Tanzania, alikuwa akilifahamu na
hata alipotembelea Italia hilo lilikuwa jambo la kwanza kutaka
kulifahamu kutoka kwa aliyekuwa akiliuza.
“Rais Kikwete akiwa
Waziri, alitembelea Italia na suala la mikataba miwili lilikuwa jambo la
kwanza alilouliza kutaka ufafanuzi. Wakati tunafanya mazungumzo
alimwuliza, muuzaji na alimjibu kwamba ndiyo utaratibu wa Italia
wanapouza jengo kwa nchi kwa gharama ya chini huingia mikataba miwili,
mmoja wa kiofisi na mwingine wa kibiashara,” alidai na kuongeza kuwa
baada ya Kikwete kupata ufafanuzi huo alicheka.
Profesa Mahalu alidai kwa sifa alizokuwa nazo na kwa ucha Mungu wake, hawezi kutenda makosa yanayomkabili mahakamani.
Februari
29, mwaka huu Profesa Mahalu akijitetea, alidai kuwa Kikwete akiwa
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alimpa nguvu ya
kisheria ya uwakilishi wa ununuzi wa jengo hilo.
Akiongozwa na
Wakili Marando kutoa utetezi huo, Profesa Mahalu alidai kuwa Septemba
2001, alipewa Nguvu ya Kisheria ya Uwakilishi (Special Power of
Attorney) ya ununuzi wa jengo hilo Kikwete.
“Aliniagiza kununua
jengo hilo la ubalozi. Machi 24, 2004 nilimwandikia barua Rais Kikwete
na kwenye barua hiyo niliambatanisha nyaraka za ununuzi wa jengo hilo
baada ya kulinunua.”
Alidai kuwa pia alipeleka barua hiyo kwa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Naibu
Waziri wa wizara hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Mhasibu Mkuu wa
Serikali, Waziri wa Ujenzi, pamoja na Waziri wa Fedha.
Alidai
kuwa baada ya kuandika barua hiyo na kuiambatanisha na nyaraka hizo za
ununuzi wa jengo hilo, hakuwahi kuhojiwa juu ya ununuzi huo.
Alisema
ushahidi uliotolewa na shahidi wa tatu wa upande wa mashtaka, Steward
Migwano Aprili 23, 2008 pamoja na vielelezo vya ushahidi kuhusu ununuzi
wa jengo hilo unalingana na wa kwake.
Lakini akasema ushahidi wa
shahidi wa tano wa upande wa mashtaka, Isdory Kyando kuhusu gharama za
bei ya ununuzi wa jengo hilo unatofautiana na wa kwake kwenye bei rasmi
na kwamba kulikuwepo na mikataba miwili ambayo Serikali iliiridhia.
Alidai kuwa mikataba yote ipo mikononi mwa Serikali kwa muda mrefu.
Profesa
Mahalu alisema pia kwamba Agosti 3, 2004 katika majadiliano ya Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika Mkutano wa 16, kikao cha 39,
Rais Kikwete akiwa Waziri wa Mambo ya Nje alitoa hotuba iliyoonyesha
kuwa ununuzi wa jengo hilo ulifuata taratibu zote za kisheria na kwa
makubaliano ya Euro 3 milioni.
Alidai kuwa kauli yake na ya Rais
Kikwete juu ya ununuzi wa jengo hilo bei zinalinga na kwamba hakuwahi
kupata malalamiko yoyote wala kuhojiwa juu ya uhalali wa matumizi hayo
ya fedha.
Pia alidai kuwa hakuwahi kuona upande wa mashtaka ukipeleka
kesi mahakamani hapo kama mama mwenye jengo hilo la ubalozi alikuwa
amelipwa fedha pungufu ya bei iliyokubaliwa na kwamba katika mgogoro
huo pia hakuwahi kuona mama huyo akipeleka malalamiko kuwa hakuwahi
kulipwa.
Source Mwananchi
No comments:
Post a Comment