Saturday, May 12, 2012

SIKU YA FAMILIA DUNIA MEI 15,2012

Siku ya Familia Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 15 Mei na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.  Maadhimisho hayo yanatokana na tamko la Baraza la Umoja wa Mataifa Na. 47/257 la tarehe 20 Septemba, 1993, linaloidhinisha kuwa na Siku maalum kwa ajili ya familia. Tanzania ni moja ya wanachama wa Umoja wa Mataifa hivyo huungana na nchi nyingine kila mwaka kuadhimisha siku hii. Mwaka huu maadhimisho haya yatafanyika kimkoa.


Madhumuni ya Siku ya Familia Duniani ni kuhamasisha, kuhimiza, kuelimisha na kutanabahisha jamii kuhusu umuhimu wa familia katika jamii kwa nia ya kuchukua hatua zinazopasa ili kuziimarisha na kuziendeleza. 


Kauli mbiu ya Siku ya Familia mwaka huu ni: “UWAJIBIKAJI SAWA KATIKA MAJUKUMU: MSINGI WA FAMILIA BORA”. Kauli mbiu hii inalenga kuhamasisha, kuhimiza, kuelimisha familia na jamii kugawa muda wa kazi za kiuchumi na kuacha muda wa kutosha kutekeleza majukumu ya familia, hasa ya kulea na kukaa na watoto/familia hivyo kujenga umoja, uadilifu na upendo kwa familia. Ushindani uliopo katika soko huria ni changamoto kwa wazazi wa kizazi cha sasa  kutopata muda wa kutosha kuwa na familia.  Aidha, majukumu yanaongezeka siku hadi siku ambayo husababisha wazazi/walezi kufanya kazi siku zote za wiki na hata usiku, hatimaye kupunguza muda wa kukaa na familia hasa watoto wao na hivyo kusababisha kutokuwepo kwa uwiano wa kazi na majukumu ya malezi.

No comments:

Post a Comment