Wednesday, June 27, 2012

Kauli ya Zitto Kabwe juu ya kutekwa na kupigwa kwa Kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dkt. Steven Ulimboka Steven

Ujumbe amenitumia Daktari yupo pale MOI

‘Kaka Zitto,hali ya Dr.Ulimboka yuko unconscious,multiple ribs fracture na kwenye mikono pia amevunjika pamoja na taya,yuko icu wanamstabilise kwanza kwasababu hapumui vizuri,the situation here is really bad,I agree with you this is outright outrageous’
Nimechukizwa sana na habari za kutekwa, kupigwa na kuumizwa vibaya kwa Dr Ulimboka, Kiongozi wa Madaktari Nchini. Mambo kama haya tumezoea kuyasikia kwenye nchi za kidikteta na kuongozwa kiimla ambapo watawala badala ya kutumia njia ya kidemokrasia na kisheria kushughulikia wanaoamini ni maadui zao katika utawala, hutumia wahuni katika Taasisi za usalama kuteka raia, kuwatesa, kuwafunga na hata kuwaua.

Sitaki kuamini kwamba Tanzania imefikia huko. Nimezungumza na baadhi ya madaktari walio karibu na Dokta Ulimboka na kujulishwa kwamba majeruhi huyu wa vitendo vya hovyo kabisa kutokea hapa nchini alikamatwa jana usiku mnamo saa sita na watu wasiojulikana na kupelekwa katika msitu wa MagwePande na kujeruhiwa vibaya. Habari hizi bado hazijathibitishwa na vyanzo huru lakini ndio zilizopo hadi hivi sasa.


Serikali kama mlinzi wa usalama kwa raia inaWAJIBU kueleza tena kwa haraka ni nini kimetokea kwa kijana huyu msomi na kiongozi wa wataalamu wenzake. Serikali INAWAJIBIKA kueleza katika nyakati kama hizi ambapo kuna mgogoro kati yake na madaktari imekuwa wapi kuhakikisha usalama wa viongozi wa madaktari ili kuepusha watu wanaoitwa ‘agente provocateure‘ kuweza kuhatarisha hali ya amani ya nchi na hata kupelekea kuweka hali ya vitisho kwa madaktari wetu.

Serikali INAWAJIBIKA kueleza kama sasa imeamua kutumia njia za kihuni kumaliza matatizo na wananchi wake.

Nimemuomba Waziri kivuli wa Afya wa CHADEMA kufuatilia suala hili kwa kwa karibu sana ili kuhakikisha kwamba ukweli wote na ukweli mtupu unafahamika. Kamwe hatuwezi kuacha Mtanzania yeyote aonewe, anyanyaswe au akandamizwe eti kwa sababu ya kudai haki yake na za wenzake. ‘An injury to one, injuries to all’


Naomba madaktari wamwangalie kwa karibu daktari mwenzao ili aweze kupata nafuu. Ulinzi uimarishwe ili kuhakikisha usalama wake.

Tuesday, June 26, 2012

MUSOMA

Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, limeonya vikali kitendo cha

Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani Tanzania, Dk. Joyce Ndalichako cha madai ya kuwafelisha wanafunzi wa kidato cha sita katika somo la maarifa ya uislamu na kudai kuwa kitendo hicho ni hujuma dhidi ya uislamu.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania Sheikh Ramadhan Said Sanze,wakati akizindua ushirika wa akiba na mikopo wa waislamu wa mji wa Musoma, unaojulikana kama Kutayba SACCOS kwenye uwanja wa shule ya msingu ya Mkendo mjini Musoma.

Sheikh Sanze, amewataka watu ambao wamehusika kuwafelisha wanafunzi wa kiislamu katika somo lao la maarifa ya uislamu kuacha kufanya hivyo, kwani matokeo ya hujuma hiyo yanaweza kusababisha chuki, uhasama na matabaka miongoni mwa wananchi.

Kwa upande Amiri Mkuu wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Nchini Sheikh Mussa Yusuf Kundecha, amewahimiza waislamu nchini kujiunga pamoja kwa ajili ya ili kukopeshana bila riba ili kuboresha maisha yao.

Waumini zaidi ya 40 wa dini ya kiislamu mjini Musoma wamehitimu mafunzo ya namna ya uendeshaji wa Saccos hiyo na kutunukiwa vyeti na zawadi mbalimbali.
,,,,,,,,,,,,,,,,,//,,,,,,,,,,,,,,,,,,,//,,,,,,,,,,,//,,,,,,,,,,,,,,

MUS0MA

SIKU chache baada ya Serikali kununua Kivuko kwaajili ya kutoa huduma ya usafiri kati ya Manispaa ya Musoma na wilaya ya Rorya mkoani Mara,kumeibuka mgogoro mkubwa ukihusisha vyama vya siasa vya CCM na Chadema,huku viongozi wa CCM wilayani Rorya wakiandaa tamko litakalo tolewa kwa Rais na Waziri wa ujenzi wakati wa uzinduzi rasmi wa safari za kivuko hicho hivi karibuni.

Wakizungumza katika mkutano wa halmashauri kuu ya CCM wilayani Rorya,baadhi ya wajumbe wa mkutano huo,wamedai baada ya kivuko hicho kuwasili mjini Musoma,viongozi wa Chadema wameonekana kukiteka kivuko hicho kwa kubadili Rangi na Jina kutoka walilopendekeza la Mv Kinesi hadi kuitwa Mv Musoma.

Baadhi ya wajumbe hao Bi Filista Nyambaya na Bw Khalfani Msima,wamesema kuwa kivuko hicho kiliombwa na wananchi wa wilaya ya Rorya lakini cha kushangaza baada ya kuwasili tu kikiwa na rangi inayofanana na ile ya bendera ya chadema kimeonekana kutekwa na kubadilishwa jina huku kilala Musoma badara ya Kinesi wilayani Rorya.

Hata hivyo akizungumza katika mkutano huo wa halmashauri kuu ya ccm,mbunge wa jimbo la Rorya Mh Lameck Airo,amesema ingawa kivuko hicho kiliombwa na wananchi wa jimbo la rorya kupitia kwa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Prof Phellemon Sarungi,lakini si jambo la busara kuanzisha mgogoro bali hoja hiyo wanapaswa kuiwasilisha kwa waziri mwenye dhamana siku ya uzinduzi rasmi wa kivuko hicho.

Akizungumzia suala hilo meneja wakala wa barabara Tanroads mkoani Mara,Mhadisi Emanuel Koroso,amesema rangi na jina la kivuko hicho halijawekwa na chama chochote cha siasa hivyo kuwaomba wananchi na wafuasi wa vyama hivyo kuachana na hoja kwani amesema nia ya serikali kutatua tatizo la usafiri katika maeneo hayo bila kujali chama cha siasa.

Serikali imenunua kivuko hicho kwaajili ya kutoa huduma ya usafiri katika ziwa victoria kwa upande wa wilaya ya rorya na musoma mjini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya rais jakaya kikwete ya kuwaondolea shida wananchi wa pande hizo mbili ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakisafiri kwa kutumia mitumbwi na boti ambazo mara nyingi si salama.
,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,//,,,,,,,,,,,,,,,,//,,,,,,,,,,,,,,,//,,,,,,,,,

RORYA

Wanawake wa kijiji cha Ikoma katika wilaya ya Roorya mkoani Mara,wanalazimika kwenda kupata huduma za matibabu hasa za vipimo mbalimbali vya uja uzito katika nchi jirani ya Kenya kutokana na kijiji hicho kukosa zahanati tangu kuanzishwa kwake miaka 40 iliyopita.

Wanawake hao wametoa kilio hicho katika kijijini hapo katika mkutano wa hadhara ambao umeitishwa na mbunge wa jimbo la Rorya Mh Lameck Airo,kwaajili ya kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa kijiji hicho.

Miongoni mwa wanawake hao Bi Monica Lucas na Bi Bather Fabiani,wamesema kukosekana kwa zahanati katika kijiji hicho pia kumechangia wanawake wengi kushindwa kupata huduma za vipimo kwa wakati wote wa uja uzito hadi kujifungua na wakati mwingine kuchangia vifo kwa wakina mama wajawazito.

Kufuatia kilio hicho,mbunge huyo Mh Lameck Airo,amemteua mkandarasi kampuni ya Sirori Investment kuanza haraka ujenzi kwaajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo la zahanati lililopo kijijini hapo katika kuwandolea adha hiyo wananchi ambayo inawafanya wanawake wajawazito na watoto kwenda kupata matibabu umbali mrefu katika wilaya ya Tarime na wakati mwingine kuvuka mpaka hadi nchi jirani ya Kenya.

Saturday, June 23, 2012

WATU WANNE WASHILIKIWA KUHUSIANA NA UJAMBAZI KATIKA HIFADHI YA TAIFA YA SERENGETI
Na Thomas Dominick,
Musoma

JESHI la Polisi Mkoa wa Mara linawashikilia na kuwahoji watu wanne wanaodaiwa kushirika katika tukio la ujambazi lililotokea June 20, mwaka huu majira ya saa 3:00 usiku Mivaro Campsite iliyopo katika Hifadi ya Taifa ya Serengeti.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Mkoa hapa, Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Absalom Mwakyoma alisema kuwa watuhumiwa hao walipatikana baada ya jeshi hlo kuendesha oparasheni kabambe ambayo ilifanikiwa kuwakamata watu hao.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ilisema kuwa majambazi wapatao nane walivamia kambi hiyo ya watalii wakiwa bunduki na mapanga, na walipofika karibu na sehemu ya kulia chakula walikutana na Meneja Msaidizi Renatus Robert (42) ambapo walimfyatulia risasi kifuani na kuanguka chini akafariki Dunia.

Baada ya hapo walikwenda kwenye hema namba 12 ambako walikuwepo Mholanzi Erick Paul (58) na kumtaka atoe fedha Uero au dola ambapo aliwaambia watoke ndipo walipompiga risasi ya paja na kumjeruhi kwa mapanga mkono wa kulia na baadaye alifariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi.

Kutokana na milio ya bunduki wananchi wa kijiji cha Ikoma Robanda walielekea kwenye Kambi hilo kwa hamasa kubwa wakiwa na silaha zao kila mmoja aliyoiona inamfaa, wahalifu hao baada ya kusikia sauti zao hawakuendelea na oparasheni yao ya uhalifu wakatoweka kwa kutumia gari walilokuwa wameliegesha porini.

Katika tukio hilo iliwamlazimu wa maliasili na utalii Balozi Khamis Kagasheki na waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Emmanuel Nchimbi kusitisha shughuli za bunge na kufika eneo hilo na kutoa maelekezo yao juu ya kukomesha matukio kama hayo yasijirudie pamoja na kuwataka wamiliki wa Makambi ndani ya Hifadhi hiyo ya Taifa kuwa na walinzi wenye silaha.
Kamanda Mwakyoma alisema kuwa Jeshi hilo linaendelea na ufuatiliaji wa wahalifu hao na kuwaomba wananchi wema kuendelea kushirikiana na Jeshi la polisi kupata taarifa za wahalifu waliobakia ili kwa pamoja wapambane na uhalifu.
                AMIA WAJITOKEZA KUMZIKA ALIYEKUWA MHARIRI WA JAMBO LEO.

Na Anthony Mayunga-Serengeti

WATANZANIA wameshauriwa kutawaliwa na hofu ya Mungu kwa kuepuka utajili unaokiuka maadili ya Mungu kwa kuwa watakosa ufalme wa Mungu.

Askofu wa dayosisi ya Rotya wa kanisa la Anglikan John Adiema katika mahubiri ya ibada ya mazishi ya aliyekuwa Mhariri mkuu wa gazeti la Jambo Leo Willy Edward Ogunde nyumbani kwao Morotonga Mugumu mjini alisema hofu ya Mungu inatakiwa kuwatawala watu wote.

                                                                  Marehemu Willy Edward

Alisema hata Yesu aliipolia kwenye kaburi la rafiki yake Lazaro kama ilivyoandikwa kwenye biblia ,machozi hayo yalikuwa kwa ajili yawaombolezaji kwa kukalia dhambi .“Umati kama ule uliokuwepo wakati Yesu analia ndio huu leo uliopo kwa wingi tukimsindikiza Willy ,ni kielelezo kuwa aliishi na watu vema ndiyo maana leo mmejaa hapa ,sijui kwa upande wa Mungu alikuwa amejiwekaje?”alihoji. Mwenyekiti wa jukwaa la wahariri.
Mwenyekiti wa jukwaa la Wahariri Tanzania Absalom Kibanda kwa masikitiko akiongoza jopo la Wahariri Kurwa Karedia,Revocatus Makaranga na Jane Mihanji alisema kifo hicho ni pigokwa wanahabari na
watanzania wote. “Ni pigo kubwa kwetu wanahabari na watanzania wote kwa kuwa alikuwa
mhimili kwenye chombo hiki,wengi wameumia sana kuondokewa na Willy,waandishi wengi wameumia sana”alisema na kupelekea Mihanji kushindwa kujizuia.

Baba mzazi amwachia Mungu.Edward Ogunde baba mzazi wa Marehemu Willy alisema yeye anamwachia
Mungu kwa kuwa ndiye alipenda akazaliwa na imempendeza kumwita kwake ,”ingawa inauma kwa kuwa niliwaandaa wanangu vizuri siku moja wanisindikize kinyume chake mimi ndio namsindikiza Willy,Mungu yu
upande wetu”alisema. Dc wa Magu anena. Jacqline Liana mkuu wa wilaya ya Magu ambaye alikuwa mhariri msaidizi
wamagazeti ya Uhuru na Mzalendo aliwataka waandishi kuhakikishawanatumia vema kalamu zao ili kumuenzi Willy kwa kuwa walifanya naye kazi kwa muda mrefu na ndiyo maana ameamua kuhudhuria mazishi hayo.

Mwenyekiti CCM ShinyangaMwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga Hamisi Mgeja ambaye alidai alikuwa rafiki wa karibu na marehemu Willy aliwataka ndugu wa Willy kumshirikisha kwa matatizo ya familia ikiwemo suala la kuwasaidia wanae kwa kuwa huo ndio wajibu kwa waliobaki.Viongozi wengine ni mkuu wa wilaya ya Serengeti kepteni Yamungu ,mwenyekiti wa CCM wilaya Chandi Marwa na askofu wa dayosisi ya Mara kanisa la Angilican,wachungaji wa madhehenu mbalimbali na waandishi
kutoka maeneo mbalimbali.

MAKAMU MWENYEKITI HALMASHAURI YA WILAYA SERENGETI AAGA DUNIA.
MAKAMU mwenyekiti wa baraza la madiwani halmashauri ya wilaya ya Serengeti na diwani wa kataya Manchira  Joseph Mechama(45)(CCM)amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu ugonjwa
wa kansa ya utumbo.

Taarifa zilizothibitishwa na kaimu Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Slivanus Lugira na kaimu makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Jumanne Kwiro zinasema amefariki juni 23,majira ya saa 12.46 mwaka huu jijini Dar es Salaam alikokuwa kwa matibabu kwa muda mrefu. Walisema taratibu za kusafirishwa mwili wa marehemu kutoka Dar es Salaam kuelekea wilayani Serengeti kwa ajili ya maziko zinaendelea na taarifa ya maziko yake itatolewa mara baada ya mwili huo kuwasili.
            Redds' miss Mara 2012 kupatikana june 29

Na Shomari Binda
Musoma,

Shindano la kumtafuta Redd's miss Mara 2012 litafanyika June 29 huku waandaji wa shindano hilo kampuni ya Homeland Entertainment$Promotion wakidai asilimia kubwa ya maandalizi ya shindano hilo yamekwisha kukamilika na kinachosubiliwa ni kumpata mrembo wa Mkoa huo atakaye shiriki katika shindano la Redd's miss Tanzania 2012.

Akizungumza na waandishi wa Habari katika kambi ya mazoezi ya warembo wanaotarajiwa kushiriki katika kinyang'anyiro hicho,mkurugenzi wa kampuni ya Homeland Goldon Mkama alisema anawashukuru wale wote ambao wameshiliiki kwa namna moja ama nyingine kutaka kufanikisha shindano la mwaka huu.
Alisema licha ya ugumu wa shughuli za kuandaa shindano hilo la warembo lakini anashukuru mpaka sasa kukamilika kwa asilimia kubwa ya maandalizi yake na kusema kuwa bado kuna nafasi kwa wale wanaohitaji kushiriki kwa namna moja ama nyingine ili kuweza kufanikisha shindano hilo.

Mkama alidai kuwa mpaka sasa warembo 8 wameshafika kambini na kuendelea na mazoezi kwa ajili ya shindano hilo waliopo chini ya msimamizi wa mazoezi hayo miss Lindi na miss Tanzania namba 3 2011Loveness Flavian ambaye kazi yake kubwa ni kuhakikisha warembo watakao shiriki shindano la Redd's miss Mara 2012 wanafanya vizuri.

Muaandaji huyo wa miss Mara 2012 aiwataja warembo ambao wapo kambini mpaka sasa kwa ajili ya kushiriki shindano hilo kuwa ni Rose James,Jacline Mzava,Aisha Bakari,Eugenia Fabian,Jesca Sprian,Justina Thomas,Love Kilasira pamoja na Hellen Mosha
Aidha mkurugenzi huyo wa kampuni ya Homeland aliishukuru kampuni ya African Gold Mine (North Mara) kwa kuendela kuwa mstari wa mbele kwa kutoa udhamini mkubwa kila mwaka katika shindano la kumtafuta mrembo wa miss Mara.

Aliwataja watu wengine waliojitokeza kudahamini shindano hilo kuwa ni chuo cha Musoma Utalii collage,Crdb banki,Coca cola,Maltivilla hotel,Mara security guard,Musoma club,Msendo mini super market pamoja na mtandao wa Shommibindablogspot $ Bindanews.

Aliongeza kuwa katika kusindikiza shindano hilo wasanii mahili wa muziki wa bongo freva Profesa J pamoja na Sharo millionea pamoja na dansa wa twanga pepeta Bokilo Bokilo wanatarajiwa kunogesha shind

Thursday, June 21, 2012

MKUU WA MKOA WA MWANZA AFUNGUA SEMINA YA UHAMASISHAJI WAANDISHI WA HABARI  KANDA YA ZIWA KUHUSU USIMAMIZI WA SHERIA YA CHAKULA, DAWA NA VIPODOZI YA MWAKA 2003 LEO KATIKA UKUMBI WA NYAKAHOJA MWANZA

 Mkuu wa mkoa wa Mwanza Injinia Ndikilo
                  Waandishi wa habari katika semina hiyo
       Mwenyekiti wa waandishi wa habari katika semina hiyo Mabere Makubi( Chnl Ten)  kutoka Mara

 Picha ya pamoja kati ya waandishi wa habari kutoka Mara na Tabora na Mkuu wa mkoa wa Mwanza

            WAZAZI NA WALEZI WATAKIWA KUFATILIA VYETI VYA KUZALIWA MAPEMA
Na Shomari Binda
Musoma,

Wazazi pamoja na walezi wametakiwa kuhakikisha wanafatilia vyeti vya kuzaliwa vya watoto mapema baada ya kuzaliwa kama inavyoelekezwa na kuacha tabia ya kuanza kufanya kazi ya kufatilia vyeti hivyo pale mtoto anapotaka kwenda chuoni au kupata ufadhiri wa kwenda kusoma nje ya Nchi.

Hayo yamesemwa na Katibu tawala wa Wilaya ya Musoma Debora Makinga alipokuwa akizungumza na BINDA NEWS juu ya kufatilia vyeti vya kuzaliwa mapema na umuhimu wake kutokana na Wananchi wengi kutokuzingatia hilo na baadae kuanza kuangaika pale wanapopata nafasi ya kufanya jambo fulani.

Alisema kwa kipindi cha hivi karibuni kumekuwepo na msungamano wa Wananchi katika ofisi ya msajili wa vizazi,vifo na ndoa wakifatilia vyeti vya kuzaliwa hususani kwa wale wanaotaka kwenda vyuoni na kudai kuwa huo si utaratibu mzuri na unaweza kumfanya mtu kukosa nafasi ya kwenda kusoma kutokana na kudharau kufatilia vyeti vya kuzaliwa mara mtoto anapozaliwa.

Makinga alisema Wazazi pamoja na walezi inabidi wabadilike na kuweka umuhimu wa pekee katika suala la kupata vyeti vya kuzaliwa vya watoto mapema bada ya kuzaliwa ili kuepuka usumbufu ambao unaweza kujitokeza pale litakapo hitajika kufanyika jambo la msingi ambalo linahusu vyeti vya kuzaliwa.

"Hili nimekuwa nikilikumbusha mara kwa mara kupitia vyombo vya Habari juu ya umuhimu wa kupata mapema vyeti vya kuzaliwa lakini bado Wazazi na walezi wamekuwa hawazingatii na matokeo wanapokuja kufatilia na kukuta kuna majukumu mengine ya kiutendaji wamekuwa wakilaumu ofisi",alisema Makinga.

"Wapo wengine licha ya kuelewa umuhimu wa cheti cha kuzaliwa wanashindwa kufatilia mapema na kuwa navyo na pale wanapopata nafasi ya kazi ama kutaka kujiendeleza zaidi kielimu ndipo wanapoanza zoezi la kufatilia cheti cha kuzaliwa,"aliongeza.

Alieleza msongamano unaojitokeza kwa sasa katika ofisi yake kuhusiana na kutafuta vyeti vya kuzaliwa umekuwa ukikwamisha kazi nyingine za kijamii na hivyo kuwaomba Wananchi pale zinapokuwa zinafanyika kazi nyingine wasilaumu bali wazingatie suala la kushughulikia suala la vyeti vya watoto mapema mara baada ya kuzaliwa.

Monday, June 18, 2012

                         DC BUNDA AONGOZA HARAMBEE YA KWAYA.

Na Naomi Milton- Serengeti

Kanisa la menonite Tanzania limetakiwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kupunguza umaskini na kuinua ubora wa maisha kwa watanzania.

Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya wa Bunda mh..Joshua Mirumbe alipokuwa akiongoza harambee ya kuchangia kwaya ya Upendo  KMT Mugumu  kanisa la menonite Tanzania wilayani Serengeti kwa ajili ya  kutoa mkanda wa picha lengo ikiwa ni  kutangaza injili.

Amesema uongozi  uwe na malengo ya  kuandaa ajira maalum kwa vijana kwa shughuli mbalimbali za kijamii mfano useremala,ushonaji,na uashi kwani hii itakuwa ni njia pekee itakayowasaidia vijana kujiendeleza kimaisha sambamba na mafunzo ya ufundi kwa vijana wote kila mkoa ili kupambana na suala la umaskin nchini

Kwa umuhimu wa kwaya ndani ya kanisa kuwa ni kuelimisha, kuburudisha na kuonya pia liwe na mtizamo mpana kuhusu  ukosefu wa ajira kwa vijana si tatizo la Tanzania pekee bali ni dunia nzima.

Kwa Tanzania  alisema tatizo hili linatokana na uchumi wetu kuwa mdogo kulinganisha na idadi ya watu waliopo kuwa kubwa.
.
Mapema akisoma risala yao mbele ya mgeni rasmi kiongozi wa kwaya ya upendo .Bw.Jamuhuri Kabati alisema wameamua kufanya harambee kutokana na mapungufu waliyonayo ndani ya kwaya.

Tatizo kubwa walilolitaja ni uchakavu wa vyombo vya muziki kama vilekinanda,gitaa,mixer,na mike vilevile kuna tatizo la ajira kwa vijana kwani vijana wengi baada ya kujitosa kwenye uimbaji wanakosa pa
kuelekea.

Jumla ya tsh.9.320,000= zimepatiakana ikiwa ni pesa taslimu na ahadi kati yan hizo mgeni rasmi alitoa tsh,3,047,000=lengo lilikuwa ni kukusanya  tsh,mil.10.

Mmoja wa waimbaji wa kwaya hiyo bi.Nezia Tanu amesema amefurahishwa na harambee hiyo kutokana na kiasi walichokipata kwani hawakutegemea kama fedha zote hizo zingepatikana kwa wakati huo.

Nae mchungaji wa kanisa hilo bw. Cleophace Nyamataga ametoa shukrani zake za dhati kwa mgeni rasmi na wote waliochangia kwaya yake kwa hali na mali  kwani wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutimiza lengo lao nawamehaidi kutenda sawasawa na walivyokusudia.
                                                  KWAHERI WILLY EDWARD


Bodi ya Wakurugenzi na wafanyakazi wa Jambo Concepts Ltd inayochapisha gazeti la Jambo Leo na Jarida la Jambo Brand wanapenda kuwajulisha Watanzania na wanahabari wote nchini kwamba Mhariri Mkuu wa gazeti hilo, Willy Edward Ogunde amefariki dunia mjini Morogoro.

Tunasikitika mno kuondokewa na mfanyakazi wetu ambaye alikuwa mchapakazi na mwenye ueledi mkubwa katika tasnia ya uandishi wa habari. Kwa wanaomfahamu Willy watakuwa mashahidi wa hilo tunalosema.

Hadi sasa hatujapata taarifa rasmi za kidaktari kuhusu kifo chake, lakini taarifa zilizopatikana kutoka kwa ndugu wa marehemu zinasema alikuwa anasumbuliwa na tatizo la moyo. Mwili wa marehemu utawasili leo, Juni 17, 2012 na maandilizi ya mazishi yanaendelea.
 WasifuWilly Edward Daniel Ogunde ambaye alikuwa Mhariri Mkuu wa gazeti la Jambo Leo alizaliwa Machi 7, 1974 katika Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.

Alisoma shule ya msingi Mapinduzi mwaka 1983 hadi 1989 kisha elimu ya Sekondari katika shule ya Serengeti mwaka 1990 hadi 1993.Baadaye alijiunga na shule ya Sekondari Musoma kidato cha tano na sita mwaka 1994 na 1995.

Mwaka 1996 alijiunga na Kampuni ya uchapishaji wa magazeti ya BTL akiwa mwandishi wa gazeti wakati huo likiitwa Majira Jioni.

Akiwa na kampuni hiyo alipata mafunzo mafupi ya kikazi yakiwemo ya kompyuta na ya uandishi wa habari.

Mwaka 1998 alihamishwa kitendo kutoka kwenye gazeti la Majira Jioni kwenda kwenye gazeti jipya la Dar Leo na kuwa mwandishi wa habari wa hazeti hilo lakini pia akishikilia nafasi ambazo alikuwa akizitumikia kwenye gazeti la Majira Jioni.

Alifanikiwa kuaminika na kutokana na uwezo wake kazini alipanda daraja na kuwa Mhariri wa gazeti la Dar Leo kuanzia mwaka 2002 hadi 2005.

Kipindi cha mwaka 2006 hadi 2007 alikuwa akitumikia nafasi ya Mhariri wa Msaidizi wa Michezo gazeti la Majira na baadaye 2006 hadi 2007 akawa Mhariri wa Michezo wa gazeti hilo .

Mwaka 2006 hadi 2007 alipata cheti cha elimu ya uandishi wa habari katika Chuo cha Ceylon (CSJ).

Amesafiri nchi mbalimbali duniani katika kuripoti habari za michezo na burudani ikiwemo Afrika Kusini mwaka 2003 hadi 2006 kwenye mashindano ya Big Brother Africa.

Pia mwaka 2007, 2008 na 2009 Kenya, Senegal na Uingereza kuripoti habari za michgezo kupitia Super Sport.Mei mwaka huu alisafiri kwenda nchini Uturuki kwenye kongamano ya wadau wa masuala ya mawasiliano ambako alikuwa kiongozi wa wahariri waliotoka Tanzania na kutoa mada kw iliyohusu mwenendo wa vyombo vya habari nchini Tanzania.

Nje ya kazi ya uandishi wa habari mwaka 2008 na 2009 alifanya kazi katika kampuni ya matangazo ya ZK akiwa Ofisa Habari na Uhusiano.

Miongoni mwa vyombo vya habari ambavyo aliwahi kufanya kazi enzi za uhai wake ni pamoja na Kampuni ya New Habari ambayo aliitumikia mwaka 2007 na 2008 akiwa Mhariri Msaidizi wa gazeti la Bingwa.

Hatimaye mwaka 2008 alikuwa Mhariri Mkuu wa gazeti la Bingwa kabla hajaacha kazi katika kampuni hiyo na kujiunga na Kampuni ya ZK.

Alijiunga na gazeti la Jambo Leo mwaka 2010 akiwa Mhariri wa Habari na kuanzia mwaka jana hadi mauti ilipomkuta alikuwa Mhariri Mkuu wa gazeti la Jambo Leo.

Taarifa hii imetolewa na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Jambo Concepts Ltd,

Ramadhan Kibanike.

source Full shangwe

Saturday, June 16, 2012

                            SIKU YA MTOTO WA AFRIKA


SERIKALI wilayani Butiama mkoani Mara,imelaani vikali vitendo vya ukiukwaji wa haki za watoto ikiwa ni pamoja na unyanyasaji ambao umekuwa ukifanywa na baadhi ya walezi na wazazi katika wilaya hiyo na mkoa wa Mara kwa ujumla.

Mkuu wa wilaya ya Butiama Bi Angelina Mabula,ameyasema hayo katika kijiji cha Kwibara kata ya Mugango wilayani humo katika maazimisho ya mtoto wa Afrika ambayo yamefanyika kiwilaya kijijini hapo.

Amesema wazazi na walezi wanawajibu wa kuwapa watoto haki zao za kimsingi ikiwa ni utekelezaji wa sera ya mtoto ya Tanzania ya mwaka 2008 na sheria ya mtoto ya mwaka 2009,kuwalinda watoto na mambo yote maovu ikiwemo kuwasikiliza,kuwajali na kuwaendeleza kiroho na kimwili.

Awali katika risala iliyosomwa na watoto wa Halmashauri hiyo wamesema kuwa wanahitaji kulindwa  dhidi ya mambo maovu ikiwemo ukatili,utekelezwaji,ubakaji,unajisi,ukeketwaji,ubaguzi wa kijinsia na kufanyishwa kazi za malipo.

Wamesema kumekuwepo na vitendo vya ubaguzi kwa watoto ambao ni walemavu  wakitolea mfano sense ya mwaka 2008 katika wilaya hiyo watoto 1056 hawakupelekwa shule kwa sababu ya ulemavu wao.

Maadhimisho ya mtoto wa Afrika hufanyika kila june 16 ambapo nchi mbalimbali barani Afrika hukumbuka mauaji ya kikatili ya watoto wa kitongoji cha Soweto nchini Afrika Kusini, waliokuwa wakidai haki za usawa katika elimu,kufundishwa kwa kutumia lugha yao kutoka mikononi mwa makaburu.

Friday, June 15, 2012

 WAHAMIAJI NA WALOWEZI 319 WAKAMATWA.

 Dinna Maningo,Mara.

JUMLA ya wahamiaji haramu na walowezi  wapatao 319 wamekamatwa kwa kipindi cha Januari hadi Mei Mwaka huu.

Akizungumza na Mwandishi wa habari ofisini kwake, Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mara, Jacob Sambai alisema kuwa kati ya hao wapo waliofikishwa mahamakani na wapo waliorejeshwa kwao na wengine waliotumikia kifungo.

Alisema kuwa kati ya hao wapo Wakenya 259, Wathiopia 44, Warundi 8,Wasomali 3, Waganda 3 na Wakongo 2.

Alisema kuwa  hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuwafukuza nchini ambapo waliofukuzwa ni watu wapatao 197 kutoka nchi mbalimbalimbali na wanaoendelea kuchunguzwa ni 39.

alisema kuwa waliokutwa ni wakimbizi ni 8, waliofugwa kwa amri ya mahakama ni 9 na kwa wale ambao kesi zao ziko mahakamani ni 7 ambapo waliogundulika ni watanzania kutokana na mwingiliano na kufanana kwa lugha kati ya makabila ya Wakurya wa Kenya na Wajaluo wa Kenya ni 9 na walioharalisha ukazi ni watu 60.  

Sambai alisema kuwa Idara hiyo ina changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwa ni pamoja na uhalifu wanaofanyiwa wafanyakazi wawapo kazini kuchomwa visu hadharani,Mauaji,  uvamizi wa kutumia silaha hali ambayo inahatarisha maisha yao pamoja na tatizo la ubora na ufanisi wa kazi jambo ambalo limewafanya  watumishi kuwa na hofu kubwa ya kufanya kazi huku wakihofia usalama wao.

“Kuna baadhi ya wenzetu si vizuri kuwataja majina yao waliwahi kuvamiwa kwa kutumia silaha,kwa bahati njema walipona na wengine kuchomwa visu wakiwa kazini,madhalani basi limekuja na abiria unawaambia washuke ili wagongewe hati ya kusafiria passport, ghafla anakuja mtu usiyemfahamu anakutaka vidole, mmoja wetu alifanyiwa hivyo, sasa hii ni hatari sana” Alisema Sambai.

Alisema kuwa chagamoto zingine zinazoikabili Idara hiyo ni pamoja na  mwingiliano wa makabila kati ya Wakenya wa kabila la Wajaluo na Wakenya wa kabila la Wakurya ambao wanafanana tabia na  Wakurya Watanzania na Wajaluo wa Tanzania, kwa hiyo inakuwa ngumu kuwatofautisha na kuwatambua kutokana na lugha zao kufanana na baadhi yao wamekuwa na mahusiano ya kindugu,pamoja na Uhaba watumishi na ukosefu wa nyumba za watumishi imekuwa ikikwamisha ufanisi wa kazi kwenye idara hiyo.

Aidha kumekuwepo na baadhi ya viongozi wakiwemo wenyeviti wa vijiji na baadhi viongozi wa vyama vya siasa hasa madiwani wamekuwa na asili ya wakenya, hivyo inakuwa ngumu kumtaja mtu ambaye ameingia nchini na anaishi bila kibali kutokana na mahusiano kati yao jambo ambalo limekuwa likikwamisha utendaji kazi.

Aliongeza kuwa ukubwa wa mipaka umekuwa changamoto kubwa kwa idara hiyo kutokana na urefu wake na umbali kwa vituo vya ukaguzi vya Kogaja na Shirati kuwa nje ya mpaka nakwamba ni vyema ikahamishwa ili kuweka ufanisi wa kazi na kufufuliwa  kwa kituo cha Bolega kilichoko Wilaya ya Tarime ambapo awali kilikuwa na msaada mkubwa.

Alisema kuwa kwa mwaka huu Idara ya Uhamiaji Mkoa huu imeweza kutoa semina katika Tarafa zipatazo nane zenye kata 56 na vijiji au mitaa 210 katika Wilaya za Bunda Tarafa ya Kikopya na Chamriho, Wilaya ya Rorya Tarafa ya Girango  na Tarafa ya Nyancha, Wilaya ya Serengeti Tarafa ya Logolo na Gurument, Wilaya ya Tarime Tarafa ya Nyancha,vijiji vya Ichange na Inchugu, Wilaya ya Musoma inatarajiwa kufanyika katika Tarafa ya Nyancha na Makongoro.

Semina hizo zilikuwa na  lengo la kuweka ufanisi na kutoa taarifa kwa vyombo vya dola ambapo namba za simu za viongozi zilitolewa kwao ili kutoa taarifa panapotokea mtu ameingia nchini na anaishi bila kuwa na vibali.

Pia aliwasisitiza viongozi hao kuwapa moyo wananchi kwani wamekuwa na uwoga wa kuwataja wahamiaji haramu kutokana na kuhofia usalama wao wa kuhatarisha maisha.

MWENGE WA UHURU WAWASILI ZANZIBAR UKITOKEA MKONI LINDI
Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi
ZANZIBAR IJUMAA JUNI 15, 2012. Mwenge wa Uhuru leo Umeingia Kisiwani Zanzibar ambapo Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Kapteni Honest Mwanossa ameweka mawe ya msingi na kuzindua miradi mbali mbali ya maendeleo katika mkoa wa mjini Magharibi.
Akiweka jiwe la Msingi la kituo kidogo cha Polisi cha Kombeni Mjini Zanzibar, kiongozi huyo amewataka viongozi wa Kitaifa kuepuka ufujaji wa fedha za wananchi na kujiingiza kwenye ufisadi na kuwataka wafanye mambo kwa maslahi ya Taifa.
Awali katika risala yao kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge, wananchi wa Makombeni wameliomba Jeshi la Polisi kuangalia uwezekano wa kuharakisha ujenzi wa kituo hicho ili kupunguza kero ya uhalifu katika eneo hilo.
Moja ya ujumbe wa Mwenge wa mwaka huu umehimiza umuhimu wa kila mmoja wetu kuhesabiwa katika Sensa ya kitaifa ili kuiwezesha Serikali kupanga vema maendeleo kwa wananchi wake.
Mwenge huo umewasili kisiwani Zanzibar ukiotokea mkoa wa Lindi ambako ulikuwa ukikimbizwa katika wilaya mbalimbali za mkoa huo.
Ukiwa Kisiwani hapa, Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa atazindua na kuweka mawe ya msingi ya miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilaya na mikoa yote mitano ya Unguja na Pemba kabla ya kuendelea na mbio zake katika mikoa mingine ya Tanzania Bara.
WANANCHI  IKOMA WAMUHITAJI WAZIRI WA ARDHI.

Dinna Maningo,Rorya.

Wananchi wa Kijiji cha Ikoma Kata ya Ikoma Wilayani Rorya Mkoani Mara wamemuomba Waziri wa Ardhi kufika Kijijini hapo kutatua tatizo linaloendelea la mgogoro wa umiliki wa ardhi kwa madai kuwa uongozi  wa Mkoa wa Mara umeshindwa kutatua  tatizo la kuporywa na kukodishwa ardhi kwa wageni kutoka Kenya na wananchi wa Kijiji cha Nyamuhunda-Tarime.

Walisema kuwa tatizo la wageni kukodishwa ardhi na kumilikishwa ardhi kinyume cha sheria na wale wa kijiji cha Nyamuhunda-Tarime,ni kuendelea kuibua migogoro baina ya wanakijiji cha Ikoma na kijiji cha Nyamuhunda.

Hayo yalibainika kwenye mkutano wa wananchi wa kijiji cha Ikoma uliohitishwa na Mwenyekiti wa kijiji hicho Adriano Jalando uliohudhuriwa na wananchi wa kijiji cha Ikoma,wajumbe wote wa Serikali ya Kijiji,Diwani wa kata ya Ikoma Laulent Adriano.

Mkutano huo ulikuwa unazungumzia ajenda ya wanaikoma kunyang’anywa ardhi na mashamba yao,kulazimishwa kuhama toka kwenye makazi yao pamoja na huhararishwa kwa  wakazi wa Tarime kuchukua mashamba ya wanaikoma.

Wananchi hao walisema kuwa licha ya Mkuu wa Mkoa wa Mara John Tuppa kuwaagiza mbele ya mkutano Wakurugenzi na Maofisa uhamiaji Wilaya ya Rorya na Tarime kutatua  tatizo la mgogoro wa ardhi na kukodishwa kwa mashamba kwa wageni pamoja na kuhakiki uraia wa wananchi wa Ikoma lakini hadi sasa hakuna ufatiliaji wala utekelezaji wowote uliofanyika.

Samweli Makori Mjumbe wa Serikali ya kijiji alisema kushindwakutatuliwa kwa wakati mgogoro wa ardhi wa wananchi wa Ikoma na kutobainishiwa maeneo halali ya kuishi imepelekea wananchi wa kitongoji cha Nyamuhunda na Nyanthacho waliovamiwa  na nyumba zao kuchomwa moto na mazao kuharibiwa kubaki kuendelea kuhifadhiwa na wananchi wenzao wa Ikoma jambo ambalo linalosababisha kushindwa kumudu gharama za kuwahifadhi.

“Baada ya kutokea mapigano baina ya Waluo na Wakurya tarehe 7-8 tukiwa kwenye mkutano wa wananchi Ikoma mkuu wa mkoa aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri ya Rorya na Tarime kushughulikia tatizo la kukodishwa ardhi kwa Wakenya,akawaagiza maofisa uhamiaji kuanza zoezi mara moja la kuhakiki uraia wa wananchi wa ikoma na wananchi 113 wanaotakiwa kusajiriwa Ikoma pamoja na wa Nyamuhunda kama njia ya kuwabaini waliomilikishwa ardhi kinyume cha sheria”alisema Makori.

Aliongeza kuwa”Ajabu mwezi mzima umekwisha hakuna utekelezaji  wowote mimi mwenyewe nahifadhi watu wawili na familia zao ambao walifukuzwa kwenye makazi yao na Wakurya wa Tarime na lemewa na mzigo maana toka mapigano na mali zao kuporwa na kuchomwa moto hawajawahi kupewa msaada wowote toka Serikalini sasa tunauomba Waziri wa ardhi aje atusaidie huu mgogoro maana Mkoa nao umeshindwa hata kufatilia  na kuhakikisha wanaikoma wanatatuliwa tatizo la mgogoro wa ardhi ikishindikana ngazi ya mkoa ninachofata ni Taifa”alisema.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Nyanthcho Gasper Olooch alisema kuwa baada ya RC kumuagiza Mkurugenzi wa Halimashauri ya Rorya kutatua mgogoro kwa sasa hali si shwari Ikoma kwa madai kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Rorya Charles Chacha  akiwa ameongozana na Ofisa utumishi na polisi waliwaagiza wananchi wa kitongoji hicho kubomoa nyumba zao ambapo alitoa siku tatu kufikia tarehe 8 juni mwaka huu wawe tayali wameshabomoa ambapo baaadhi yao walitii agizo na wengine wamekaidi na waliokubali wanaifadhiwa kwa ndugu zao baaada ya kukosa mahali pa kuishi.

Pia wananchi walilaani kitendo cha polisi wa Tarime kwa kitendo cha walichokifanya cha kuwakamata ovyo wananchi 30 wa kijiji cha Ikoma-Rorya wasiokuwa na hatia  akiwemo Diwani wa kata ya Ikoma Laulent Adriano na Mwenyekiti wa Kijiji na kuwekwa ndani kwa siku 4 katika kituo cha polisi Sirari-Tarime kwa madai walihusika kufanya uchochezi katika mapigano baina ya Waluo na Wakurya huku wenzao Wakurya wa kijiji cha Nyamuhunda-Tarime wakisalia kuwa huru pasipokukamatwa jambo ambalo walisema ni ubaguzi wa kikabila,
PIKIPIKI YAGONGA NA KUUA, DEREVA WA BODABODA AVUNJIKA TAYA
Na Mohammed Mhina na Pardon Mbwate, wa Jeshi la Polisi
KIGOMA ALHAMISI JUNI 14, 2012 Mzee mmoja mwenye umri wa miaka 60 mkazi wa  kijiji cha Muhunga Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma Vesta  Mahwa, amefariki dunia baada ya kugongwa na pikipiki huko kwenye Barabara ya Lumumba eneo la Mwanga mjini Kigoma.
Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma ACP. Frasser Kashai, amesema kuwa ajali hiyo ilimetokea majira ya saa 12.45 jioni ya Jumapili wiki iliyopita  huko kwenye Barabara ya Lumumba Mwanga mjini Kigoma.
Amesema ajali hiyo ilitokea wakati Dereva mmoja wa bodaboda aitwaye Kayuza Mgambo(35), mkazi wa Burega mkoani Kigoma alipokuwa akiende pikipiki yake kwa mwende wa kasi na hatimaye kumgonga mzee huyo aliyekuwa  akitembea pembeni mwa barabara.
Alisema mpitanjia huyo ambaye kwa sasa ni marehemu, alipata jelaha kubwa kichwani huku Dereva huyo wa pikipiki yeye akivunjika taya zote na kupelekea kupoteza fahamu.
Kamanda Kashai amesema mara baada ya ajali hiyo, majeruhi wote walichukuliwa kupelekwa katika Hospitali ya Mkoa Kigoma Maweni kwa matibabu zaidi lakini wakati madaktari walipokuwa wakiendelea kuwatibu majeruhi hao, mzee Mahwa alifariki dunia.
Hata hivyo, Kamanda Kashai amesema, dereva wa pikipiki ambaye alikuwa akiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Mkoa ya Maweni, hivi sasa amehamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando mkoani Mwanza kwa matibabu zaidi ya taya zake.
Katika tukio lingine, Jeshi la Polisi mkoani linamshikilia mkazi mmoja mkazi wa Mpeta Sarah Dasse(23), kwa tuhuma za kumua mtoto wake aitwaye Zainabu Sita mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu kwa kumkaba shingo hadi kufa.
Kamanda Kashai amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa chanzo cha mauaji hayo na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu shitaka lake la mauaji ya kikatili.
Aidha Kamanda Kashai, ametoa wito kwa madereva wa pikipiki (bodaboda) kuwa  mbali ya kujiepusha na uporwaji wa pikipiki zao na wateja, lakini pia amewataka kuwa waangalifu barabarani ili wasiwe kikwazo ama kusababisha ajali kwa watumiaji wengine wa barabara.
Kuhusiana na masuala mengine ya Kiusalama, Kamanda Kashai pia amewaomba wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi hilo kwa kutoa taarifa za siri Polisi endap[o watabaini kuwepo kwa uhalifu na wahalifu ili wahusika wawekewe mitege na kutiwa mbaroni.
Mwisho

Wednesday, June 13, 2012

MTOTO MCHANGA AOKOTWA HAI AKIWA AMETUPWA KWENYE MIBA.

Dinna Maningo,Tarime

Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Tarime Mkoani Mara Marco Nega amewataka wanawake  kuepukana na mimba ambao hazijatarajiwa ili kuepukana na tatizo linaloendelea nchini la kutupwa kwa watoto wachanga pindi wanapozaliwa.

Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake Nega alisema kuwa imefika wakati wanawake watambue umuhimu na haki ya mtoto ya kuishi kwani wanawake wamekuwa wakibeba ujauzito na kisha kutoa mimba huku wanawake wengine wakitupa watoto wachanga pindi wanapojifungua.

Dactari Nega alisema kuwa mnamo tarehe 10 siku ya jumapili asubuhi mtoto mchanga akiwa ameokotwa na msamalia mwema akiwa ametupwa kwenye fensi ya miba mtaa wa Bomani mjini Tarime alifikishwa hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu baada ya kuonekana mwili wake kuchomwa na miba.

"Wanawake wamepukane na mimba zisizotarajiwa hii itasaidia kupunguza tatizo la watoto wachanga kutupwa au kunyongwa pindi wazaliwapo,ikishindikana wafuate uzazi wa mpango hospitali inatoa huduma bure na siyo kutupa mtoto ambaye umemlea kwa miezi 9 tumboni leo hii mama anajifungua na kutupa mtoto huo ni ukatiki kwa mtoto asiye na hatia"alisema Nega.

"Anaongeza"tumempokea mtoto kutoka kwa msamalia mwema tunampatia matibabu kwa sababu alikuwa amechomwa na miba tumeitoa miba yote na kumpaka dawa na sasa anaendelea vizuri anapatiwa uduma ya kunyweshwa maziwa wa ng'ombena mama aliyemwokota ndiye anaye hapa hospitalini anamlea wakati tunafanya maandalizi ya kumpeleka kituo cha Misheni cha kulelea watoto kilichopo Nyabange Musoma,  Serikali haina vituo vya kutunza watoto kama hao wakifika hospitalini tunaomba kituo cha misheni wakikubali tunawapelekea ili wawalee.


Hellena Bon alisema kuwa alimwokota mtoto huyo aliyekuwa ametupwa katika fensi ya miba Nyumani kwakwe nakwamba yuko tayali kumlea mtoto huyo baada ya kutimiza miaka 2 atakayolelewa kwenye kituo cha misheni Musoma.

"Tunahisi mtoto alitupwa usiku wa saa 6 siku ya jumamosi  usiku huo tulisikia sauti ya mtoto akilia nilifikili ni kwa jilani tukalala ilipofika jumapili asubuhi mwanangu akiwa anafagia uwanja alimkuta mtoto huyo akiwa ametupwa kwenye fensi ya miba ikabidi tuchukue panga na kukatakata ili kumfikia mtoto bahati nzuri alikuwa hai mtoto wa kiume isipokuwa alikuwa amechomwa na miba katika sehemu za mwili nikampeleka hospitali nashukuru amepatiwa huduma nzuri na anaendelea vizuri kama unavyomuona anakunywa maziwa ya Ng'ombe na sasa anafanyiwa utaratibu apelekwe kituo cha kulelea watoto atakapofikisha miaka 2 ntamchukua na kumtunza ntakuwa namtembelea tumempatia jina la baraka kwa sababu ni muujiza wa mungu maana mtoto kakesha kwenye baridi tena akiwa uchi wa myama akiwa ameochoma miba na wakati huo kitovu kilikuwa wazi lakini yuko hai hadi sasa hata tulipomwokota hakuwa na mduu yeyote."alisema mama huyo.

Pia mganga Nega ameishauri Serikali kuanzisha vituo vya kulelea watoto katika hospitali za Wilaya na Mkoa kama njia ya kurahisisha uduma kwa watoto kama hao na kuongeza kuwa kuna haja  ya elimu ya uzazi kufundishwa mashuleni ili wanafunzi waelewe jinsi ya kujikinga na kuondokana na mimba zisizotarajiwa.

Kamanda wa polisi Mkoa wa kipolisi Tarime/Rorya Justus Kamugisha alisibitisha kuokotwa kwa kichanga hicho na kwamba hadi sasa hakuna aliyekamatwa kutupa mtoto huyo ambapo pia amewataka wananchi kwa kushirikiana na polisi kumbaini muhusika wa tukio hilo la kutupa mtoto.
POLISI KIGOMA WAPAMBANA NA MAJAMBAZI NA KUFANIKIWA KUMUUA MMOJA NA KUPATA SILAHA AINA YA SMG YENYE RISASI NNE
Na Mohammed Mhina na Pardon Mbwate, wa Jeshi la Polisi
KIGOMA JUMATANO JUNI 12, 2012 Makachero wa Jeshi la Polisi mkoani Kigoma jana walilazimika kutumia risasi kupambana na kundi la majambazi wenye silaha waliokuwa wamepanga kumvamia mmoja wa wafanya biashara mkoani humo.
Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma ACP. Frasser Kashai, amesema kuwa katika tukio hilo Polisi walimpiga risasi mmoja wa majambazi hayo aliejulikana kwa jina la Lowasi Moria(22) mkazi wa Kijiji cha Kabale mkoani humo.
Kamanda Kashai amesema wakati wa mapambano hayo, majambazi wengine watatu walifanikiwa kutoroka huku wakimuacha mwenzao aliyekuwa na silaha hiyo aina ya SMG akiwa anagaragara chini kutokana na majeraha ya risasi.
Hata hivyo Kamanda Kashai amesema jambazi huyo aliyekuwa na SMG yenye namba TU 8453 ikiwa na risasi nne zilizobaki kwenye magazine yake alifariki dunia wakati Polisi walipokuwa wakimpeleka Hospitali kwa matibabu.
Kamanda kashai amesema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 06.00 mchana huko kwenye pori la Ruhuru lililopo karibu ya kijiji cha Gwarama wilaya ya  Kibondo mkoani Kigoma.
Amesema Polisi walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa kuna majambazi  yenye silaha na wamepanga kuwavamia wafanyabiashara wanaopita katika eneo hilo na ndipo askari waliokuwa wakifanya doria katika barabara hiyo walipoamua kuweka mtego katika eneo hilo.
Kamanda huyo amesema kuwa, wakati wakiwa katika eneo hilo, Polisi walimuona mtu mmoja akiwa na pikipiki akitokea Kakonko kwenda Muhange Kabale na baada ya muda si mrefu majambazi hayo walijitokeza na kumvamia na ndipo walipoanza kurushiana risasi na kufanikiwa kumjeruhi mmoja wao.
Katika tukio lingine Kamanda Kashai amesema juzi majira ya saa nne usiku huko kwenye eneo la Mwanga mjini Kigoma, dereva mmoja wa bodaboda aitwaye Puldence Gasto(28), mkazi wa Majengo alimwagiwa tindikali usoni na abiria aliyembeba kisha kumpora pikipiki yake.
Kamanda huyo ameitaja pikipiki iliyoporwa kuwa ni yenye namba T 692 BLZ aina ya SUNLG, rangi nyekundu ambayo hadi sasa haijajulikana mahali ilipo.
Amesema dereva huyo wa bodaboda amelazwa kwenye hospitali ya mkoa ya Maweni kwa matibabu zaidi wakati Polisi wakiendelea na msako dhidi mtuhumiwa pamoja na pikipiki hiyo.
Kufuatia tukio hilo, Kamanda Kashai, ametoa wito kwa vijana waendesha boda boda mkoani humo, kuwa na ushirikiano na kwamba kila mmoja wao amzingatie abiria aliyechukuliwa na mmoja wao ili iwe rahisi kumkamata linapotokea tatizo kama hilo.
Mwisho
           MBARONI KWAKUJIFANYA WAGANGA WA KIENYEJI
Na. Luppy Kung'alo, Polisi Dodoma.
DODOMA JUMATANO JUNE 13- 06 – 2012 : Jeshi la Polisi Mkoani Dodoma linawashikilia watuhumiwa tisa wa utapeli wanaojifanya Waganga wa Jadi na Tiba Asilia kwa kuwalaghai wananchi katika vijiji mbalimbali kisha  kuwatapeli na  kusababisha hofu, na uvunjifu wa Amani miongoni mwa wanakijiji mkoani humo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Bw. Zelothe Stephen akiwaonyesha waandishi wa habari hawapo pichani vyeti feki vya watuhumiwa wa  kundi la Matapeli la LAMBA LAMBA   vyeti hivyo ni vya (UMAWATI )– cha mtuhumiwa  DK. Shabani R Kisoma amacho kirefu chake ni UMOJA WA WAGANGA WATAFITI WA MAGONJWA  SUGU UKIMWI NA TIBA ASILIA TANZANIA, na  (CHAUMUTA) – Cha mtuhumiwa anayejiita DK. Hussein Shomari Mabogo, ambaye amekamatwa , kirefu chake ni CHAMA CHA UTAFITI WA MAGONJWA SUGU NA UKIMWI KWA TIBA ASILIA.
Pic: Na Luppy Kung’alo wa Jeshi la Polisi Dodoma.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Bw. Zelothe Stephen alisema watuhumiwa hao wanajiita LAMBA LAMBA walikamatwa juzi  katika Wilaya ya Kongwa, katika kijiji cha Mkoka  baada ya Polisi kupata taarifa kuwa, wanakijiji hicho kuwavamia katika nyumba waliyofikia na kutaka kuwauwa. 

    Baadhi ya watuhumiwa wa utapeli wa kufanya waganga wa kienyeji wa  Kundi la Lamba Lamba  wakiwa wameshika dhana za kazi wakiwaonyesha waandishi wa habari pamoja na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Bw. Zelothe Stephen hawapo pichani. Kutoka kushoto waliovaa kawaida ni Mkude S/O Mwenda 32 yrs, Mkulima, na Joseph S/O John miaka 27, Mkulima, wote wakazi wa Mkoka – Kongwa na  SALEHE S/O OMARI, mwenye umri wa miaka26, mkulima wa Songe Kilindi Mkoani Tanga aliyevaa lubega nyekundu kwa nyeusi na ndani ana fulana mistari.
 
 
Pic: Na Luppy Kung’alo wa Jeshi la Polisi Dodoma.
 

”Matapeli hawa wametokea Mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Marogoro, na kuvamia mkoa wetu, kisha kufanya utapeli wao na kuzusha hali ya hofu na isiyo ya kawaida kwa wanakijiji wa maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dodoma”. Alisisitiza Kamanda Zelothe Stephen.
Aidha Mkuu huyo wa Polisi Mkoa wa Dodoma alisema, Kundi hilo la LAMBA LAMBA limekuwa  likichochea Chuki na Uadui  miongoni mwa wanajamii kwa kufanya vitendo vya kupandikiza vitu nyakati za usiku, halafu baadae  mchana wanakwenda kuvifukua na kudai wanabaini wachawi na kutoa uchawi katika kila nyumba kwa madai ya kualikwa na wazee wa Kimila.
Kamanda Zelothe Stephen alisema Matapeli hao, wamedai kualikwa na wazee wa kimila  chini ya Mwenyekiti na Katibu waitwao SAMANDARO S/O?  Na CHIPENDWA S/O? Na kupewa makazi katika nyumba mbili za ukoo wa MAPUGA S/O? Ambazo zinasimamiwa na Bw. SOSPETER S/O MAPUGA.

 Watuhumiwa wa utapeli wa kujifanya Waganga wa Kienyeji na Tiba Asilia wa  Kundi la Lamba Lamba  wakiwa wameshika dhana za kazi, wakitekeleza amri ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Bw. Zelothe Stephen kuonyesha kile wanachowafanyia wanakijiji mbele ya waandishi wa habari pamoja na Kamanda huyo  hawapo pichani.

Akizungumza moja ya tukio lilozua hofu na kusababisha uvunjifu wa amani alisema katika shuguli zao walipita kila nyumba katika kijiji walichodai kualikwa na wazee hao  lakini walipofika  katika nyumba ya MESHACK s/o MAPUGA aliwakatilia kuingia kwake hivyo waliondoka kwenda katika vijiji vingine.
Alisema Baada ya kuondoka  hapo Mtoto wa Mzee MESHACK S/O MAPUGA aitwaye MARTHA S/O AINEA MAPUGA MIAKA (34) mgogo mkazi wa kijiji cha Mlanje alianza kuumwa tumbo kisha kupelekwa zahanati ya Mkoka na hatimaye Hospitali ya wilaya Kongwa ambapo madaktari walithibitisha kifo cha binti huyo kutohusiana na imani za kishirikina lakini kwa bahati mbaya alifarikia dunia usiku wa tarehe 10/06/2012 akiwa Hospitalini hapa.

 Watuhumiwa wa utapeli wa kujifanya Waganga wa Kienyeji na Tiba Asilia wa  Kundi la Lamba Lamba  wakiwa wameshika dhana za kazi, wakitekeleza amri ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Bw. Zelothe Stephen kuonyesha kile wanachowafanyia wanakijiji mbele ya waandishi wa habari pamoja na Kamanda huyo  hawapo pichani.
”Kifo hicho kilileta sintofahamu katika familia hiyo, iliyopelekea kufikiri kwamba kikundi cha LAMBA LAMBA walihusika na kwamba  ndio tatizo kwa sababu za imani kishirikina.”aliongeza Bw, Zelothe Stephen.
Mkuu huyo wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma alisema kutokana na hali hiyo  wanakijiji waliungana na familia ya wafiwa na kwenda kuwavamia kundi la LAMBA LAMBA   wakiwa na silaha za jadi, ambazo ni mikuki, mapanga na marungu kwa lengo la kutaka kuwaua lakini walifanikiwa kuvunja mlango na madirisha na kukuta wametoroka. 
Baadhi ya wanakijiji walitoa   taarifa  za tukio hilo kwa Jeshi la Polisi na  Operesheni ya kuwatafuta watu hao ilianza  ambapo jumla ya watuhumiwa saba kati ya tisa wa kundi hilo  walikamatwa usiku huo na wengine wawili walikamatwa siku iliyofuta wakiwa wanawafuatilia wenzao, alisema Kamanda Zelothe.
 Bw. Zelothe Stepen alisistiza kwamba  pindi upelelezi  utakapo kamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.
Hata hivyo Kamanda Zelothe alisema, Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limeunda Kikosi kazi Maalumu katika wilaya zake zote kwa lengo la  kufanya Operesheni Maalum  ili kudhibiti  na kutokomeza kundi hilo na washirika  wake na kuahidi kuwasiliana na Makamanda wenzake wa mikoa ili kudhibiti vitendo hivyo.
”Napenda kutoa wito kwa wananchi wote, viongozi wa Serikali katika ngazi za Vijiji, Kata, Tarafa na  Wilaya kusimamia Sheria, Kanuni na taratibu za nchi zinavyotaka, ili kuweza kudhibiti uhalifu huu na  kuondoa hali ya sintofahami miongoni mwa jamii inayoweza  kusababisha uvunjifu wa Amani ndani na nje ya mkoa wa Dodoma inatokomezwa.” Alisistiza kamanda Zelothe Steven