Na Salum Vuai, Maelezo Zanzibar
WAANDISHI wa habari Zanzibar, wameaswa kufanya uchunguzi wa kina kabla
kuandika au kutangaza taarifa wanazopewa na vyanzo mbalimbali.
Wameelezwa kuwa, si kila jambo wanaloambiwa, kusikia au kuona, kulichukulia
kuwa ndiyo habari na kukimbilia kuitoa kwa umma.
Nasaha hizo zimetolewa na mwandishi wa habari mkongwe Salim Said Salim,
wakati akitoa mafunzo katika warsha inayofanyika katika ukumbi wa Idara
ya Habari Maelezo, juu ya namna ya kuandika habari kwa kuzingatia maadili
na haki ya kujibu.
Salim alifahamisha kuwa, mara mwandishi anapoambiwa jambo, hana budi
kulifanyia utafiti wa kina kabla kuliandika au kulirusha hewani, ili
kuepuka migogoro.
"Taarifa mnazopata kuhusu jambo lolote, liwe kama mbegu ya kutafuta
undani badala ya kukurupuka na kuandika, kwani watu wengine wanakuwa
na ajenda zao, ambazo zinaweza kukutieni kwenye matatizo", alifafanua.
Alisisitiza kuwa mwandishi anapaswa kufanya maamuzi sahihi kabla kushika
kalamu na kuandika taarifa anayoikusudia ili kujiepusha na kuwavunjia
watu heshima.
Aidha aliwataka kupima juu ya kile wanachokiandika, na kujiepusha
na habari zinazoweza kuwakashifu watu wengine mbele ya jamii kwa kuelezea
mambo yao ya ndani ambayo hayana faida yoyote kwao na jamii wanayoiandikia
zaidi ya kupandikza chuki na uhasama.
Akizungumzia juu ya matukio yanayopigwa picha, Salim alieleza kukerwa
kwake na jinsi wapiga picha wengi wasivyojali wala kuzingatia staha
ya mtu wanayempiga picha na hivyo kuijengea jina baya tasnia ya uandishi
wa habari.
Alitoa mfano kwa wapiga picha katika mchezo wa netiboli, kusubiri
sketi za wachezaji ziinuke, na kuona hapo ndipo pahala pa kupata picha
nzuri, akisema ni lazima wanawake wastahiwe kwani ni mama na dada katika
jamii inayowazunguka.
"Tusipendelee kuandika habari za kashfa hata kama ni za kweli
kwani pamoja na kuishi katika zama za uwazi na ukweli, lakini kila mtu
ana haki ya kuheshimiwa faragha yake", alieleza mwanahabari huyo
mkongwe.
Alisisitiza kuwa mwandishi anapaswa kufanya maamuzi sahihi kabla kushika
kalamu na kuandika taarifa anayoikusudia ili kujiepusha na kuwavunjia
watu heshima.
Alisema hata pale kunapokuwa na makosa yaliyofanywa na viongozi wakuu
wa nchi ambayo mwandishi nataka kuyabainisha, asitukie lugha ya kejeli,
dharau na kusuta, na badala yake atoe yaliyo moyoni mwake kwa njia nzuri
na lugha yenye staha huku lengo likiwa ni kufikisha ujumbe kwa muhusika
na jamii kwa jumla.
Mafunzo hayo ya siku nne yameandaliwa na Baraza la Habari Tanzania
(MCT) kupitia ofisi yake ya Zanzibar.
No comments:
Post a Comment