Musoma.
Vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mikononi vinaonekana kushamiri katika wilaya ya Musoma mkoani Mara.
hatua hiyo imeonekana kufuatia hatua ya wakazi wa kijiji cha Mwibagi kata ya Kyanyari wilayani humo kuwachomea nyumba wenzao wawili wakiwatuhumu kujihusisha na vitendo vya ushirikina huku wengine watatu wakiishi kama wakimbizi baada ya kudaiwa kuwa wahalifu sugu wanaosakwa ili wauwawe.
Waliochomewa nyumba zao wakituhumiwa kuwa ni wachawi ni Nyamhanga Mhiri na mama yake Mtongori Mhiri waliochomewa nyumba tano pamoja na kuchukuliwa mabati 48 mpya;simu moja ya mkononi huku wakiteketezewa mbuzi 28;ng’ombe 7 na kondoo 18 na kuharibiwa kabisa vyombo vyao vya ndani vikiwamo magodoro;samani mbalimbali na Tv.
Aidha wanaoishi kama wakimbizi wakilazmika kuziacha familia zao kwa kuhofia kuuwawa kwa vile wanadaiwa kujihusisha katika vitendo vya uhalifu wa kutumia ni Kasola Masingili;Amos Embe Nyamsha na Hamidu Marwa Mohamed ambao kwa
Wakiongea na waandishi wa habari mjini hapa jana waathirika hao walisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa tisa alasiri katika vitongoji vya Magharibi na Kati vya kijijini humo kufuatia yowe iliyopigwa mapema asibuhi ya kuhamasishana ili kuwachomea watu hao nyumba pamoja na kuharibu mali zao zote kama njia waliyosema ya kukitakasa kijiji hicho kutokana na uchafu huo.
Kwa mujibu wa waathirika hao kabla ya wananchi hao kufikia hatua hiyo waliazimia kupitia kikao chao yowe kilichofanyika mapema alfajiri kuwasaka watu hao ambao waliwaelezea kuwa wamekiingizia ubaya kijiji hicho tangu walipohamia kijijini hapo miaka miwili iliyopita wakitokea maeneo mbalimbali ndani ya mkoa huo.
Habari zaidi zinasema kufuatia hali hiyo ilimlazimu mkuu wa wilaya hiyo kapten Geoffrey Ngatuni akifuatana na kamati yake ya ulinzi na usalama ya wilaya kufika kijijini hapo kwa lengo la kujaribu kuwatuliza wananchi hao ingawa hata hivyo habari zinasema alikuwa amechelewa kwani alikuta tukio limeshafanyika na hivyo kuishia kufanya mkutano wa hadhara.
Akiongea na gazeti hili mkuu huyo wa wilaya alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kamati yake ya ulinzi na usalama kwa kutumia busara zake ililazimika kuwachukua watu hao na kuwapeleka kusikojulikana kwa maslahi ya usalama wao akisema kama wangebakia mahala hapo wangedhuriwa zaidi na watu hao walioonekana kujazwa na ghadhabu dhidi yao.
“Ni kweli tatizo hilo lipo na tumefika pale na kufanya mkutano wa hadhara na wananchi hao tukikemea vitendo vya kujichukulia sheria mikononi lakini pia tukiwataka watu wa jinsi hiyo wajisahihishe.Lakini kwa usalama wao tuliondoka nao.”alisema Kapteni Ngatuni alipoongea na gazeti hili kwa njia ya simu.
Kwa upande wake kamanda wa polisi mkoani Mara Robert Boazi alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alisema jeshi hilo lina taarifa kamili za kuwepo kwake na kwamba linaendelea na uchunguzi wa kujua chanzo chake sahihi na kwamba hadi leo(Ijumaa) hakuna mtu yeyote aliyekuwa akishikiliwa huku akiahidi kutoa taarifa kamili baada ya uchunguzi kukamilika.
,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,
No comments:
Post a Comment