Friday, September 14, 2012

MWANDISHI AFUKUZWA UANACHAMA KWA KUWASALITI WENZAKE

MUSOMA

CHAMA cha Waandishi wa Habari mkoani Mara MRPC, kimemfukuza uanachama wa chama hicho, mwandishi wa habari wa radio Free Afrika mkoani Mara Bw Maxmilian Ngesi baada ya kukiuka makubalino ya chama hicho yaliyofikiwa juzi ya kutoandika kabisa habari za jeshi la polisi mkoani humo.

Akizungumzia kufukuzwa kwa Mwandishi huyo mwenyekiti wa chama hicho  Bw Emmanuel Bwimbo,alisema kuwa Ngesi amekiuka makubaliano ya waandishi wenzake na chama kwa ujumla baada ya kusikika akitangaza habari za jeshi la polisi kwa kumkariri kamanda wa polisi wa mkoa wa Mara. 


 “ Sisi kwa kauli moja tumekubaliana kutofanya kazi na Jeshi la Polisi Mkoani Mara baada ya Matukio kadhaa likiwemo ya kuuawa kwa mwandishi wa habari mkoani Iringa na kutunyima kibali cha Maandamano yetu ya Amani kupinga Mauaji hayo” alisema Bw Bwimbo



Bw Bwimbo alisema kuwa kitendo hicho kinaonyesha jinsi gani mwandishi huyo alivyokiuka makubaliano ya pamoja na kuwasaliti wenzake ambao wamekubaliana kwa pamoja kuwa hawataandika habari za jeshi hilo kutokana na kuzuiwa waandishi kutoandamana katika maandamano ambayo yaliitishwa nchini kote kulaani kitendo cha mauaji ya mwandishi wa kituo cha chanel Ten mkoani Iringa Daud Mwangosi.

Alisema Ngesi  kama mwanachama alitakiwa kutii maamuzi ya chama na tamko la chama chake kwa vile tamko hilo limewataka wananchama wote na siyo kwa mkoa wa Mara tu lakini pia baadhi ya mikoa imetoa matamko na misimamo hiyo lakini cha kushangaza yeye amekaidi na kwenda kinyume.
Aidha Mwenyekiti huyo alisema  kamwe chama hicho hakiwezi kuvumilia mwandishi atakaye kiuka agizo hilo na hatua ambayo imechukuliwa kwa Ngesi ni  mfano kwa waandishi wengine hadi hapo tamko hilo litakapo tenguliwa.
 
 Akiongea kwa njia ya Simu na Mtandao huu,Mwandishi huyo alisema kuwa alifanya hivyo bila kuwa na taarifa zozote kama kuna msimamo wa chama katika kufanya kazi na Jeshi la Polisi mkoani Mara.

Bw Maximillian Ngessi alisema kuwa anajuti kwa hilo na uongozi wa Chama hicho cha Waandishi wa Habari Mkoani hapa kimefanya uamuzi huo kwa haki,aidha aliongeza kuwa anajutia kwa hilo kutokana na kutokuwa na taarifa zozote kutoka katika Chama hicho.

  "Ni kweli nimevuliwa uanachama lakini ni sahihi maamuzi hayo kwani nimekwenda kinyume na makubaliano ingawa nimetoa taarifa hiyo bila kuwa na taarifa zozote kutoka ofisini na pia najutia kwa hilo" alisema Bw Ngessi


Jumatatu wiki hii waandishi wa habari walifanya maandamano nchi nzima wakilaani mauaji ya mwandishi mwenzao Daudi Mwangosi  ambapo kwa mkoa wa Mara maandamano hayo yaliuzuiwa na polisi hali iliyofanya chama cha waandishi wa habari kukataa kuandika habari za jeshi hilo mkoani Mara.

No comments:

Post a Comment